Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Huzuni, majonzi vilitawala mwaka 2023

Hegfgf Huzuni, majonzi vilitawala mwaka 2023

Tue, 12 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Pumzi ni zawadi ambayo Mungu amekuwa akitoa bure sio kwa ujanja wala chochote ambacho ukonacho pengine haya ndio maneno ambayo yanaweza kuwa na thamani kwa sasa wakati bado tunapumua huku tukiwa wenye afya tele licha ya mitihani mingi ambayo tumekumbana nayo katika mwaka 2023.

Kwa wale ambao wanapitia changamoto za kiafya au nyinginezo Mwenyezi Mungu aendelee kuwapigania, ni zaidi ya wiki 50 kuumaliza mwaka sio jambo dogo maana wapo ambao walitangulia mbele za haki bila ya hata kuuona mwaka huu na wengine walimaliza mwendo baada ya wiki chache tu kupita.

Yapo matukio mengi ambayo yametokea mwaka huu, lakini hawa ni baadhi ya wanamichezo na wasanii ambao tumewapoteza kwa nyakati tofauti.

PIGO KWENYE RIADHA

Aprili mwaka huu, mwanariadha maarufu wa Tanzania, Alphonce Simbu, alipata pigo la kumpoteza kocha wake, Francis John. John alifariki dunia usiku katika Hospitali ya KMC, Moshi baada ya kupata ajali katika eneo la maji ya chai, Arusha akitokea Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Riadha Mkoa wa Arusha (ARAA), Rogat John alimwelezea marehemu kwa kusema: “Francis alikuwa mwalimu wa kweli wa riadha na nyota wengi walipitia mikononi mwake.”

Mbali na Simbu aliyeleta medali ya fedha katika Michezo ya Jumuiya ya Madola na medali ya shaba Mashindano ya Dunia, wengine walipitia mikononi mwake ni Christopher Isegwe. Mtanzania wa kwanza kushinda medali katika Mashindàno ya Dunia. Isegwe alitwaa medali ya fedha.

Wanariadha wengine ni Samson Ramadhani mwenye medali ya dhahabu ya Jumuiya ya Madola, Bonay Akonay, Zebedayo Bayo na wengine.

Kocha huyo pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Riadha Tanzania (RT), kipindi ambacho Tanzania ikifanya vizuri katika riadha kimataifa. Baada ya kumaliza kipindi chake, Kocha Francis nafasi yake RT ilichukuliwa na Antony Mtaka.

KOCHA MTIBWA

Machi, Mtibwa Sugar ilimpoteza mchezaji Iddy Mobby ambaye alifariki baada ya kudondoka na alipopelekwa Hospitali ya Benjamini Mkapa jijini Dodoma kwa matibabu ndipo mauti yakamkuta.

Agosti mwaka huu, Kocha Ahmed Mumba ambaye aliwahi kuifundisha timu hiyo naye alifariki dunia akiwa jijini Dar es Salaam baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Enzi za uhai wake mbali na kuifundisha Mtibwa Sugar, Mumba alizinoa klabu mbalimbali zikiwemo Nazareth ya Njombe, Majimaji ya Songea, Polisi ya Iringa na Morogoro pamoja na Mawenzi Market ya Morogoro.

SHABIKI TAIFA

Mei mwaka huu, serikali ilithibitisha kifo cha shabiki mmoja wa Yanga SC kufuatia vurugu zilizozuka mapema nje ya uwanja huo wakati wa zoezi la mashabiki kuingia uwanjani kwenye mchezo wa kwanza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kati ya Yanga SC dhidi USM Alger.

Taarifa ya awali iliyotolewa na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu ilieleza Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke ilipokea jumla ya majeruhi 30 ambapo mmoja amefariki (mwanaume mwenye umri wa takribani miaka 40.) na majeruhi wengine walikuwa wanaendelea vizuri.

MWIMBAJI WA DANSI

Aprili mwaka huu, Mwanamuzi Hussein Jumbe alifariki wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Amana jijini Dar es Salaam, ndugu wa karibu na marehemu walithibitisha.

Jumbe amewahi kuimba na Bendi za Tabora Jazz, Musoma Jazz, DDC Mlimani Park “Sikinde”, TOT Band, Msondo Ngoma, Tabora Jazz, Urafiki Jazz, Mikumi Sound na nyingine nyingi.

Msanii huyo wa mziki wa dansi alikuwa akisumbuliwa na kifua kwa muda mrefu.

BONGOFLEVA

Septemba Mosi, msanii wa Bongofleva, Haitham Kim ambaye wasanii nawadau mbalimbali walianzisha kampeni ya kumsaidia kwa kuchangisha pesa kwa ajili ya matibabu yake alifariki siku hiyo katika Hospitali ya Rufaa ya Temeke Jijini Dar es salaam.

BNB ambaye ni rafiki wa mume wa marehemu Haitham, alithibitisha kuwa Haitham kufariki hospitalini hapo. Katika mahojiano ilielezwa hali ya Haitham ilibadilika ghafla siku saba ambapo alikuwa akisumbuliwa na upumuaji, hali iliyoanza kama homa ya kawaida lakini baadaye akawa anakosa pumzi hadi kupekwa hospitali ambako alitumia mashine ya kupumulia.

AFIA UWANJANI

Machi mwaka huu, mchezaji chipukizi wa Ivory Coast, Sylla Moustapha alifariki baada ya kuanguka uwanjani wakati wa mechi ya Ligi Kuu kati ya klabu yake, Racing Club d’Abidjan na SOL FC kwenye Uwanja wa Robert Champroux.

Moustapha, anayecheza beki alifariki akiwa na umri wa miaka 21. Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Patrice Motsepe alikuwa miongoni mwa watu mashughuli ambao walituma salamu za pole kwa familia ya Moustapha.

DWAMENA WA GHANA

Novemba mwaka huu, mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Ghana, Raphael Dwamena alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 28 baada ya kuanguka uwanjani akiwa Albania.

Katika dakika ya 23 ya mchezo wa Ligi ya Albania Superliga kati ya FK Egnatia na Partizani, Dwamena alianguka uwanjani na kufariki dunia.

Mchezaji huyo wa zamani wa Red Bull Salzburg, ambaye alicheza mechi tisa za Ghana kati ya 2017 na 2018, alitolewa nje ya uwanja na licha jitihada mbalimbali ambazo zilifanywa na madaktari kuokoa maisha yake, baadaye alitangazwa alifariki dunia.

Maisha ya mshambuliaji huyo mwenye kipaji yalitatizwa na matatizo ya moyo, licha ya kwamba alishauliwa kutundika daruga mapema lakini hakutaka kujiondoa kwenye mchezo wa soka ambao aliupenda.

SIMANZI SINGIDA

Januari mwaka huu, Singida Big Stars ilithibitisha kutokea kwa kifo cha aliyekuwa mchezaji na nahodha wa timu yake ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Mohammed Banda, kilichotokea asubuhi ya Januari 19.

Banda alipoteza maisha alipofikishwa Hospitali ya Mkoa wa Singida baada ya kugongana kichwani na mchezaji mwenzake wakiwa mazoezini katika Uwanja wa Magereza, Singida.

JAMIN PUGH ‘JAY BRISCOE’

Mwanamieleka Pugh alishindana katika ulingo kama Jay Briscoe kwa miongo miwili, akipata sifa za ubabe pamoja na kaka yake Mark kama timu ya lebo “The Briscoe Brothers.” Wawili hao walishinda taji la Timu ya Tag ya Dunia ya ROH mara 13, rekodi iliyojumuisha taji la 2022. Pugh alifariki Januari 24, 2023. Alikuwa na umri wa miaka 38.

AFARIKI KWA KUPIGWA RISASI

Februari mwaka huu, msanii maarufu kutokea Afrika Kusini, Kiernan Jarryd Forbes ‘AKA’ ambaye amewahi kufanya kazi na wasanii mbalimbali wa Kitanzania, aliripotiwa kufariki dunia kwa kupigwa risasi tano yeye pamoja na mtu msanii mwingine kwenye Barabara ya Durban ya Florida.

Msanii mwingine wa Afrika Kusini, Costa Titch amabaye amewahi kufanya kazi na wasanii wa Tanzania akiwemo Diamon, alifariki dunia Machi 11, 2023, Costa. Kifo cha msinii huyu kilitokea baada ya kuanguka jukwaani na kupelekwa hospitali ambapo ilitangazwa alishafariki.

Chanzo: Mwanaspoti