Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ilunda ashindwa kuokoa jahazi la Uchukuzi lisizame Mei Mosi

7905bb193a39fffd4436460ecee477b0 Ilunda ashindwa kuokoa jahazi la Uchukuzi lisizame Mei Mosi

Mon, 19 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KATIBU Mkuu wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta) na mchezaji wa zamani wa timu ya taifa, Judith Ilunda ambaye ni mchezaji wa timu ya Uchukuzi ameshindwa kuokoa jahazi lao lisizame baada ya kufungwa na Ikulu kwa mabao 37-14.

Ilunda ambaye pia wakati wa uchezaji wake alikuwa mchezaji mahiri wa timu ya Bandari ya Dar es Salaam, alikuwa tegemeo kubwa katika mchezo huo wa jana wa Michezo ya Mei Mosi uliofanyika kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa.

Nyota huyo aliyekuwa akicheza nafasi ya ufungaji akisaidiana na Neema Mwanu, waliipeleka timu yao mapumziko wakiwa nyuma kwa magoli 14-8.

Wachezaji wengine wanaounda timu hiyo ni Neema Makassy, Habiba Othman, Mchilo Rajabu, Irene Mitava na Martha Kibona, wakati wachezaji wa Ikulu ni Restuta Boniface, Elizabeth Fussi, Irene Kivile, Chuki Kikalao, Sophia Komba, Salome Mika, Anna Msulwa, Amina Mwampole na Lilian Sylidion.

Katika mchezo mwingine, timu ya Tanesco imewachapa bila huruma Wizara ya Mambo ya Nje kwa mabao 56-2.

Washindi waliongoza kwa magoli 25-2 hadi mapumziko.

Nayo timu ya Shirika la Maendeleo ya Petrol Tanzania (TPDC) ilipata ushindi wa chee wa magoli 40 na pointi mbili baada ya wapinzani wao Ulinzi kutoonekana uwanjani.

Katika michezo ya soka, timu ya Uchukuzi ilianza vyema kwa kuwafunga Wizara ya Mambo ya Nje kwa mabao 7-0 mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Nyamagana.

Magoli ya washindi yalifungwa na Selemani Kaitaba na Idrisa Bahatisha kila mmoja akifunga mawili, huku Salim Salehe, Lugano Mwasomola, Said Singano na David Kunambi wakifunga bao moja moja kila mmoja.

Nayo timu ya Tanesco iliwaadhibu Ukaguzi kwa magoli 6-0. Mabao ya washindi yalifungwa na Kurwa Mangarano mabao matatu, huku Ndere Maketa, Khalifa Shekule na Castory Mhemchele kila mmoja alifunga bao moja moja.

Timu ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) iliwafunga wenyeji timu ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza (RAS Mwanza) kwa mabao 4-2.

Wafungaji wa NCAA ni Tumaini Pendemu mawili, huku Regan Peter na Liberatus Rwechungura wakifunga moja kila mmoja.

Kwa upande wa michezo ya kuvuta kamba, timu ya wanaume ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro iliwavuta Ukaguzi mivuto 2-0 na kwa upande wa dada zao waliwavuta Wizara ya Kilimo kwa mivuto 2-0, wakati katika mchezo wa wanawake, Taasisi ya Saratani Ocean Road ilipata ushindi wa chee wa mivuto 2-0 baada ya Wizara ya Mambo ya Nje kuingia mitini.

Michuano hiyo inaendelea leo, ambapo katika soka kwenye Uwanja wa CCM KIrumba timu ya Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) itakutana na Ulinzi, huku Wizara ya Mambo ya Nje itacheza na Wizara ya Kilimo wakati katika Uwanja wa Nyamagana Ukaguzi itakutana na Mamlaka ya Majisafi na Taka Mwanza (Mwauwasa).

Katika michezo ya netiboli ambayo yote inafanyika CCM Kirumba, timu ya Mwauwasa itapepetana na Tanesco na Ulinzi watawakaribisha Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mambo ya Nje watacheza na ndugu zao Wizara ya Mambo ya Ndani.

Nayo michezo ya kuvuta kamba wanawake, timu ya Uchukuzi itakutana na Tanesco na Mwauwasa itacheza na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) wakati kwa upande wa wanaume TPDC itavutana na Tanesco.

Fainali za michezo ya soka, netiboli na kuvuta kamba zinatarajiwa kufanyika Aprili 29 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.

Chanzo: www.habarileo.co.tz