Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

IVO MAPUNDA: Ile video anaombewa lile taulo lake langoni

82438 Mapunda+pic IVO MAPUNDA: Ile video anaombewa lile taulo lake langoni

Fri, 1 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

WAHENGA wanasema “fimbo ya mbali haiui nyoka” au “utamu wa ngoma uingie ucheze”. Haikuwa rahisi kuamini kama Ivo Mapunda, kipa mwenye historia na soka batrani Afrika alikuwa amemaanisha kuombewa.

Baada ya video kusambaa kwenye mitandao ya kijamii ikimuonyesha staa huyo wa zamani ameshika magongo kisha akayatupa baada ya kuombewa na mmoja wa manabii waliopo Dar es Salaam, jambo hilo liliibua mijadala miongoni mwa Watanzania na hasa wanamichezo wanaomfahamu.

Mwanaspoti lilifunga safari hadi Mwanagati, jijni humo ambako ndiko anakoishi Mapunda na kuzungumza naye kuhusiana na maisha yake kwa ujumla ikiwemo tukio la kuombewa na jambo hilo lilivyozua gumzo kwenye mitandao ya kijamii.

Katika mazungumzo hayo, kuna wakati kicheko kilitawala kutokana na utani wa kipa huyo wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, lakini pia kuna wakati ambapo kope za macho zilikuwa zinalengwa na machozi akisimulia mateso ya kusumbuliwa na mgongo.

Ni katika amzungumzo hayo kuna wakati alikuwa anapata shida ya kujinyoosha mgongo kutokana na kukaa muda mrefu, ingawa alionekana kujikaza ili wageni wake (Mwanaspoti) wasijisikie vibaya au kukatiza mazungumzo.

Nyota huyo mstaafu alifunguka mengi yenye mafunzo ndani kwa mastaa ambao wanacheza soka kwa sasa, ukiachana na hilo akaeleza nini anafanya sasa na malengo yake ya baadaye.

Ivo alianza kusumbuliwa na mgongo tangu alipotua Azam FC akitokea Simba na maumivu hayo hakuyatilia maanani hadi pale alipoona hali inazidi kuwa mbaya ndipo alipoenda hospitali kwa ajili ya vipimo.

“Yalianza muda mrefu, ingawa niliona sio maumivu makali sana. Hali ilivyoendelea kusonga nikazidi kusikia maumivu zaidi, niliamua kwenda hospitali kwa ajili ya vipimo, nilipiga x-ray na kubainika pingili (za mgongo) kama tano hivi zina shida,” anasema.

“Nilikwenda kufanya kipimo kingine cha MRI ambapo nilishauriwa kufanyiwa upasuaji, lakini hilo suala kwangu lilikuwa gumu kulikubali moja kwa moja ingawa walinipa dawa za kutumia na kufuata masharti.

“Niliendelea na masharti pamoja na kutumia dawa, hali ilikaa vizuri ingawa nilichukua uamuzi sasa wa kuacha kucheza soka la ushindani, nilipomaliza mkataba Azam niliamua kustaafu na kufungua kituo changu (cha soka) kwani soka ndiyo kazi ninayoipenda.

“Nilikaa muda mrefu bila kufanya mazoezi ya kutumia nguvu kufuatana na ushauri niliopewa na daktari hali iliendelea vizuri. Nakumbuka kuna siku nilienda kufanya mazoezi ndipo nilipochokonoa upya maumivu ya mgongo ambayo yaliniweka kitandani kwa miezi miwili nikitumia msaada wa magongo kutembea.

“Kilikuwa ni kipindi kigumu sana kwangu kwani sikuwa na uwezo wa kufanya jambo lolote lile, nilipewa msaada kwa kila jambo nililotaka kulifanya, niliumia sana.

“Kuna jirani yangu mmoja ndiye aliyeniambia anipeleke kwa nabii (anamtaja jina) ingawa wengine walinishauri niende kwenye tiba mbadala za miti shamba, kote huko ilikuwa ni kuhangaika kupata tiba.

“Lakini kitu cha mwisho nilichokiamua ni kwenda kwa nabii. Nilikuwa simfahamu ila huyo jirani yangu ndiye aliyeniongoza kufika hapo, siku ya kwanza tulijiandikisha na kupewa utaratibu wa siku ya maombezi.

“Siku hiyo niliwahi pamoja na huyo rafiki yangu, tulifika kanisani na kupewa utaratibu wa jinsi ya kukaa kusubiri ibada hiyo ya maombezi, niliingia kwenye kanisa hilo nikiwa na imani kubwa ya uponyaji baada ya kupata mateso makubwa kwa kipindi nilichokuwa kitandani.

“Nakumbuka siku hiyo wakati naombewa alikuwepo Mkuu wa Mkoa (wa Dar es Salaam), Paul Makonda ambaye pia alikuja kusali hapo, maana ibada husaliwa popote na yeye ni mtu anayemwamini sana Mungu, hivyo watu wajue sikufanya maigizo nilikuwa na matatizo ya kweli.

“Niliombewa na nabii baadaye aliniambia nitupe magongo, nikayatupa akaniamuru nitembee bila msaada wa hayo magongo, kweli ikawa hivyo, nilimshukuru sana Mungu kutenda huu muujiza kwangu.

“Hata niliporudi nyumbani, jirani zangu hawakuamini kama mimi natembea bila msaada wa magongo, natembea peke yangu pasipo msaada wowote, kwa hakika Mungu anastahili.”

Je ameokoka?

Ivo ambaye ni mkurugenzi wa kituo cha michezo cha Ivomapunda Sports anafafanua juu ya kuokoka kama baadhi ya watu wanavyodhani kwamba kuombewa kwake na kupona kumesababisha aokoke.

“Kuokoka ni jambo pana sana, ni kitu kinachohitaji imani kubwa mno, mtu hutakiwi kucheza na ulokole. Ila watu wajue kutenganisha kati ya imani na kuokoka.

“Mimi namwamini Mungu kwa kila jambo kuwa anatenda pale mtu amwombapo kwa kumaanisha, nikiwa na maana kwamba ukimwamini Mungu kuwa ni mwokozi wako basi hata ugonjwa atakuponya na mengine mazuri atakutendea.

“Hivyo mimi sijaokoka, bali nina imani. Ndugu zangu kuokoka ni hatua kubwa sana mbele za Mwenyezi Mungu na hakutakiwi kurudi nyuma kabisa,” anaeleza.

Je amehama dhehebu?

“Sijahama dhehebu, ila nasali kwa nabii (anamtaja) tangu nianze kuombewa hapo. Mtu yeyote anaruhusiwa kusali kwake pasipo kuhama dhehebu, maana wenzetu Waislamu wapo wengi tu wanakuja kuombewa na hakuna aliyeambiwa ahame dini yake ama dhehebu lake, pale ni maombi tu na kuondoka, kila mtu kwa imani yake.”

Vipi kuhusu kulipa pesa kumuona Nabii

Ipo dhana kwamba, baadhi ya viongozi wa dini hususan wanaoitwa manabii huwatoza fedha watu wanapotaka kuombewa, Ivo anakana kuwa hakukumbana na hilo.

“Huwa nasikia baadhi ya wahubiri ama wachungaji wakielezwa kwamba huwatoza waumini fedha kwa ajili ya kuwaona, ila kwa nabii (anamtaja) binafsi sijawahi kutozwa chochote zaidi ya sadaka ya kawaida,” anasema.

“Unajua kila mmoja ana imani yake na jinsi anavyoongozwa na roho mtakatifu kuwaombea watu, hivyo watu waamini huku hakuna pesa yoyote inayotolewa ukitakiwa kumuona nabii ama kuombewa kama inavyodaiwa, nimepona kwa imani na miujiza ya Mwenyezi Mungu.”

Vita yake na Casillas

Wakati Ivo anaichezea Simba akitokea Gor Mahia ya Kenya ndicho kipindi ambacho kipa Hussein Shariff ‘Casillas’ naye alisajiliwa kutoka Mtibwa Sugar.

Ivo alitokea Gor Mahia akiwa kwenye ubora wake wakati Casillas naye alitoka Mtibwa Sugar akiwa kipa namba moja.

Vita ilikuwa kali kati ya wawili hapo ambapo Manyika Peter Jr, aliyekuwa amepandishwa kutoka U20 ya Simba akiwa anakaa benchi kusubiri kuingia pale inapobidi. Wakati huo kocha wa makipa wa wawili hao alikuwa Idd Pazi, na wote aliwafundisha kwa usawa pasipo kuangalia nani zaidi kuliko mwenzake.

Wawili hao walianza kuwa na bifu ndani ya timu ambalo lilitoka hadi nje na kuwa wazi kwa wadau na mashabiki wa Simba kwani hata kupeana salamu kwao ilifika mahali ikawa shida.

Tatizo kubwa lililokuwepo ni juu ya namba, kwamba nani awe namba moja huku wengine wakiwashauri viongozi wa Simba wakati huo, Evans Aveva (rais), kwamba ili amani iwepo kwa wawili hao ni lazima mmoja aondolewe. Ulikuwa ni mtihani kwao.

Ivo anaelezaje juu ya bifu hilo? “Ni kweli mimi na mdogo wangu Casillas tulikuwa hatupatani kabisa, ilifikia hatua hata salamu ilikuwa ni shida kuitikia. Hii yote ilitokea baada ya Casillas kusikiliza na kukubali maneno ya kuambiwa kwamba namroga ili asipate nafasi ya kudaka.

“Ila ukweli ni kwamba kwa kipindi kile ilikuwa ni lazima mimi niwe kipa namba moja. Nakumbuka bifu lilinoga zaidi alipoumia Afrika Kusini, aliamini kuwa nimemroga, sikuwa miongoni mwa wachezaji waliokwenda kuweka kambi nchini humo kwa sababu nilivunjika kidole gumba tukiwa kambini Zanzibar.

“Madaktari walinishauri kupumzika na kweli ilikuwa lazima iwe hivyo, ndio maana sikuona sababu ya kwenda Afrika Kusini. Wakiwa huko walicheza mechi ya kirafiki ambapo Casillas aliumia zikiwa zimebaki siku chache kurejea nchini kwa ajili ya mechi ya Mtani Jembe na Yanga.

“Uongozi ulilazimika kunikatia tiketi ya ndege ili nikaungane na wenzangu, ila ukweli nilikuwa sijapona kabisa, nilipelekwa kama ushahidi tu wa kuongeza nguvu kwani alibaki Manyika peke yake.

“Nilipofika huko sikubahatika kuonana na Casillas kwani muda wote alikuwa maelazwa kwenye hospitali ya ile timu waliyocheza nayo mechi ya kirafiki hadi siku ambayo tulikuwa tunaondoka. Cha ajabu na kusikitisha nilipomjulia hali hakuitikia salamu yangu, hapo ndipo nilipovunjika moyo kuwa huyu mdogo wangu imekuwaje? Mawazo yakanijia kuwa kweli atakuwa ameamini maneno ya watu kuwa nimemroga.”

Ivo anasema, “yote kwa yote baadaye kila mmoja aliondoka Simba, huku akiwa hana amani na mwenzake, ila ikumbukwe kwamba kuna maisha baada ya soka ama baada ya timu fulani. Tulikutana mtaani tukiwa wanachama wa chama cha makipa ambapo mazoezini tulikuwa tunaonana kama kawaida.

“Tulikaa chini na kutafakari tuligundua kuwa kilichotokea Simba hakikuwa na faida kwetu, tuliyamaliza huku kila mmoja akiilaumu nafsi yake ambapo hadi sasa maisha yetu yanasonga na tunawasiliana.

“Tunapaswa kujifunza kuishi kwa upendo bila chuki hata kama mtu akimkosea mwenzake anapaswa kujishusha na kumuomba msamaha kwani iliwahi kunitokea hata kwa Matola (Selemani), lakini nilivyogundua kuwa nimemkosea nilimuomba msahama maisha yakaendelea.”

Juhudi za kumpata Casillas kuelezea kulikoni walitofautiana na Ivo zinaendelea.

Kuhusishwa na ushirikina?

Ivo anasema kwamba ushirikina kwenye soka ni kitu cha kawaida na umetawala, na kwamba hakuna mchezaji ambaye amepitia timu kongwe za Simba na Yanga ambaye hajawahi kuufanya au kukumbana nao.

Anasema hizo ni imani tu na hazisaidii lolote kwenye soka, na kuwataka wachezaji kujituma zaidi mazoezini huku wakimwamini Mungu kwani hizo njia mbili pekee ndizo zinazoweza kuwavusha na kufikia mafanikio.

“Soka la Tanzania lina ushirikina mwingi, labda niwaambie ukweli nimepitia hayo na wala sikuona faida yake, ndio maana kwenye mataulo yangu nilikuwa naandika neno la Mungu,” ansema.

“Sitaji nikiwa timu gani ila kuna wakati nilikuwa napewa vitu niweke kwenye glovu au chini ya soksi nilikuwa nikivichukua wakiondoka naweka kando, kwani ningekataa kupokea basi kila siku ningekorofisha na viongozi wangu ambao ni kama imani na utamaduni wao.

“Mchezaji anapaswa kuzingatia nidhamu, ajitume mazoezini, waache zinaa, basi watacheza kwa kiwango cha juu. Laiti kama waganga wangekuwa wakweli wangekuwa wanakuja mazoezini na sio wakati wa mechi, hapo ndipo tunapoachwa na Wazungu.”

Kila mechi taulo tisa

Ivo alikumbwa na tuhuma za ushirikina tangu akiichezea Gor Mahia ambapo alianza kutumia taulo wakati wa mechi, lakini yeye anasemaje? “Mataulo yangu yote yalikuwa na upako wa Mungu na wala siyo ushirikina kama walivyodhani, niliyatumia kufutia jasho mikononi wakati wa mechi kwani mpira ulikuwa unaendelea, mashabiki na wachezaji walitafsiri tofauti kwamba mataulo yangu yana uchawi.”

Kesho katika sehemu ya pili ya makala za Ivo Mapunda ataeleza kwa undani juu ya mataulo hayo na nini mtazamo wake katika soka la sasa.

Chanzo: mwananchi.co.tz