Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

KCB yamwaga noti Ligi Kuu Bara

9323 Kcb+pic TanzaniaWeb

Wed, 1 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Benki ya KCB, imetia saini mkataba na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa ajili ya udhamini wa Ligi Kuu Bara kwa Sh420 milioni.

Mkataba huo uliwekwa saini na Rais wa TFF, Wallace Karia na Mkurugenzi Mtendaji wa KCB, Cosmas Kimario katika hafla iliyofanyika Hoteli ya Serena, Dar es Salaam jana.

Benki hiyo imeboresha udhamini wake baada ya mwaka jana kutia saini mkataba wa msimu mmoja wenye thamani ya Sh325 milioni.

Akizungumza katika hafla hiyo, Kimario alisema benki hiyo ni wadau wa maendeleo ya michezo nchini hasa mpira wa miguu.

Kimario alisema msimu uliopita walipata mafanikio katika udhamini huo, hivyo wameamua kuendelea kudhamini mashindano hayo msimu ujao.

“Tumefarijika na udhamini wa msimu uliopita, Ligi Kuu Tanzania Bara ilikuwa na ushindani mkubwa pia tunafikiria kudhamini Ligi Daraja la Kwanza na Ligi ya Wanawake endapo tutafikia makubaliano,” alisema Kimario.

Klabu 20 zinazoshiriki Ligi Kuu kila moja itapata Sh15 milioni na fedha nyingine zitatumiwa katika shughuli mbalimbali za ligi.

Kwa upande wake Karia alisema wanaendelea na mazungumzo na benki hiyo kuona uwezekano wa kudhamini ligi nyingine nchini.

“Kama nilivyosema lengo la TFF ni kupunguza makali kupitia wadhamini tumepata Benki ya KCB na sasa tunaendelea na wadhamini wengine, ligi yetu ni ndefu na timu zinahitaji fedha za kutosha tunatoa wito kwa klabu kuendelea kutafuta fedha za kusaidia uendeshaji,” alisema Karia.

Naye Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi (TPLB), Boniface Wambura aliziomba klabu zinazotarajia kupata wadhamini kuwasilisha mikataba ili kuondoa mkanganyiko endapo TFF itapata mdhamini mkuu ambaye ni mshindani na mdhamini wa klabu husika kwa kuwa kanuni za udhamini zinakataza.

Chanzo: mwananchi.co.tz