Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

KMC, Azam mechi ya kisasi leo

73111 Kmc+pic

Tue, 27 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Baada ya kutolewa katika mashindano ya kimataifa, KMC inarejea katika Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini inakutana na kigingi kingine kwa Azam FC, leo.

Timu hizo zitavaana katika mchezo unaomrudisha nyumbani Kocha Etienne Ndayiragije aliyeinoa KMC msimu uliopita na kuipa tiketi ya kucheza Kombe la Shirikisho Afrika.

KMC ilitolewa na AS Kigali ya Rwanda katika Kombe la Shirikisho Afrika kwa kufungwa mabao 2-1 wakati Azam FC ilishinda 3-1 dhidi ya Fasil Kenema ya Ethiopia na kufuzu.

Timu hizo zinakutana zikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare katika mechi zote mbili za msimu uliopita. Katika mzunguko wa kwanza zilitoka sare ya mabao 2-2 kabla ya kutoka suluhu ziliporudiana.

Ndayiragije mwenye falsafa ya kutumia zaidi vijana tangu akiwa Mbao FC na KMC, alisema haitakuwa mechi rahisi licha ya kuwahi kuwanoa wapinzani wake.

“Utakuwa mchezo wa ushindani. Kweli nimetoka kule na wachezaji wengi nawafahamu lakini hiyo haimaanishi mchezo utakuwa rahisi kwa upande wetu kwani mpira ni mbinu.

Pia Soma

“Hata wao wanaweza kuja tofauti na vile ulivyowaona mchezo uliopita wa kimataifa dhidi ya AS Kigali, lakini tumejipanga kuwakabili na kuhakikisha tunapata pointi tatu,” alisema Ndayiragije alipozungumza jana Jumatatu.

Wakati Ndayiragije akisema mechi hiyo haitabiriki, kocha wa KMC ambaye ni nyota wa zamani wa SC Villa ya Uganda, Jackson Mayanja alisema anataka kushinda.

“Mashindano ya kimataifa yametupa uzoefu licha ya kutoka mapema. Tunarejea kuikabili Azam moja ya timu nzuri hapa nchini, hivyo ni lazima tujipange. Nina furaha kurejea kwa wachezaji wangu waliokuwa majeruhi,” alisema Mayanja.

Rekodi

Katika michezo mitano iliyopita Azam FC imeshinda minne na kupoteza mmoja wakati KMC ilishinda mmoja, ilipoteza miwili na kutoa sare mara mbili.

Azam FC iliifunga TP Mazembe ya Congo mabao 2-1, ilitoka suluhu dhidi ya Maniema Union, iliifunga KCCA ya Uganda bao 1-0, ilichapwa 1-0 na Fasil Kenema ya Ethiopia kabla ya kushinda 3-1.

KMC ilitoka sare ya bao 1-1 na Atlabara ya Sudan Kusini, ilifungwa bao 1-0 na TP Mazembe, iliifunga Rayon Sports ya Rwanda 1-0, ilitoka suluhu dhidi ya AS Kigali ya Rwanda kabla ya kuchapwa mabao 2-0 ziliporudiana.

Chanzo: mwananchi.co.tz