Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

JICHO LA MWEWE: Nilienda kumtazama Chama, nikamkuta Mzamiru

82123 Chama+pic JICHO LA MWEWE: Nilienda kumtazama Chama, nikamkuta Mzamiru

Tue, 29 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

MPIRA wetu bwana! Jumatano iliyopita nikajivuta kwenda Uwanja wa Taifa kuitazama Simba. Sikuwa nimeiona kwa muda mrefu. Ilikuwa inacheza dhidi ya Azam FC. Wachezaji wakubwa huwa wanatamba mechi kubwa.

Nilienda kumtazama mchezaji anayeitwa Clatous Chota Chama. Mara ya mwisho nilienda Uwanja wa Taifa alinikosha sana. Kabla yake nilikuwa nimesusa kwenda uwanjani kwa sababu mchezaji aliyekuwa ananihamasisha nikamtazame, Thaban Scara Kamusoko alikuwa majeruhi na alikuwa amepotea.

Chama akanirudisha uwanjani kwa pasi zake maridadi. Maono yake ya mpira ya hali ya juu. Achilia mbali lile bao lake la kisigino katika pambano dhidi ya Nkana Red Devils. Lilinikumbusha bao fulani ambalo Hamis Thobias Gaga akiwa na jezi ya Simba aliwahi kuifunga Pamba ya Mwanza mwanzoni mwa miaka ya 1990.

Simlaumu hata rafiki yangu Haji Manara ambaye alikuwa anaongoza kwa kumsifia Chama. Binafsi nilikuwa namuelewa kwa sababu Chama alikuwa anakushawishi utapike sifa zote dhidi ya kiungo mkamilifu ambaye umewahi kumuona.

Chama alianzia benchi. Akaingia katika kipindi cha pili. Kuanzia kwake benchi nasikia kulichangiwa na nidhamu yake mbovu nje ya uwanja. Alipoingia nikashangaa jinsi alivyoifanya Simba ionekane ikiwa na wachezaji pungufu. Alipoteza karibu kila mpira aliopasiwa. Hakuwa na kazi na wala hakuweza kulinda mpira aliopasiwa.

Mtu mwingine ambaye nilipenda kwenda kumtazama alikuwa ni kiungo mrefu wa kimataifa wa Sudan, Shiboub Sharaf. Alitolewa wakati wa mapumziko. Alikuwa na siku mbaya kazini. Huyu siwezi kumfananisha na Chama kwa sababu sijasikia kama ana mambo mengi nje ya uwanja. Huenda tu hakuwa na siku nzuri kazini. Baada ya wote hao kuniangusha macho yangu yakaangukia kwa mtu aliyeitwa Mzamiru Yassin. Alikuwa na mapafu ya mbwa. Alikuwa injini ya Simba. Alikuwa kila kitu katika eneo la kiungo cha Simba hasa katika siku ambayo Jonas Mkude alikuwa jukwaani pia.

Pia Soma

Advertisement
Hapa katikati Mzamiru alishapotea. Sijui kama ni kwa tabia zake binafsi au hulka ya mashabiki wetu kupenda wachezaji wapya. Aliletewa wachezaji wengi katika nafasi yake ya kiungo aliletewa wachezaji wa ndani kama kina Hassan Dilunga na wa nje hawa kina Chama, Haruna Niyonzima na Shiboub. Nilidhani siku zake zilikuwa zinahesabika Simba.

Hata hivyo, kwa Mzamiru niliyemuona majuzi nadhani amezaliwa upya au amejitafakari. Alihaha uwanja mzima kwa dakika zote. Alikaba vema, alisambaza mipira vema, wakati mwigine alikokota na mpira kwenda nao mbele kiasi kwamba kuna wakati alileta utata wa penalti baada ya kuangushwa na wachezaji wa Azam katika boksi.

Hapa kuna mambo mawili. Tunaanza na Chama. Kwanini wachezaji wengi wa kigeni mahiri wanaotua nchini huwa wanaanza na moto kisha wanapoa? Nchi ina mambo mengi hii, hasa kwa Jiji la Dar es salaam. Wachezaji wanafurahia maisha kama wale wa Brazil.

Wachezaji wanatua wakiwa na nafsi za ushindani lakini wale wa timu kubwa huwa wanapoa wanapogundua kuna wepesi wa kushinda mechi hasa za ligi ya ndani. Lakini pia wanagundua kwamba ukifanya mambo makubwa siku za mwanzo basi ushindani wa nafasi unakuwa mdogo. Nidhamu inapungua.

Kinachokera ni kwamba wanalipwa mishahara mikubwa kuliko wazawa lakini zipo nyakati ambazo wachezaji wa kigeni ndio wanaongoza kwa nidhamu mbovu kambini badala ya kuonyesha thamani yao kwanini wanalipwa pesa nyingi.

Wanapopungua ndipo mchezaji kama Mzamiru anaporudi kwa kasi kuchukua nafasi yake. Kwa mfano, naamini kama Mkude angeanza, huku pia Chama akiwa katika ubora wake na Shiboub akiwa katika ubora wake basi Mzamiru asingeanza. Ameanza na ametumia nafasi.

Kama tatizo binafsi lilikuwa kwake Mzamiru, kwanini amesubiri mpaka apate changamoto kubwa kama hii ya kuletewa watu wazito katika nafasi yake ndipo achangamke? Hili ndio tatizo kubwa la wachezaji wetu. Wakati mwingine sio wachezaji wa ndani tu, bali hata wale wa nje ya nchi.

Kitu kikubwa ninachosubiri kutoka kwa Mzamiru ni kumuona akizomewa na mashabiki pale anapokosea kidogo tu uwanjani. Wakati mwingine hilo ndio tatizo letu. Akikosea Mzamiru mashabiki wanamtoa uwanjani kwa maneno machafu. Akikosea Shiboub basi hakuna tatizo. Huwa tunawakariri wachezaji.

Vinginevyo Mzamiru ashikilie palepale aliposhikilia mara ya mwisho nilipomuona Jumatano iliyopita katika pambano dhidi ya Azam. Alikuwa bora kuliko wachezaji wengi uwanjani. Ana nguvu nyingi katika mwili wake ambao wachezaji wengi wa Kitanzania hawana. Kucheza kwa kasi ile na kwa nguvu ile kwa dakika 90 katika pambano kama lile sio kitu cha masikhara.

Na ni wachezaji hawahawa ndio ambao tunawategemea katika michuano ya Chan pale Cameroon Februari mwakani. Hatuna wengine. Kama wao wanashindwa kuwa bora katika ligi basi hakuna wachezaji wengine ambao wanaweza kutuondolea aibu katika michuano ya Chan. Hakuna.

Chanzo: mwananchi.co.tz