Kocha Mkuu wa klabu ya Simba, Hitimana Thierry amefunguka vitu vinavyopelekea Simba kupata matokeo kwa mbinde kwenye michezo ya Ligi kuu ya NBC Tanzania.
Hitimana amesema, kwanza washambuliaji wake hawamalizii nafasi wanazotengeneza, kukosa muda wa maandalizi ya mchezo ili kurekebisha mapungufu hayo pamoja na kuwa na wachezaji wengi wenye majeraha.
Akizungumza mbele ya wanahabari baada ya mchezo wa Simba 1-0 Namungo kumalizika, Hitimana amesema:
"Nafikiri Ligi yenyewe unaiona, Ligi ni ngumu. Kipindi tunachopitia kwasasa ni kipindi chetu kigumu. Bila kusahau, Kama Simba imemaliza miaka 4 iko kipindi kizuri, kwahiyo nafikiri ni transition ambayo inabidi tuangalie jinsi ya ku-manage vizuri"
"Kimchezo kweli tumacheza. In terms za ku-create chance tunapata, Lakini finishing inakuwa kama hainatukubalia. Na bahati mbaya, Unajua tulivyomaliza mechi ya Galaxy hatukuwa na muda tukaanza hivi viporo ambavyo ni kila baada ya siku tatu"
"Hakuna muda ambao unaweza sema utachukua striker uwafundishe hiki na hiki hakuna. Ni namna ya kumange kuangalia nini kinafuata. Nafikiri cha muhimu ni kupata hizo point tatu kwanza hata kama tumechelewa kupata point tatu"
Baada ya kusema hayo huku akiwa mwenye upole mkubwa, Hitimana aliendelea kugusia suala la majeraha linavyoisumbua timu yake kupata aina ya uchezaji hata matokeo uwanjani.
"Point ya pili, tuna majeraha wengi sana. Kila mechi watu wanabadilika. Wakina Mugalu, wakina Kanoute, Wakina Mzamiru, Taddeo. Ni lazima hata style ya uchezaji itapungua lakini hatutakaa kulalamika wale ambao hawapo, lazima tuwatumie ambao wapo" Hitimana amesema.
Mwisho akamaliza kwa kusema atatumia muda wa mapumziko ya takribani majuma mawili kurekebisha mapungufu yanayoikabili Simba.
"Katika kipindi hiki cha mapumziko, tutakaa tutizamane tuangalie kila kinafuata"
Simba inashika nafasi ya pili kwa kuwa na alama 11, utofauti wa alama 3 na kinara Yanga baada ya wawili hao wote kucheza michezo yao mitano ya mwanzo kwenye msimu mpya wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania.