Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Huyu Manji kaliamsha tena Yanga, atoa maagizo mapya. Cannavaro achekelea

13802 Pic+manji TanzaniaWeb

Sat, 25 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

YANGA juzi usiku iliandika ushindi wake wa pili mfululizo kwenye mechi za mashindano huku siri kubwa ikibaki kwa Mwenyekiti wake, Yusuf Manji. Yanga, ilianza kwa ushindi mabao 2-1 dhidi ya USM Algers kwenye Kombe la Shirikisho Afrika kisha ikawachapa Mtibwa Sugar kwa idadi kama hiyo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ushindi huo si kwamba Yanga imeupata kwa kubahatisha, bali imepiga mpira mwingi ambao mashabiki wake hawajawahi kuuona tangu alipoondoka Mzambia, George Lwandamina hivyo, kuwapa mzuka mwingi Wanajangwani.

Kwa sasa Yanga itakwea pipa siku mbili zijazo kwenda Kigali, Rwanda kumalizana na Rayons Sports kukamilisha ratiba, safari ambayo ndio itakuwa ya mwisho kwa Yanga kwenda anga za kimataifa kutokana na msimu uliopita kuambua patupu huku ikicheza soka la kiwango cha chini.

Hata hivyo, hilo halijawahi kuwa tatizo kabisa kwa Manji, ambaye ameamua kuliamsha tena akiwapa mzuka wachezaji wake kwenda Rwanda kufanya kweli. Manji ametuma ujumbe mzito kwa wachezaji akipitia mabosi wa Yanga huku akitoa maagizo mazito ambayo anataka yafanyike ili kuifanya timu hiyo kuwa ngangari.

Iko hivi. Wakati kikosi kikijiandaa kwa safari ya Rwanda keshokutwa Jumatatu kuikabili Rayon Sport, Manji amewapa maelezo mabosi wa Yanga ili yafikishwe kwa wachezaji, ambapo amewaagiza kucheza soka kama lile lililomlaza hoi mwarabu na kukubali kipigo cha 2-1.

Mwanaspoti linafahamu kwamba, Manji alifurahishwa na kiwango kilichoonyeshwa na vijana wake kwenye mchezo dhidi ya USM Algers na ametaka kasi hiyo kuendelea hadi Ligi Kuu Bara ili kurudisha heshima ya Wanajangwani.

Pia, gazeti hili limethibitishiwa kuwa kiongozi huyo, ambaye nafasi yake haitagombewa katika uchaguzi wa Yanga wa kujazia nafasi, amewaeleza wachezaji wake kuongeza kasi kwani, soka walilocheza dhidi ya Mtibwa lilipungua kidogo hivyo, anataka moto ukawawakie Rayon.

Katika salamu hizo, Manji aliwaambia wachezaji wake kuwa wana kila sababu ya kuondoka na ushindi dhidi ya Wanyarwanda hao ili kumaliza nafasi ya tatu kwenye msimamo na kujenga heshima.

Pia, amewatuma viongozi maalumu kuambatana na timu kwenda Kigali, Rwanda ili kuhakikisha morali ya wachezaji haishuki.

Mwanaspoti liliwatafuta viongozi wa Yanga, ambapo Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano, Hussein Nyika amekiri kufikiwa kwa ujumbe wa Manji na kueleza kuwa kila kitu kinaendelea vizuri kwa sasa.

“Ni kweli Mwenyekiti wetu ametuma salamu kwa wachezaji na kutoa maelekezo kwetu, amewataka wachezaji kucheza kwa nguvu dhidi ya Rayon kama ilivyokuwa dhidi ya Mwarabu pale Uwanja wa Taifa na kuondoka na ushindi.

“Unajua huu mchezo kwetu una uzito mkubwa kwa sababu tunawakilisha Taifa hivyo, tunaposhinda mbali na kumaliza nafasi ya tatu na kupata pesa za Caf, lakini tunaendelea kulinda heshima ya Taifa na Rais wetu, Dk. John Magufuli,” alisema Nyika.

Kwa upande wake, Meneja mpya wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alikiri kuwepo kwa salamu hizo na kueleza kuwa, wachezaji wamejipanga kikamilifiu kuhakikisha tunashinda mchezo huo.

“Hizo taarifa ni sahihi, tumeshaambiwa hilo hakuja mwenyewe lakini tayari zimetufikia, unajua hata kushinda kwetu mechi ile tulikuwa ni kuhakikisha tunatunza heshima ya nchi. Si unajua hata Mweyekiti (Manji) muda mrefu hakuwa ameiona timu yake hivyo, uwepo wake uliongeza hamasa zaidi na matokeo mliyaona wenyewe,” alisema.

Chanzo: mwananchi.co.tz