Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

JICHO LA MWEWE: Mbabe wa Ibrahim Ajibu anatukumbusha sehemu tulipo

77935 Ajib+pi

Tue, 1 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

VIDEO iliyomuonyesha staa wa Kagera Sugar, Zawadi Mauya akimpiga kiungo wa Simba, Ibrahim Ajibu mateke ya ovyo, ya hasira, ya kijinga, ilisambaa mitandaoni wikiendi hii iliyoisha jana. Iliwashangaza wengi kisha ikashtua kidogo. Sikushtuka.

Ilituonyesha tulipo. Ilituonyesha jinsi wachezaji wetu walivyo. Ilituonyesha jinsi ambavyo tuna safari ndefu katika soka. Yule Zawadi ni mchezaji wa kulipwa ambaye anaishi kwa ajili ya soka lakini alikuwa akifanya vile.

Kwanza kabisa kuna mambo mawili. Katika video hauwezi kuona kosa la Ajibu. Alikuwa anakokota mpira vema na kujaribu kuonyesha uhodari wake. Lakini labda kabla ya hapo Ajibu alikuwa ametoa maneno ya kuudhi kwa Zawadi na hivyo akapandisha hasira. Bado haiwezi kukubalika.

Mwanasoka wa kulipwa (professional footballer) anapaswa kuonyesha uweledi wake katika kazi yake (Professionalism). Ni jambo la kawaida katika soka kwa mwanasoka kuudhiwa. Anachopaswa ni kuhimili hasira zake ili asiigharimu timu yake. Mara nyingi wenzetu wamekuwa wakituonyesha hivyo. Uwezo wa kuhimili hasira.

Bahati nzuri kwa Zawadi alikutana na mwamuzi mzembe. Inawezekana vipi akampigia mchezaji mwenzake mateke matatu halafu mwamuzi akatoa kadi ya njano? Vinginevyo angepewa kadi nyekundu ambayo kwanza ingeigharimu timu yake katika pambano husika, lakini pia katika mechi inayofuata au mechi zinazofuata.

Jambo la pili la kawaida kabisa ni kwamba inawezekana Ajibu hakutoa maneno machafu kwa Zawadi lakini Zawadi alikuwa ameudhika na matokeo yaliyokuwa yakiendelea katika mechi. Bado mchezaji unapaswa kuonyesha uweledi wa kazi yako na kuhimili hasira.

Pia Soma

Advertisement
Nje ya hapo unajaribu kuwaza mambo mengine mawili. Jinsi ambavyo mchezaji alikuwa akicheza rafu za ‘kisela’. Tunawaelewa wachezaji wanaocheza rafu mbaya za kunyemelea. Inakuaje Zawadi anacheza rafu za kitoto badala ya kunyemelea na kucheza rafu ya ‘kiutu uzima’? Alikuwa akicheza rafu kama vile yuko katika pambano la shule ya mbili za msingi.

Hapohapo Zawadi anatukumbusha jinsi ambavyo wachezaji wetu wa kileo wasivyo na ‘afya njema’. Inakuaje anapiga mitama mitatu bila ya kumuangusha mchezaji anayemchezea rafu? Hasa pale tunapokumbuka kwamba mchezaji mwenyewe ni Ibrahim Ajibu ambaye amekuwa akisifika kwa ‘uvivu wa mazoezi’.

Hii ilikuwa inaonyesha wazi kwamba kulikuwa na pengo kubwa la stamina kati ya wachezaji wa Kagera Sugar na wale wa Simba. Haishangazi sana kwa sababu mara nyingi huwa tunaona wachezaji wa Simba, Yanga na Azam wakiwa katika vyumba vya mazoezi ya viungo (gym) na si wachezaji wa klabu nyingine. Kumbe picha za magazeti hazidanganyi.

Hapo hapo unahoji jambo jingine. Kwanini wanasoka wa kulipwa huwa wanajizuia kufanya mambo ya kijinga? Ni kwa sababu wanajua kwamba mechi huwa zinaonyeshwa katika televisheni. Ina maana mpaka leo tuna wanasoka wa aina ya Zawadi ambao hawahofii kufanya ujinga mbele ya kamera za televisheni?

Ina maana Zawadi alikuwa hajui kwamba mechi inaonyeshwa moja kwa moja na kituo cha Azam TV? Ina maana alikuwa hajui ujinga wake ungekuwa unafuatiliwa na kamera zilizokuwa zinaonyesha pambano hilo lililokuwa linasubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka kila pembe ya Tanzania. Hawa ndio wanasoka wetu walivyo.

Lakini pia tukio lile linatukumbusha mambo mengi ya ziada. Kwanza kabisa ni kwa namna mwamuzi alivyokuwa mzembe. Ungeweza kumsamehe mwamuzi kama Ajibu angekuwa amechezewa rafu ile mara moja. Lakini kumbe alichezewa mara nyingi ndani ya muda mchache. Alikatwa mara ya kwanza, mara ya pili, kisha mara ya tatu. Mwamuzi alikuwa wapi?

Mwamuzi alikuwa mzembe wa pili. Mzembe wa kwanza alikuwa Zawadi, mzembe wa pili alikuwa mwamuzi ambaye siamini kama aliona. Kama angeona kwa macho ya uhakika, basi Zawadi angepewa kadi nyekundu. Lakini inawezekana alimpa zawadi kadi ya njano kwa sababu aliona zaidi tukio la Zawadi kukunjana na Mohamed Hussein wa Simba baada ya Hussein kuchukizwa na tabia za kijinga za Zawadi.

Mwisho kabisa wa tukio hili, Zawadi akatukumbusha tunaishi katika dunia nyingine. Sijui nimpongeze au nimponde? Akakimbilia zake katika mtandao wa Instagram na kuomba radhi. Ni jambo la kiungwana. Nani hafanyi makosa?

Lakini ilinifurahisha kidogo jinsi ambavyo wachezaji wetu wanavyotumia mitandao yetu ya kijamii. Huwa wanaiga tabia kama hizi za kuomba radhi lakini hawaigi maisha ya kina Cristiano Ronaldo ambao siku zote huwa wanatuonyesha wakiwa katika maisha bora kupitia mchezo wa soka.

Mbwana Samatta amekuwa akiposti gari lake aina ya Range Rover na ambacho Zawadi ameweza kuiga ni tabia ya wachezaji wa kisasa kuomba radhi mitandaoni. Hajaiga tabia ya kuposti gari lake la kisasa mitandaoni. Nadhani kwa sababu hamiliki hilo gari. Hata hivyo, kutomiliki hilo gari sio kosa. Kosa ni kutoonyesha zile hasira zake za uwanjani dhidi ya maendeleo yake binafsi. Inachekesha sana.

Chanzo: mwananchi.co.tz