Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

JICHO LA MWEWE: Anko Ngassa na Yanga katika urafiki wa mashaka

90385 Ngassa+pic JICHO LA MWEWE: Anko Ngassa na Yanga katika urafiki wa mashaka

Tue, 31 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

WIKI ile iliyopita Anko Ngassa akazua jambo mitandaoni. Namzungumzia Mrisho Khalfan Ngassa. Mmoja kati ya mastaa waliowahi kuushikilia mkononi mpira wa Tanzania kama ilivyo kwa Mbwana Samatta sasa.

Tofauti ni kwamba Samatta anaushikilia mpira wa Tanzania akiwa nje ya nchi, Ngassa aliushikilia akiwa ndani ya nchi. Kila nabii na zama zake. Wakati ule ukizungumzia timu yetu ya taifa, basi tulikuwa tunaenda uwanjani kuangalia Ngassa akiwakimbiza watu.

Wiki ile Anko aliandika katika mtandao wake wa Instagram ujumbe uliokuwa unaashiria kwamba Yanga walikuwa hawayajali matatizo yake na mama yake alikuwa mgonjwa. Lakini hapohapo akadokeza kwamba mabosi wa klabu yake wanawapenda zaidi wachezaji wa kigeni kuliko wazawa.

Anko bwana! Ana kitu moyoni. Sijui kama anaweza kujisuta lakini ukweli ni kwamba yupo katika uhusiano wa shaka shaka na klabu yake. Ukiitazama klabu yake ni wazi inaona ni hisani tu kwa Ngassa kuichezea timu yao.

Wengi hawauoni umuhimu wake kama ule ambao walikuwa wanauona wakati ule. Baada ya Anko kuzunguka Azam FC, Simba, Mbeya City, Ndanda na kwingineko, mabosi wa Yanga na baadhi ya wanachama maarufu wanaamini kitendo cha Ngassa kucheza Yanga ni kama vile wamemsitiri.

Zamani matatizo ya Anko yasingefika mitandaoni au katika vyombo vya habari. Alikuwa mtoto mpendwa. Kitu cha kwanza kwa mabosi wa wakati ule pamoja na wanachama wao ilikuwa ni kuhakikisha Anko anaishi kwa raha mustarehe.

Leo upepo umebadilika na Ngassa ni kama kila mchezaji mwingine klabuni. Maisha bwana! Nyakati zimekwenda kasi na Anko anaanza kupata maumivu ya kuchukulikuwa kama mchezaji mwingine tu klabuni. Anaumia.

Huu upande wa Ngassa unaonyesha kwamba Anko mwenyewe anaamini kuwa ameitoa mbali Yanga. Anaamini anapaswa kuthaminika zaidi Jangwani. Ameifanyia klabu mambo mengi. Anahitaji thamani yake.

Anachosahau Anko ni kwamba mambo yote aliyoyafanya Yanga hayajafika walau nusu ya mambo ambayo mtu kama Edibily Lunyamila ameyafanya. Yanga wamepita wengi na sasa wanaendelea na maisha yao nje ya Yanga huku klabu ikiwa haina habari na wanachofanya.

Ndio maana sio mbaya tukimkumbusha Anko kwamba nyakati zile alizokuwa anatakiwa na klabu mbalimbali za nje ya Tanzania ilikuwa muhimu kwake kuchukua nafasi zile na kutengeneza maisha. Huenda sasa hivi angekuwa na uwezo wa kumkodia mama yake ndege binafsi ya kumtoa Mwanza hadi Nairobi kwa ajili ya matibabu mazuri zaidi.

Ofa ya mwisho ambayo Anko aliipiga teke ni ile ya kulipwa Dola 5,000 kwa mwezi na Klabu ya El Marreikh ya Sudan. Ile ofa ilikuwa tamu. Watu wa Yanga wakamtoa njiani na kumsainisha klabuni kwao ili aelekee katika njia ya umaskini.

Kabla ya hapo Ngassa aliwahi kutakiwa na klabu moja ya Norway kwa dau la Dola 50,000 lakini Yanga wakagoma. Mwenyekiti wa wakati huo, rafiki yangu, Imani Madega akadai Ngassa alikuwa na thamani ya Dola 250,000. Kwa wakati huo Ngassa hakuwa na thamani hiyo. Labda kama jamaa wangemtengeneza na kumuuza kwingineko Yanga ingeweza kuambulia pesa nyingi zaidi.

Dili lilikufa huku Anko akiona Yanga ni mahala panapomfaa zaidi. Wala hakulalamika kwamba Yanga walikuwa wanamzibia rikizi yake. Leo anapochukua simu yake na kuandika kitu kuhusu kutojaliwa, Anko anakumbuka mambo mengi.

Na sasa zimebaki kuwa pande mbili zenye urafiki wa mashaka. Yanga inaamini inamsitiri Ngassa, na wakati huohuo Ngassa anaamini Yanga inapaswa kumfanyia makubwa kwa sababu amewahi kuifanyia makubwa huko nyuma.

Urafiki wa namna hii hauwezi kudumu sana. Muda wowote Yanga inaweza kuachana na Ngassa kama ikipata uwezo mkubwa wa kipesa. Kwanini ilipokuwa na Yusuph Manji haikumtaka Ngassa na badala yake ikampeleka Afrika Kusini?

Tutaendelea kusikia malalamiko mengi kutoka kwa Anko Ngassa kwa sababu kwa sasa hana thamani sana. Haya yanayoendelea tuliwahi kumwambia zamani. Hizi klabu mbili za Kariakoo huwezi kuziwekea dhamana. Wamepita ‘miunguwatu’ wengi ambao mpaka sasa hatujui walipo. Hata ambao wamefariki basi makaburi yao tumeshayasahau.

Kitu cha msingi katika mpira wa Tanzania ni kujali zaidi maisha yako mwenyewe pindi unapokuwa fomu. Hakuna anayeweza kukujali baadaye. Kila mtu anahusika zaidi na maisha yake mwenyewe. Tatizo la wachezaji wetu huwa wanageuzwa kuwa wanachama na mashabiki wa timu hizi.

Badala ya kugeuka kuwa wafanyakazi huwa wanageuzwa kuwa wanachama au mashabiki na mara nyingi wanaishia pabaya. Anko Ngassa sio mtu wa kuiomba klabu imuhudumie mama yake. Anko pia hakuwa mtu wa kuanza kuhangaikia malipo yake ya mshahara au pesa alizoahidiwa katika mkataba. Anko Ngassa alipaswa kuwa Ulaya akimalizia maisha yake ya soka.

Chanzo: mwananchi.co.tz