Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hofu, ulevi chanzo mashabiki Simba, Yanga kuzimia uwanjani

99016 Pic+ulevi Hofu, ulevi chanzo mashabiki Simba, Yanga kuzimia uwanjani

Mon, 16 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Huwa inashangaza kwa nini zinapocheza timu za Simba na Yanga mashabiki wengi wa soka huzimia, tofauti na zinavyocheza timu nyingine.

Matukio hayo yamekuwa yakijirudia, lakini hali huwa tofauti timu hizo mbili kongwe nchini zinapokutana na nyingine.

Katika mchezo wa Simba na Yanga uliochezwa Jumapili iliyopita katika Uwanja wa Taifa na vijana wa Jangwani kuibuka na ushindi wa bao 1-0, kulijitokeza matukio ya namna hiyo.

Baadhi ya mashabiki, kati ya 59,325 walioingia kuangalia mchezo huo, walipatwa na matatizo tofauti kama kuzimia.

Mwenyekiti wa Tasma na mwenyekiti wa Kamati za Tiba za TFF ambaye katika mchezo huo alikuwa daktari wa mchezo, Lisobine Kisongo anasema kulikuwa na kamati maalumu ya kutoa huduma ya kwanza.

“Suala la tiba katika mkusanyiko wa watu wengi kama mechi ya Simba na Yanga, kutokea kwa majanga na vitu vingine tofauti ni kawaida, ndiyo maana kunakuwa na maandalizi ya kutosha kwa ajili ya uokoaji kama red cross, skauti na wengine,” anasema Kisongo.

Pia Soma

Advertisement
Alisema lengo ni kuona namna gani tunaweza kwenda sawa na tukio lolote litakalojitokeza ndani ya muda huo pamoja na vifaa.

Pia alisema walikuwa na magari matatu wagonjwa ili kufanya uokoaji na matibabu kwa haraka.

“Ambulance zinakuwa na kila kitu kwa ajili ya matibabu ingawa kwa baadaye tunataka zenye ubora zaidi. Tulikuwa wahudumu wa red cross 40, idadi ambayo ni kubwa,” anafafanua.

Watu waliozimia

Mashabiki 22 walitibiwa, idadi ambayo imeongezeka tofauti na ilivyokuwa mzunguko wa kwanza uliomalizika kwa sare ya 1-1.

Kati ya wagonjwa hao, wanawake walikuwa 12 na wanaume 10. Wawili kati yao, walipelekwa Temeke kwa ajili ya uangalizi zaidi na walipotibiwa waliruhusiwa kwenda nyumbani.

“Wagonjwa tuliowapokea walikuwa na matatizo tofauti, wapo waliong’atwa na mbwa, kupasuliwa kwa kupigwa; hao wa kuzimia walikuwa wengi zaidi.

“Waliong’atwa na mbwa walikuwa wawili mwanaume na mwanamke,” anasema mmoja wa watu wa huduma ya kwanza.

“Mechi ya kwanza idadi ya wagonjwa ilikuwa ndogo, walikuwa 13, wanane kati yao walipekewa hospitali kwa matibabu zaidi,” anasema.

Kwa mujibu wa mavazi waliyovaa, wengi waliozimia walikuwa Simba.

Mashabiki wa Simba hujulikana na sare za rangi nyeupe na nyekundu na Yanga huvaa njano na kijani.

Daktari wa Azam FC, Mwanandi Mwankemwa, anasema: “Hiyo yote ni kutokana na kilichotarajiwa kuwa tofauti na kilichotokea. Inawezekana mashabiki wa Simba waliamini watashinda kutokana na ubora wa timu yao, lakini matokeo yakawa kinyume, ndio maana wengi walizimia.”

Ulevi wachangia

Mmoja wa madaktari aliyekuwa zamu katika mchezo huo ambaye huwatibu wachezaji wa Taifa Stars, Emily Urasa anasema, katika uchunguzi wake aligundua ulevi ni moja ya sababu iliyofanya baadhi ya mashabiki hao kuzimia hovyo uwanjani.

“Unakuta shabiki anaingia uwanjani huku akiwa amelewa hajitambui, anapokutana na mtikisiko kidogo wa mechi anazimia. Sitanii, wapo ambao walipokuja kuzinduka tuligundua sababu ilikuwa pombe,” anasema.

Hofu, matarajio tofauti

Daktari wa Azam FC, Mwanandi Mwankemwa, anasema kitu kikubwa kinachosababisha wagonjwa wengi wa kuzimia ni mshtuko.

“Mtu anapopata habari ya kushtua anapata mshtuko. Wapenzi wa Simba na Yanga wanapokwenda uwanjani kutokana na mapenzi na imani waliyonayo na timu zao, wanapokutana na matukio tofauti na walichokitegemea mambo yakuwa tofauti,” anasema Mwankemwa.

“Mfano mdogo, kuna tukio la watoto mapacha, Kulwa alifariki dunia; Doto alipopewa taarifa kutokana na mshtuko na yeye alikufa kukawa na misiba miwili. Iko hivyo kwa wapenzi wa soka, shabiki anakwenda akiamini timu yake inashinda, mwisho wa siku wanafungwa, ndipo mambo ya kuzimia kama hivyo yanatokea.”

Shabiki azungumza

Mmoja wa shabiki wa Yanga maarufu kwa jina la Bakhresa anasema: “Kikubwa kinachosababisha ni mapenzi ya timu. Unapokwenda uwanjani unategemea timu yako kushinda na inapofungwa unakosa amani kama huna ustahimilivu, ndipo unakutana na matukio ya namna hiyo.”

Chanzo: mwananchi.co.tz