SAKATA kubwa la kashfa ya mpira wa Tanzania sasa ni juu ya madaoi ya kipa wa Yanga Ramadhan Kabwili alipoibuka na kueleza juu ya alipokaribia kuingia katika harakati za kuhongwa asiidakie timu yake.
Kabwili ameshtua uma wa soka kupitia madai yake hayo ambayo aliyatoa katika kituo kimoja cha redio akielezea hatua ya kutakiwa kupokea hongo akitakiwa ahakikishe anapata kadi ya njano ili asiweze kuidakia timu yake katika mchezo uliofuata.
Madai hayo yamewashtua wengi hasa wakiangalia umri wa kipa huyo akiihusisha Simba ambayo ni klabu kubwa nchini huku akionyesha hana wasiwasi wowote kuelezea suala hilo.
Baada ya matamshi hayo ya Kabwili, Simba wenyewe wakawa wakali wakipambana kuimarisha heshima yao kupitia madai hayo ambayo ni wazi yamekuja katika mrengo wa kuishushia hadhi klabu hiyo kongwe.
Baada ya muda tamko la Simba lilifuatiwa na lile la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wakionyesha kusikia madai hayo na kwamba watahakikisha yanafanyiwa kazi na mamlaka husika bila kufumbiwa macho. Binafsi sikushtushwa na madai ya Kabwili, ila nilichoona ni hatua ya nyumba kuharibika na sasa mtoto kaamua kuyasema wazi makosa ya wazazi kutokana na malezi anayoona alilelewa.
Umri wa Kabwili ndio unaotuumbua katika hili kwani tumeyalea madai ya namna hii, tukijifanya kuishi kama watu wazima huku tukilindana na sasa watoto wanakuja kuweka wazi kisha tunajifanya tunataka kuchukua hatua.
Habari zinazohusiana na hii
- TIMUA VUMBI : Hili la Kabwili liachwe kwenye vyombo vya dola
- Kabwili aongeza petroli moto wa rushwa Simba
- Yanga yamweka chini Kabwili tuhuma za kupewa rushwa na Simba SC
Nakumbuka kocha Abdallah Kibadeni mwenye heshima kubwa katika soka letu aliwahi kujitokeza hadharani akiwaita TFF kwamba ana ushahidi wa kuwepo kwa rushwa katika soka lakini alipoitwa kesi ile haifahamiki hitimisho mpaka sasa.
Kama haitoshi kesi kama hiyo iliwahji kuwahusisha wachezaji wa Azam ambao walidaiwa kupokea rushwa wakati huo timu yao ikiwa na mchezo dhidi ya Simba,wachezaji husika walisimamishwa kwa muda na mambo kuonekana yanashika moto lakini jioni kabisa tukasikia keshi hiyo imezimwa na wachezaji wakarudi kazini.
Kama hiyo haikutosha likaibuka sakata la kipa wa Mtibwa Sugar Shaba Kado kuibua madai kama hayo yakimuhusisha mchezaji mmoja wa zamani wa Simba Ulimboka Mwakingwe lakini nayo licha ya kuwa kesi nzito ambayo wapo walofika mpaka kituo cha polisi lakini baadaye ikazimwa maisha yakaendelea kama kawaida yetu.
Msimu uliopita tu aliyewahi kuwa kocha wa Mbeya City wakati huo na sasa yupo pale Singida United Mrundi Ramadhan Nswazurimo tunakumbuka alitoa kauli gani ya wazi tena baada ya timu yake kumaliza mchezo na klabu moja kubwa hapa nchini?
Haya ni madhara ya kuyafumbia macho mambo ya msingi na kuamua kulindana na sasa baada ya kuyasema babu yetu Kibadeni naona hata mjukuu wake Kabwili ameamua kupita njia ya babu yake katika kesi hiyo. Kelele kama hizi zinaashiria kuwa rushwa ni kubwa katika soka, lakini hatujaamua kuzifanyia kazi kwa ukamilifu ingawa tunataka kuishi kwa kuangalia nani anayasema haya na yanamhusisha nani na je tumlinde au tumuangamize.
Nilifurahi wakati fulani Rais wa TFF, Wallace Karia wakati akianza tu kipindi chake cha uongozi aliwahi kuwaita waamuzi wote wa ligi na kuwatangazia vita kubwa juu ya rushwa, lakini hebu leo tujiulize licha ya mkwara mkali wa Karia ambaye alifikia hatua ya kueleza kwamba ameweka mtego tujiulize umemnasa nani mpaka leo?
Waamuzi wamekuwa katika usafi gani katika kazi zao na je hakuna mazingira ya wazi katika kutupatia mshindi ambaye hastahili hata kufikiriwa?
Kesi hizo ziko nyingi za rushwa na naona Kabwili ametufikisha tamati katika kuamini kwamba rushwa katika soka letu ni kubwa na sasa tunatakiwa kuamka na kuwa wakali bila kuangaliana katika klabu unayoshabikia.
TFF haitakiwi kumfanya Kabwili kama mtu adui badala yake anatakiwa kuchukuliwa kama msaada mkubwa wa kijana mdogo aliyeona mambo machafu ya mzazi wake kisha kuamua kuyaweka wazi kwa jamii ili hatua ya kuuokoa mpira wetu ichukuliwe haraka.