Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jellah Mtagwa: Nahodha Taifa Stars anayeteseka kwa miaka 15 kitandani

59913 Pic+jellah

Tue, 28 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

“Acheni Mungu aitwe Mungu”. Hiyo ni kauli ya aliyekuwa nahodha wa timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ iliyoshiriki fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) mwaka 1980, Jellah Mtagwa.

Jellah anasema anateseka kwa maradhi kwa miaka 15 mfululizo, mkewe Mboni Ramadhani na watoto wake walikata tamaa, lakini Mungu amemsimamia.

Anasema anatamani kunyanyuka na kutembea, lakini miguu haina nguvu tena, si Jellah yule aliyekuwa beki na nahodha tegemeo wa Taifa Stars kwa miaka 10 mfululizo tangu mwaka 1974.

Si kutokana na sababu ya umri mkubwa wa nguli huyo, la hasha ni maradhi ambayo yamemlaza kitandani mpaka sasa.

Tatizo lilivyoanza

Mkewe anakumbuka ilikuwa mwaka 2004 ambapo waliletewa taarifa kuwa Jellah Mtagwa amedondoka barabarani.

Pia Soma

“Mzee alikuwa na nguvu vizuri tu, aliondoka nyumbani kwenda Kisutu sokoni kwenye shughuli za kawaida,” anasimulia Mboni.

Anasema wakiwa katika hekaheka za kufuatilia, mara walimuona akiletwa nyumbani na watu waliomsaidia, lakini akionekana kuwa mgonjwa.

“Tulimpeleka hospitali ambako alipimwa na kugundulika ana presha na tatizo la kupooza mwili, alianza matibabu, lakini hali yake ilizidi kuwa mbaya, alipopimwa zaidi ikaonekana pia ana tatizo la kisukari,” anasema.

Wakati mkewe akisimulia hayo, Jellah alikuwa akimsikiliza kwa makini na kutikisa kichwa, huku akijitaidi kuonyesha tabasamu hafifu ambalo lilimezwa na hali ya ugonjwa unaomkabili.

Licha ya kuumwa kwa muda mrefu, Jellah hajapoteza kumbukumbu, anakumbuka namna alivyojitoa katika timu ya Taifa, anasema asilimia 80 ya maisha yake yalikuwa mpira, lakini haukumnufaisha.

“Hata wanangu walikuwa hawanifahamu wakati ule, sikupata muda wa kuwa nao, muda mwingi nilikuwa kambini ndani ya mwezi mmoja, kama nilikaa nyumbani sana basi ni siku tano, nyingine zote nakuwa kambini au katika mechi.

“Muda mwingi niliutumia kwenye mpira, kama sio Stars, basi Yanga au Pan African ambako nilicheza baada ya kuondoka Yanga,” anasema.

Maisha ya Soka

Nguli huyo anasema amekuwa nahodha wa Taifa Stars kwa miaka 10 mfululizo na alianza kucheza akiwa shule ya sekondari.

Anasema maisha yake ya soka yalianzia Shule ya Msingi Mwembesongo mkoani Morogoro kisha akaendeleza kipaji chake akiwa Shule ya Sekondari Moro.

“Tangu nikiwa Moro Sekondari kipaji changu kilionekana kwenye mashindano ya shule, nikaanza kuitwa timu ya Taifa wakati ule nahodha alikuwa Zimbwe Omari ambaye baadaye alinikabidhi unahodha.

Akiwa Moro Sekondari, ndipo alipokutana na Leodeger Tenga, rais wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) aliyekuwa akisoma Kibaha na walikutana kwenye mashindano ya shule. “Tenga ndiye mtu ambaye tumecheza pamoja tangu ujana,” anasema Jellah.

Anasema wakati ule kulikuwa na ‘skauti’ nzuri ya wachezaji na yeye alijiunga na Yanga baada ya kuonekana katika michuano ya Kombe la Taifa.

“Nilipohitimu sekondari nilichezea Nyota Afrika ya Morogoro, pia nilikuwa miongoni mwa wachezaji wa Morogoro kwenye Taifa Cup, hapo ndipo Yanga waliponiona na kunichukua,” anaeleza.

Anasema hakudumu Yanga, kwani aliichezea kwa miaka miwili, ukaibuka mgogoro ambapo wachezaji tisa walifukuzwa.

“Kocha wa Yanga wakati ule (Tambwe Leah) alikuwa na nguvu, alitaka kuwafukuza wachezaji wanne, wengine tukagoma, hivyo sote tukaingizwa katika mkumbo ule.

“Siku tunafukuzwa, mashabiki walijaa Jangwani kuona kama ni kweli. Kocha akatamka kwamba tusipoondoka sisi basi yeye atarudi kwao Zaire (sasa DRC), alikuwa na nguvu hivyo tukafukuzwa na kwenda kuanzisha Pan African,” anasimulia.

Taifa Stars, Afcon 1980

Jellah anasema tukio kubwa ambalo hatasahau ni heshima waliyopewa wakiwa kwenye ziara ya soka nchini China.

“Tulikwenda kwa ziara ya mwezi mmoja, tukiwa kule, Kiongozi mashuhuri wa China, Mao Tse Tung alifariki mwaka 1976.

“Diplomasia wakasema nchi zitawakilishwa na watu wao walioko kule, hivyo kwa Tanzania Taifa Stars ndiyo tulipewa fursa hiyo, nikiwa nahodha,” anasema Jellah.

Anasema pamoja na kwamba ulikuwa msiba mzito kwa China, lakini heshima waliyopewa Taifa Stars ilikuwa ya kipekee katika kutoa heshima za mwisho kwa kiongozi huyo wakiongozwa na Balozi wa Tanzania nchini China wakati ule (Balozi Job Lusinde).

Jellah akikumbuka walivyoianza safari ya Afcon 1980, anasema waliifunga Kenya, kuitoa Zambia na kufuzu.

“Zambia walitudharau wakati ule nchi yao ilikuwa vizuri, tulipowafunga 1-0 Dar es Salaam, walijua wameshinda, waliapa tukienda kwao Zambia hatutoki.

“Mechi ya marudiano ilichezwa Ndola, siku tulipofika Uwanja wa Ndege wa Ndola, ilikuwa ni shamrashamra kwa kila Mzambia, wengine walituonyesha vidole vinne, wengine vitatu, ilimradi kila shabiki kule alijua tutafungwa,” anasema.

Anasema siku ya mechi, kila mmoja alikuwa anawaza ni namna gani ataisaidia Taifa Stars kushinda, wenzao walikuwa wakirushiwa funguo za magari, rais wao wakati huo (Keneth Kaunda) alikuwa uwanjani kuwahamasisha.

“Zambia ilikuwa na wachezaji hatari wa mpira, mechi ilipoanza nilikaba hadi kuna wakati nilihisi kizunguzungu, tulishambuliwa na mashuti ya nguvu.

“Kuna moja lilipigwa, nikaona isiwe tabu nikalipisha, ila kwa aibu nikajifanyisha kama nafunga kamba za viatu, nikasikia Pondamali (Juma, aliyekuwa kipa) anapiga kelele kuniambia kaka Jellah hiyo umekwepa.

“Kwanza nilijua ni goli, nilipogeuka nikakuta Pondamali ana mpira kifuani, nikamwambia nisamehe mdogo wangu hapo nilizidiwa,” anasimulia Jellah.

Anasema “kila mchezaji wa Taifa Stars aligangamala, kwani mmoja akicheza vizuri, wote wanacheza, akiharibu basi ni wote, timu nzima ilikuwa na hamasa kutoka moyoni”.

Anasema goli la Peter Tino lilianza kupigiwa kelele wakati akiambaa na mpira katikati ya uwanja akiwa amewazidi mbio mabeki na kubaki na kipa baada ya kupokea pasi ya Hussein Ngurungu.

“Tino alitaka kupiga ule mpira akiwa katikati baada ya kuona kipa ametoka kumfuata, tukamwambia bado uko mbali…sogea tena Tino.

“Tulifanya hivyo kama mara tatu na mara ya nne tukamwambia piga sasa uko karibu, lakini ilikuwa ni tukio la haraka likatupa bao la kusawazisha dakika za lala salama kabla ya mechi kumalizika.

Anasema uwanja mzima ulinywea, rais Kaunda ambaye alikuwa akipeperusha kitambaa cheupe hewani, alikaa chini, furaha ikabaki kwa mashabiki wachache wa Stars baada ya kukata tiketi ya kucheza Afcon kwa jumla ya mabao 2-1.

Kilichotokea Nigeria

Baada ya kufuzu, Jellah anasema walikwenda kuweka kambi Mexico kujiandaa na fainali hizo zilizofanyika Lagos, Nigeria.

Taifa Stars ilipangwa kundi moja na Nigeria, Ivory Coast na Misri timu ambazo zinafanya vizuri mpaka sasa Afrika. “Tungefika mbali kwenye yale mashindano, lakini tulifungwa kwa ushamba, pia kuna mmoja wetu (anamtaja jina) alituhujumu na nilimwambia,” anasema.

Anasema mechi na Nigeria walifungwa 3-1 lakini kwa tabu, ila baadae ikagundulika mmoja wao huyo aliwahujumu.

“Baada ya mechi tulikaa kikao cha wachezaji, kwenye vikao kama hivyo, makocha zamani tulikuwa tunawaomba watupishe, nikamsema (mchezaji aliyetuhumiwa), akaomba radhi, ila nikamwambia kabisa wewe mechi zilizobaki huchezi.

“Nilipanga kikosi cha mechi inayofuata usiku ule ule,” anasema.

Anasema katika kikosi hicho, alimwambia Ahmed Amasha ambaye alikuwa mdogo sana kwenye timu kuwa atacheza namba tatu na Adolph Rishard namba mbili.

“Hizo hazikuwa namba zao, lakini kwenye timu yetu tulikuwa tunasikiliza mno, vijana walicheza na matokeo yaliyofuatia pamoja na kwamba tuliishia makundi, lakini tulipambana,” anasimulia.

Amenufaika vipi na mpira?

Pamoja na kujitoa kwa asilimia kubwa ya maisha yake katika kuitumikia Stars, Yanga na Pan African, Jellah anasema alicheza kwa mapenzi na hakupata fedha ambayo leo anaweza kujivunia kuwa imetokana na kipaji chake cha mpira.

Maisha ya Jellah ni ya kawaida ambayo hata nyumba anayoishi eneo la Manzese, Dar es Salaam, mvua ikinyesha maji yanajaa ndani.

“Natamani kujenga nina kiwanja Mkurunga, lakini kabla ya kuanza ujenzi ndipo nikaanza kuugua, hivyo sijaweza kufanya jambo lolote.

“Hii nyumba ninayoishi sasa, mvua ikinyesha maji lazima yaingie ndani, kuna watu wanaweza kuuliza fedha ya mpira nimeitumia vipi, lakini kiukweli sikuambulia chochote katika maisha yangu ya mpira,” anasimulia.

Picha yake katika satempu za Posta

Miongoni mwa mastaa ambao picha zao zilitumika kwenye stempu ni Jellah ambaye anasema hakujua hata mkataba au makubaliano ya picha yake kutumika kwenye stempu yalifanywa na nani.

“Nilistukia tu picha yangu iko katika stempu, nilianza harakati za kufuatilia kujua, nilikwenda ofisi za FAT (sasa TFF) mara mbili bila mafanikio,” anasema.

Anasema Mwenyekiti wa FAT wakati ule, Said El-Maamry mara ya kwanza alimueleza kwamba, picha yake imetumika kwenye stempu kwa sababu ya kipaji chake.

“Niliondoka lakini sikuridhika, nikarudi tena mara ya pili mwenyekiti akaniambia hulipwi na hakuna chochote unachopewa eti kwa kuwa picha yako imetumika kwenye stempu. Sikunufaika na chochote mpaka leo,” anasema.

Familia yake

Nyumbani kwa Jellah, watoto wake wote wanne wanafuatilia mpira hadi mama yao huku mtoto pekee wa kiume kwenye familia hiyo akifuata nyayo za baba yake.

Familia hiyo yenye haiba ya ucheshi, imehifadhi kumbukumbu za baba yao enzi akiwa mchezaji nyota, lakini wanapata simanzi wanapokumbuka namna walivyopambana kama familia katika kupigania afya ya baba yao.

Binti wa Jellah, Mariam Mtagwa anasema ilifikia mahali walikata tamaa ya kuendelea kumuona mzee wao akiwa hai.

“Baba hakuwa na bima ya afya kwa muda mrefu tangu apatwe na maradhi, miaka minne iliyopita ndipo tulipofanikiwa kumpatia bima ya afya,” anasema.

Anasema mwanzoni alipoanza kuugua, kuna msamaria mwema ambaye hawakumtaja jina alijitolea kugharamia matibabu yake katika Hospitali ya Agha Khan.

“Afya ya mzee ilianza kuimarika, lakini siku moja ilibadilika ghafla, familia hatukuweza kumpeleka Agha Khan, hivyo tukampeleka Mwananyamala.

“Ilikuwa siku ngumu mno kwetu, baba alikuwa haelewi chochote, tulihangaika usiku kucha, hadi asubuhi ilitugharimu Sh600,000 za matibabu, alfajiri saa 11 ndipo kwa mbali akaanza kuonyesha matumaini.

“Hali ile ilitufunza jambo kwamba, kama tusingekuwa na kiasi kile cha fedha, huenda leo tungekuwa tunazungumza mengine,” anasema.

Anasema familia imekuwa ikimhudumia baba yao kwa kujichangisha ili kupata matibabu kwani kwa miaka 11, matibabu ya Jellah yalikuwa ya kulipia fedha taslimu.

“Tulipambana hadi hapa mzee alipofikia. Mbali na presha na kiharusi, kisukari nacho kikaanza kumtesa zaidi, hasa kwenye vyakula, ilitubidi kuwa makini sana ili kumuona mzee anaendelea kuishi,” anaeleza.

“Nakwenda klikini mara tatu kwa wiki, bado nakuwa na changamoto ya kufika kiliniki, siwezi kutembea mwenyewe, siwezi kufanya kitu chochote pasipo usaidizi wa mtu mwingine,” anasema Jellah.

Asimulia ugumu uliokuwepo kucheza Simba

Jellah licha ya changamoto anazopitia, lakini anakumbuka namna ilivyokuwa ngumu mchezaji wa Simba kuhamia Yanga, vivyo hivyo wa Yanga kwenda Simba enzi zao.

“Simba na Yanga ilikuwa kama dini, lazima ufanye kazi ya ziada kutoka kwenye Uislamu kwenda katika Ukirsto au kutoka kwenye Ukristo kuhamia Uislamu.

Anasema hata mashabiki walikuwa hawakubali mchezaji wa Yanga kuchukuliwa na Simba.

Hata hivyo, Jellah anasema katika maisha yake ya mpira alimpenda sana mshambuliaji nyota wa Simba enzi zao, Zamoyoni Mogella. “Mogella alikuwa na akili ya mpira, nakumbuka kuna bao alitufunga katikati ya uwanja wakati ule nacheza Pan, lilikuwa goli zuri sana ambalo hadi leo siwezi kulisahau,” anasema.

Alivyodumu miaka 10 akiwa nahodha

Jellah anasema alijitunza kwa kuepuka anasa, alijituma na kila kocha aliyekuwa akiletwa Stars, Yanga na Pan alimpendekeza kuwa nahodha. “Starehe yangu ilikuwa kwenda Makwizi (bendi ya muziki) na mke wangu basi, lakini kipindi kingine chote nilikuwa mazoezini na kambini.

Chanzo: mwananchi.co.tz