Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hivi unajua kwanini unahitaji ufanye mazoezi?

44805 Mazoezi+pic Hivi unajua kwanini unahitaji ufanye mazoezi?

Tue, 5 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Katika maisha ya kila siku tunashauriwa kufanya mazoezi mara kwa mara ili kujenga afya ya mwili kwa ujumla lakini si wote ambao wanajua ni kwanini tunahitaji kufanya mazoezi.

Kitabibu ili kujenga mwili na afya inahitajika kutumia dakika 150 kwa wiki kufanya mazoezi mepesi yanayojulikana kitabibu kama Aerobics yaani dakika 30 kwa siku kwa siku 5 za wiki.

Dondoo zifuatazo zinakupa ufahamu wa faida za kiafya ambazo ndizo zinazofanya mwanadamu kuhitajika kufanya mazoezi mara kwa mara.

Kupunguza hatari ya kupata magonjwa yasiyoambukiza ikiwamo magonjwa ya moyo, kiharusi, saratani na kisukari kwa sababu mazoezi yanasaidia kuwa na mfumo wa Moyo na damu wenye afya njema.

Kudhibiti unene ambao ni kihatarishi cha kupata magonjwa mbalimbali, mazoezi huushughulisha misuli na kuchoma mafuta yaliyorundikana na pia kuufanya mwili kuwa imara na kudhibiti uzito.

Kushusha shinikizo la damu kwasababu mazoezi yanasababisha kuwa na moyo na mishipa ya damu yenye afya njema hivyo kukukinga na shinikizo la juu la damu.

Kufanya mazoezi kama kutembea, kukimbia na kuogelea kunasaidia mtawanyiko mzuri wa oksijeni mwilini na vile vile kutumika katika mapafu na damu kwa ufanisi.

Kuimarisha misuli na kukupa ukakamavu wa mwili kwani mazoezi yanaifanya misuli kuwa imara na iliyojengeka.

Kusaidia maungio na viungo vya mwili kuwa na wepesi hivyo kufanya matendo mbalimbali na kupunguza hatari ya kupata majeraha kirahisi.

Mazoezi ni moja ya mambo yanayorekebisha na kuondoa hisia hasi ikiwamo hasira, huzuni na msongo wa mawazo na shinikizo.

Kupunguza hatari ya kupata saratani, tafiti zinaonyesha wanaofanya mazoezi hatari ya kupata saratani za ziwa, utumbo mpana na mapafu ni ndogo.

Kudhibiti lehemu au cholestrol (mafuta) kwani mazoezi yanapunguza kiwango cha lehemu mbaya na kuongeza kiwango cha lehemu nzuri mwilini ambayo ina faida mwilini.

Husaidia kuwa na mifupa imara iliyojengeneka hivyo kupunguza hatari ya kupata tatizo la kumomonyoka mifupa lijulikanalo kitabibu kama osteoporosis.

Kuimarisha kinga ya mwili, kadiri unavyofanya mazoezi mara kwa mara na ndivyo hatari ya kuumwa na magonjwa mbalimbali inavyopungua.

Mazoezi yanachangia kupata usingizi mnono, usingizi una faida kwa mwili ikiwamo kusahihisha hitilafu za mwilini, kujenga kinga na mwili.

Husaidia kuboresha afya ya akili, kwani humfanya mtu kuondokana hisia za hofu, woga, sonona (depression) na vile vile kuongeza umakini na kujiamini.

Kujenga utegemezi na mazoezi, mtu akiyakosa hujiona hayuko sawa kimwili hivyo hulka hii kuwa na faida ya kumuepusha mtu na vishawishi mbalimbali ikiwamo utumiaji tumbaku, ulevi na uasherati.

Kuondoa taka sumu mwilini kwa njia ya ngozi, wakati wa mazoezi jasho hutoka kwa wingi ambayo hutoka na taka hizo hivyo kuboresha afya ngozi na mwili kiujumla.

Kuondoa uchovu wa mwili, mazoezi magumu huweza kuleta uchovu wa viungo lakini mazoezi mepesi huondoa uchovu hivyo kukupa utulivu wa mwili na akili.

Kuimarisha tendo la ndoa, mazoezi huwa na faida kutokana kuongeza uimara wa misuli ikiwamo ile ya misuli ya kitako cha kiuno ambayo inaongeza ufanisi katika tendo.

Kuishi maisha marefu, ujumla wa faida hizi zote ndizo zinazochangia wanaofanya mazoezi kuwa na afya njema hivyo kusababisha kuishi muda mrefu.



Chanzo: mwananchi.co.tz