Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

KUFUZU AFRIKA :Soka la vijana lilivyoipeleka Tanzania fainali za Afcon 2019

48945 Pic+kufuzu

Wed, 27 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Hakuna njia ya mkato katika kuelekea mafaniko ya jambo lolote ambalo mwanadamu analifanya kwa malengo fulani.

Ndiyo kauli unayoweza kuitoa kuelezea mafanikio ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ambayo Jumapili ilifuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) baada ya kupata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Uganda kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Stars imefuzu fainali hizo baada ya kufikisha pointi nane ambazo hazikufikiwa na timu za Lesotho na Cape Verde ambazo zilitoka sare ya bila kufungana katika mchezo mwingine wa Kundi L uliochezwa Praia siku hiyo. Stars imeungana na Uganda, ambayo ni kinara wa kundi hilo, kwenda fainali hizo ambazo kuanzia mwaka huu zitashirikisha mataifa 24 ya Afrika. fainali hizo kubwa za soka barani Afrikazitafanyika Misri kuanzia Juni 21 hadi Julai 19.

Lakini mafanikio hayo ni hitimisho la safari ndefu. Ukitazama idadi ya nyota wanaounda kikosi cha Stars ambacho kimefanikisha Tanzania kuingia katika historia ya kufuzu kwa mara ya pili, utabaini ukweli kwamba ili mafanikio yapatikane ni lazima masuala kadhaa yafanyiwe kazi na si kwa njia za mkato kama ambavyo baadhi watu wanavyojiaminisha.

Soka la vijana ni miongoni mwa maeneo ambayo kama nchi ikifanya uwekezaji mzuri, tunaweza kufanikiwa zaidi.

Waliopitia soka la vijana

Hilo linajidhihirisha katika kikosi kilichofanikiwa kuiongoza Tanzania kufuzu AFCON kwa kuwa kundi kubwa kama si lote la wachezaji wake ni zao la uwekezaji kwenye soka la vijana.

Aishi Manula, Himid Mao, Simon Msuva, Gadiel Michael, Farid Mussa, Shaban Chilunda, Yahya Zaydi, Rashid Mandawa, John Bocco na Metacha Mnata wamepitia katika mfumo wa soka la vijana wa klabu ya Azam FC, wakati Hassan Kessy na Thomas Ulimwengu wao ni zao la kilichokuwa kituo cha soka Tanzania (TSA) ambacho kilikuwa chini ya usimamizi wa Shirikisho la Soka (TFF) wakati wa utawala wa Leodgar Tenga.

Erasto Nyoni ni matunda ya kituo cha Rollingstone cha Arusha kinachoendesha mashindano yaliyomfanya aonekane na kusajiliwa na Vital’O ya Burundi kabla ya kuhamia Azam.

Hakuna asiyependa sifa kwa kazi nzuri ambayo ameifanya na hilo linaweza kudhihirika kupitia kauli ya meneja wa Azam FC, Phillip Alando ambaye amekiri kufurahishwa na klabu yake kuwa chachu ya mafanikio ya Stars huku akiahidi kuendeleza kile walichokianzisha.

“Kwetu sisi Azam FC ni jambo la kujivunia kuona wachezaji waliopitia katika mikono yetu wakitoa mchango mkubwa kwa Taifa Stars,” anasema Alando.

“Lakini pia hili linatupa moyo na ari ya kuhakikisha tunawekeza zaidi kwenye soka la vijana ili nchi yetu izidi kupiga hatua.”

Hata wachezaji kama Mbwana Samatta, Jonas Mkude, Feisal Salum, Ally Mtoni na Aron Kalambo ni zao la timu za vijana.

Pia, kundi kubwa la wachezaji hao wamepita katika mikono ya timu za Taifa za Vijana ambazo zilipewa uzito mkubwa wakati wa utawala wa Tenga, chini ya kocha Mbrazili Tinoco na baadaye Kim Poulsen.

Pamoja na kufuzu, Tanzania ni kama imechelewa kuvuna matunda ya soka la vijana ambalo baada ya utawala wa Tenga, liliyumbishwa na programu ya Taifa Stars Maboresho ambayo hata hivyo hayakuweza kuzaa matunda, badala yake ilichangia upotevu wa fedha za maendeleo ambazo kama zingewekezwa vyema, leo hii Stars ingekuwa kwenye daraja jingine.

“Tunatambua wazi kwamba soka la vijana ndio moyo wa mpira wa miguu katika nchi yoyote na ndio maana akili na nguvu zetu kubwa tumeziweke hapo,” alisema Rais wa TFF, Wallace Karia.

“Na hilo unaweza kulithibitisha kupitia bajeti yetu tuliyotenga mwaka huu, ambayo fungu kubwa tumelielekeza kwenye miradi ya maendeleo, (hasa) soka la vijana na wanawake.”

Ligi bora

Eneo jingine ambalo linaweza kuwa chachu kwa soka la Tanzania kupata mafanikio kama kufuzu Afcon, ni Ligi Kuu ambayo kama itakuwa na ushindani na usimamizi bora, itachangia kutoa wachezaji wazuri ambao watakuwa na manufaa kwa timu ya taifa.

Tukiwa na ligi yenye ushindani ambayo itatoa nafasi kwa wachezaji wazawa kucheza mara kwa mara, tunaweza kupata kundi kubwa la wachezaji walio imara na wanaoweza kuisaidia nchi.

Kiwango bora cha wachezaji kama John Bocco, Erasto Nyoni, Kelvin Yondani na Aishi Manula ni matunda ya uzoefu na uimara ambao wachezaji hao wameupata kutokana na kucheza mechi nyingi za kiushindani kulinganisha na wengine na hii yote imechangiwa na klabu zao kupata nafasi ya kushiriki mashindano ya Afrika kwa ngazi ya klabu.

Ni vigumu kuzalisha kundi kubwa la wachezaji katika mazingira ambayo klabu zetu zinasajili kundi kubwa la wachezaji wa kigeni ambao wengi wao wana viwango vya chini ambavyo vinazidiwa na vile vya wazawa.

“Hatupingi ujio wa wachezaji wa kigeni, lakini basi wanapaswa wawe na kitu cha tofauti ambacho kitawafanya wachezaji wetu wa Kitanzania kujifunza kutoka kwao,” anasema kocha wa Stand United, Athuman Bilali ‘Billo’

Pia fursa ya kucheza soka la kulipwa nje ya nchi inaweza kutumika tu pale tutakapokuwa na wachezaji walioandaliwa vizuri udogoni.



Chanzo: mwananchi.co.tz