Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

KMC na Lipuli yatinga nusu fainali Kombe la Shirikisho

49068 Simbapic

Thu, 28 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. KMC na Lipuli ya Iringa zimetinga nusu fainali za michuano ya Kombe la Shirikisho baada ya kushinda mechi zao za leo na sasa zinawasubiri vigogo Yanga SC, Azam na Kagera Sugar pamoja na timu mpya ya Alliance kuamua wapinzani wao wawili.

Ushindi wa mabao 2-0 ambao KMC waliupata mbele ya African Lyon umeiwezesha timu hiyo ya manispaa kufika nusu fainali za FC, huku Lipuli ikiifuata baada ya kupata ushindi wa bao 2-0 dhidi ya Singida United.

Yanga, ambayo inaongoza Ligi Kuu, itakuwa ikisaka nafasi ya kucheza nusu fainali Jumamosi kwenye Uwanja wa CCM Kirumba itakapoivaa Alliance, timu iliyopanda daraja msimu huu baada ya jitihada za miaka kadhaa tangu ainzishwe kama kituo cha soka la vijana.

Azam, mabingwa wa zamani wa michuano hiyo, watatakiwa kuitangulia Yanga au Alliance watakapoivaa Kagera Sugar, mchezo unaotarajiwa kuwa mkali na wa kuvutia.

KMC, inayoshika nafasi ya tano katika msimu wake wa kwanza Ligi Kuu Bara, ilionekana pia kuwa na nia ya kufanya vizuri katika michuano ya mtoano, ikitangulia kupata bao katika dakika ya 47 lililofungwa na Mohamed Rashid, anayechezea klabu hiyo kwa mkopo akitokea Simba.

Rashid alimchambua vizuri kipa Lyon baada ya kukimbilia pasi mbele ya lango la wapinzani wao.

Cliff Buyoya alihitimisha ushindi huo wa Kinondoni katika dakika ya 88 na kuipa timu hiyo tiketi ya kucheza nusu fainali kwa mara ya kwanza.

 Kocha wa KMC, Ettiene Ndayiragije alifurahishwa na jinsi wachezaji walivyofuata maelekezo yake, lakini akaangalia hatua inayofuata.

"Kila hatua ni ngumu. Tunasubiri tutacheza na nani baada ya michezo iliobaki kati ya Yanga na Alliance, Azam FC na Kagera Sugar,” alisema kocha huyo Mrundi.

“Tunajipanga kuhakikisha tunafikia malengo ya ubingwa."

Mjini Iringa, wenyeji Lipuli walitumia vizuri uwanja wa nyumbani walipoibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Singida United, ambayo imekuwa ikiyumba tangu ilipokimbiwa na kocha wake Hans Pluim.

Jimmy Shoji aliitanguliza timu hiyo katika dakika ya 33 alipofunga bao la kuongoza kabla ya mchezaji wa zamani wa Simba, haruna Shamte kupigilia msumari alipofunga bao la pili kwa njia ya penati katika dakika ya 90.

“Haya ni mafanikio makubwa,” alisema kocha wa Lipuli, Selemani Matola baada ya mchezo huo.

"Hii ni michuano ambayo tumewekeza nguvu kuhakikisha tunashiriki michuano ya Shirikisho Afrika mwakani kama ilivyokuwa kwa Mtibwa Sugar."

Bingwa wa michuano hiyo atakata tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika mwakani.



Chanzo: mwananchi.co.tz