Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Huku Yondan kule Ambokile Mbeya, Simba iko Dar

33960 Pic+yanga Tanzania Web Photo

Sat, 29 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar/Mbeya. Shughuli ipo leo kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya wakati Mbeya City itakapoialika Yanga, mechi ya Ligi Kuu Bara.

Mchezo wa leo unatarajiwa kuwa mkali na kusisimua lakini macho na masikio ya mashabiki wa soka yatakuwa kwa watu wawili, beki wa Yanga, Kelvin Yondan atakayesimama na mpachika mabao matata wa Mbeya City, Eliud Ambokile.

Ambokile ndiye kinara wa mabao Ligi Kuu akiwa na amefunga mabao tisa sawa na Herieter Makambo na Said Dilunga na kuwaacha Emmanuel Okwi na Meddie Kagere wote wa Simba wenye magoli saba kila mmoja.

Akizungumza na Mwananchi kutoka Mbeya jana, Ambokile alisema licha ya kukosekana baadhi ya wachezaji katika kikosi hicho, anajua kabisa Yanga wana safu nzuri ya ulinzi lakini atajitahidi kuipenya ili afunge.

“Kila mara nina njaa ya mabao, ninachotaka mimi ni kufunga katika kila mchezo ili niwe sehemu nzuri, naiheshimu Yanga kwa sababu wana wachezaji wazuri kwa hiyo inabidi nipambane ili nipenye upande wao.

“Nikicheza kwa nguvu, ninaamini nitafunga, najua wana ngome ngumu na hawataki kupoteza, lakini nitapambana kuhakikisha ninafunga,” alisema.

Yanga ndio vinara wa Ligi Kuu, wanaendelea kuikosa huduma ya kipa Beno Kakolanya ambaye amesimamishwa na kocha wake Mwinyi Zahera, Andrew Vincent anayesumbuliwa na majeraha pamoja na Papy Tshishimbi bado yupo kwao Congo akishughulikia mambo kifamilia.

Simba yaliamsha Dar

Mechi ya Simba dhidi ya Singida United imerudishwa nyuma siku moja kutoka kesho Jumapili na sasa itapigwa leo kuanzia saa 1:00 usiku kwa sababu uwanja wa Taifa utakuwa na matumizi mengine.

Simba iliyokuwa na majukumu ya kimataifa, wanaingia katika mchezo huo na Singida United wakiwa na kumbukumbu ya kuondolewa katika hatua ya awali katika Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Mashujaa ambao waliwafunga 3-2.

Msimu uliopita Simba waliwafunga Singida United katika mechi zote mbili kwani ile ya kwanza ambayo ilipigwa uwanja wa Taifa iliisha kwa Simba kushinda 4-0 wakitoka kufanya vibaya katika kombe la Mapinduzi Zanzibar ambapo waliondolewa katika hatua ya makundi chini ya kocha Masoud Djuma.

Baada ya hapo walikutana tena Mei 12 siku moja mbele mara baada ya Simba kutangaza ubingwa msimu uliopita na walishinda bao 1-0 katika uwanja wa Namfua goli ambalo lilifungwa na Shomary Kapombe ambaye kwa sasa ni majeruhi.

Kocha wa Simba Patrick Aussems alisema: “Nitawatumia wachezaji wote wa kikosi cha kwanza katika mechi hii ili kurudisha morali katika timu kwa kupata ushindi kwani hilo ndio lengo letu,” alisema Aussems ambaye alianza kukinoa kikosi cha Simba mwezi Juni mwaka huu akichukua mikoba hiyo kutoka kwa Mfaransa Pierre Lechantre.

Mastraika wawili wa Simba Meddie Kagere na Emmanuel Okwi wanatazamwa kuwa mwiba katika mechi hii kutokana na kasi yao ya kufunga mabao kwani mpaka sasa kila mmoja amefunga saba huku vinara wakiwa na mabao tisa.

Vinara wa mabao katika Ligi Kuu Bara ni Eliud Ambokile wa Mbeya City, Said Dilunga wa Ruvu Shooting na Herietier Makambo wa Yanga wote wakiwa wamefunga mabao tisa kila mmoja.



Chanzo: mwananchi.co.tz