Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hoja ya Barbara ni fikirishi isijadiliwe kiushabiki

Barbar Pic Data Hoja ya Barbara ni fikirishi isijadiliwe kiushabiki

Sat, 26 Jun 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

USHABIKI wa Simba na Yanga ni wa kipekee na wa kushangaza sana kutokana na hulka na tabia zake.

Linapofika suala linalohusu timu hizo, ni rahisi kuona mtu au shabiki anatoa kauli na maoni ambayo katika hali ya kawaida asingeweza kuyatoa.

Ni rahisi kuona shabiki wa Simba na Yanga akisifia jambo au tukio hata kama halistahili kupewa sifa au ni baya na lisilofaaa ilimradi limefanywa na upande wake lakini kwa upande mwingine unaweza kuona akikosoa na kukejeli jambo zuri na linalostahili sifa kwa vile tu limefanywa au linahusu upande wa pili.

Mahaba kwa hizo timu mbili kubwa na kongwe hapa nchini ni ya kupitiliza kiasi cha kupelekea hata wale ambao pengine wana uelewa mpana wa masuala ya soka au elimu ya juu, kuamua kuweka kando joho hilo na kuvaa lile ambalo linavaliwa na wale ambao wamewaacha mbali kieleimu na kiupeo.

Tunaweza kulishuhudia hili kwa kutazama mjadala ulioibuka hivi karibuni baada ya mtendaji mkuu wa klabu ya Simba, Barbara, Gonzalez kutoa mtazamo wake kupitia ukurasa wa mtandao wa Twitter juu ya ugumu ambao klabu zinapata kuishi na wachezaji wasiojituma.

Barbara aliandika hivi, “ni hatari sana kushikilia wachezaji ambao hawana uchu wa mafanikio na njaa ya kutaka kucheza.”

Hoja hiyo ya Barbara imezua mijadala tofauti. Wapo wanaoiunga mkono lakini pia imepata wakosoaji ambao wameipinga

Sio dhambi kwa hoja kupingwa lakini kwa suala la Barbara wengi wanamkosoa kwa mlengo wa kishabiki kwa vile tu ni mtendaji wa Simba na pengine wao sio wapenzi wa klabu hiyo lakini bado hawaonyeshi udhaifu au mapungufu ya hoja aliyoibua.

Kundi kubwa la wakosoaji linadai kwamba Barbara hakupaswa kutoa maoni kama yale hadharani kutokana na nafasi yake klabuni na kwa kufanya hivyo ni kama anawashambulia watumishi wa klabu ambao wako chini yake.

Lakini ukiitazama kwa umakini hoja ya Barbara, andiko lake linaweza kutafsirika na wengi kama linahusu wachezaji wa Simba lakini kiuhalisia linawagusa wachezaji wengi wa Kitanzania juu ya mwenendo wao kinidhamu na ufanisi na mchango wao katika timu.

Kundi kubwa la wachezaji wetu wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la kutojitambua na kufahamu wajibu wao katika timu na wanahisi wao ndio wenye haki ya kuchuma tu kutoka katika timu pasipo wao kuzalisha.

Mishahara mikubwa na stahiki nyingine wanazopata katika timu pengine bila hata kutoa mchango mkubwa au kuzisaidia timu, wanaona kama ni haki yao lakini hawaoni kama nao wanapaswa kuwajibika kwa kuhakikisha timu zinafanya vizuri.

Hii inapelekea wengi wao kuridhika na kushindwa kujitolea na hivyo kuzipa mzigo mkubwa klabu katika kuwahudumia pasipo kuingiza kitu kupitia wao. Kwa maana nyingine unaweza kutafsiri kuwa klabu zetu zimekuwa zikihudumia watumishi hewa wengi ambao hazinufaiki na jasho lao.

Kwa bahati mbaya kwa muda mrefu klabu zetu zimekuwa zikiwalea wachezaji ambao hawaonekani kujitolea kwa ajili ya timu na wanakula mishahara na posho za bure huku wenzao wachache wakivuja jasho kusaka mafanikio ambayo mwisho wa siku yanaonekana kuwa ya wote.

Katika dunia ya sasa ambayo soka ni biashara, klabu kuendelea kuwa na wachezaji wa namna hiyo wasiojituma na wanaoishi kama kupe, ni jambo ambalo halipaswi kuendekezwa na muda umefika kwa klabu kutowapa kipaumbele na kuwaonyesha mlango wa kutokea kuliko kuendelea kuingia hasara kwa sababu yao.

Soka letu haliwezi kupiga hatua kama wachezaji wetu hawaoni wivu wa kimaendeleo kwa wenzao wanaocheza na kufanya vizuri na badala yake litazidi kurudi nyuma huku tukiendelea kulalama pasipo kuchukua hatua.

Leo hii Tanzania inakosa idadi kubwa ya wachezaji wanaocheza soka la kulipwa katika ligi za ushindani Afrika na duniani kiujumla sio kwa sababu ya uwezo mdogo wa wachezaji wetu bali ni hii tabia ya uvivu na kuridhika ambayo Barbara ameibuka na kuizungumza hadharani.

Hawaoni haja ya kuondoka hapa nchini kwa sababu kuna maisha rahisi na yasiyo na presha kubwa kwao pale wanaposhindwa kufanya vyema au kujituma kulinganisha na huko ambako hawataki kwenda.

Tusiitazame hoja ya Barbara Gonzalez kama ameilenga Simba tu. Ameonyesha tatizo sugu ambalo lipo kwa klabu zote kuanzia zile za Ligi Kuu hadi za mchangani.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz