ENDAPO beki wa Simba, Henock Inonga ‘Varane’ ataendeleza kiwango alichokionyesha mchezo wa kwanza Ligi ya Mabingwa dhidi ya Jwaneng Galaxy FC ya Botswana atampa wakati mgumu mkongwe, Joash Onyango kurudi kikosi cha kwanza, watu wa mpira wamekubali.
Akida Makunda aliyewahi kutamba na Pan Africans, Simba na baadaye kujiunga na Yanga alisema Inonga ni beki mzuri, mtulivu akiwa na mpira anatoa pasi zinazofika anajua kucheza na mpira na anatumia akili kucheza na sio nguvu kama mabeki wengi walivyozoeleka.
“Ni mechi moja amecheza lakini kiwango alichokionyesha mchezo ukiwa ni nje ya uwanja wa nyumbani anahitaji kupongezwa ni mzuri kama ataendeleza kiwango hicho anateteresha ugali wa Onyango ambaye amekuwa bora tangu amejiunga na Simba kutokana na kuwa
na vitu vingi ambavyo Onyango hana mfano kurukia mipira ya juu na anakasi,” alisema.
“Pia umri wake unambeba anaweza kuwa hazina kwenye kikosi ukizingatia Simba inawachezaji wenye umri mkubwa eneo la beki wa kati hivyo damu yake changa ikichanganywa na mmoja wapo anaweza kuwa bora na kuisaidia timu.”
Naye Kocha Msaidizi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Ligi ya Wanawake, Simba Queens, Matty Mseti alisema baada ya wadau kuzungumzia ubora wa nyota walioondoka Simba, Clatous Chama na Luis Miquissone sasa matunda yameanza kuonekana kwa usajili mpya kuanza kujibu.
“Lilikuwa ni suala la muda wachezaji kuanza kuonyesha uwezo wao hasa usajili mpya sasa anatajwa Varane kwangu naona Simba imefanya usajili mzuri na inaonyesha itakuwa bora baada ya huyo kuna majina mengi mazuri yatatanjwa amefanya vizuri naameonyesha utofauti kuwa yeye ni mgeni na amekuja kufanya kazi,” alisema.
“Beki ya kati sasa inampa mtihani Gomes kwani imekuwa na wachezaji wenye ubora kuna Onyango ambaye amekuwa bora tangu ametua Simba lakini ujio wa damu changa utampa kazi ya kuhakikisha anajinoa vizuri ili kuonyesha ushindani kwake.”
Awali, Yanga walimtaka Varane wakati wa usajili lakini walizidiwa kete na Simba baada ya wakala wake kulielewa zaidi dau la Mnyama na kumuuza mchezaji huyo.