Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

KMC yatambia usajili kimataifa

65543 Kmc+pic

Fri, 5 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati KMC inatarajiwa kuondoka leo kwenda Kigali, Rwanda kucheza Kombe la Kagame, mambo manne yanaweza kuipa mafanikio katika mashindano ya kimataifa endapo yatafanyiwa kazi.

Mbali na kushiriki michuano ya Kombe la Kagame iliyopangwa kuanza Julai 7 hadi 21 mjini Kigali, KMC itacheza Kombe la Shirikisho Afrika.

Mambo manne yanayoweza kuiweka pazuri KMC katika ushiriki wake wa michuano ya kimataifa ni usajili, benchi la ufundi, bajeti ya kutosha na maandalizi mazuri.

Akizungumza jana, Meya wa Manispaa wa Kinondoni, Benjamini Sitta, alisema KMC inaondoka leo kwenda Kigali kushiriki Kombe la Kagame ikiwa na kikosi imara cha ushindani.

Sitta alisema wamezingatia mambo yote manne ambayo yataipa KMC mafanikio katika ushiriki wa Kombe la Kagame na Kombe la Shirikisho Afrika.

“Wachezaji 20 na makocha watano wanaondoka kesho (leo) kwenda Rwanda kushiriki Kagame. Michuano hii tunaipa umuhimu wa pekee kwa sababu ndio itatoa taswira ya ushiriki wetu wa Kombe la Shirikisho Afrika,” alisema Sitta.

Pia Soma

Meya huyo alisema wamefanya usajili wenye tija uliozingatia ripoti ya benchi la ufundi na wachezaji wote wakiwamo wapya wamepewa mkakati wa kutimiza malengo ya KMC.

Alisema baada ya kumnasa kiungo mshambuliaji raia wa Togo, Serge Alainnogue, waliyetarajia kumalizana naye jana, timu hiyo imefunga usajili wake rasmi.

Wachezaji wengine waliotua KMC ni kiungo, Kenny Ally, washambuliaji Vitalis Mayanga, Ramadhani Kapera na Salim Aiyee, mabeki Boniface Maganga, Abdallah Mfuko na Janvier Besala Bokungu (beki wa zamani wa Simba) kutoka DR Congo, kipa Aaron Kalambo na Amosi Charles.

KMC imeimarisha benchi la ufundi kwa kumnasa nyota wa zamani wa SC Villa ya Uganda, Jackson Mayanja aliyewahi kuzinoa Kagera Sugar na Coastal Union.

Mayanja ametua KMC kujaza nafasi ya aliyekuwa kocha mkuu Ettiene Ndayiragije aliyejiunga na Azam FC.

Sitta alisema wana imani kubwa na Mayanja ataipa mafanikio KMC katika mashindano mbalimbali ikiwemo Kombe la Kagame na Shirikisho Afrika.

Mayanja alisema ndoto yake ni kufanya vyema katika mashindano ya kimataifa na Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.

“Vijana wana morali bila shaka tutafanya vizuri, tumejiandaa na hatuna hofu licha ya kushiriki mashindano ya kimataifa kwa mara ya kwanza,” alisema Mayanja.

Akizungumzia bajeti ya KMC, Sitta alisema wako katika mazungumzo na baadhi ya wadau ambao wameonyesha dhamira ya kuwapa udhamini.

“Baadhi ya wadau wameonyesha nia ya kuidhamini timu yao pia wapo wanaotuchangia kwasababu bajeti ya halmashauri pekee haitoshi,” aliongeza Sitta.

Meya huyo alisema hakuna njia ya mkato KMC kupata mafanikio katika mashindano yake, hivyo wamejiandaa kuipa maandalizi ya kutosha timu.

Chanzo: mwananchi.co.tz