Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Himid aeleza tamu, chungu maisha Misri

9245 PIC+HIMID TanzaniaWeb

Wed, 1 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Baada ya kupambana muda mrefu akicheza soka ya ridhaa, hatimaye Himid Mao ‘Ninja’ amekuwa miongoni mwa wachezaji wa Tanzania wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi.

Baada ya kuiongoza vyema Azam akiwa ndiye nahodha wa kikosi hicho, Himid amepanua wigo na kuongeza idadi ya wachezaji wa Tanzania wanaocheza soka la kulipwa.

Kiungo huyo mkabaji, anafuata nyayo za nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta ambaye anatamba katika kikosi cha KRC Genk ya Ubelgiji, baada ya kung’ara TP Mazembe Englebert ya DRC Congo.

Kiungo huyo ambaye ni mtoto wa nyota wa zamani wa Pamba ya Mwanza, Mao Mkami, alikuwa na ndoto ya kucheza soka nje ya nchi ingawa mara kadhaa aliwahi kuhusishwa na Yanga.

Pamoja na kuhusishwa na Yanga, shauku ya Himid ilikuwa kucheza soka la kulipwa ndiyo maana kwa nyakati tofauti aliondoka nchini kwenda kufanya majaribio kwenye klabu za Randers inayoshiriki Ligi Kuu Denmark na Bidvest Wits ya Afrika Kusini.

Baada ya kugonga mwamba, Himid hakukata tamaa aliendelea kucheza kwa kiwango bora katika Ligi Kuu akiwa na kikosi cha Azam hadi msimu uliopita.

Baada ya kupambana muda mrefu, Himid amejiunga na Petrojet FC inayoshiriki Ligi Kuu Misri na tayari ameanza kuonyesha makeke nchini humo.

Nyota huyo amefanya mazungumzo na gazeti hili kuzungumzia maisha mapya anayoishi Misri na changamoto anazokutana nazo ndani na nje ya uwanja.

Katika mazungumzo hayo na jarida hili la Spoti Mikiki, Himid anasema ameanza kupata mafanikio na matarajio yake ni kutimiza malengo aliyoweka miaka mitano iliyopita.

“Lengo lilikuwa kucheza soka la kulipwa Ulaya, lakini mambo yamekwenda tofauti kwa hiyo imebidi niwe na njia mbadala ambayo ni kupitia huku Misri ambako wachezaji wengi wanaofanya vizuri wanakwenda kwa wepesi.

“Msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara ilivyomalizika ilibidi nije huku kumalizana nao kwasababu walionyesha nia ya kunihitaji muda mrefu nilivyofika tulikubaliana baadhi ya mambo na kusaini.

“Wachezaji wengi wa huku wanazungumza Kiarabu hiyo ni changamoto ambayo nilitegemea lakini nashukuru Mungu wapo wachache ambao wanaongea Kingereza,” anasema Himid.

Mchezaji huyo anadokeza changamoto nyingine ambazo ni tofauti ya vyakula kati ya wenyeji wageni.

Joto pia ni miongoni mwa changamoto ambazo Himid amekutana nazo Misri, lakini amekuwa akipambana nalo kwa kuwa ni sehemu ya maisha.

Akizungumzia namna alivyopokewa na wachezaji wenzake wa Petrojet , Himid anasema alifarijika baada ya kupata mapokezi mazuri.

“Nilichangamkiwa na kila mmoja alinikaribisha kwa lugha ya Kingereza ingawa kilikuwa cha kubabaisha kwa wale ambao walikuwa hawana uwezo mzuri wa kukiongea, benchi zima la ufundi lilinipokea vizuri,” anasema Himid.

Kiungo huyo mkatabaji ambaye pia ana uwezo wa kucheza kama beki wa kati au mlinzi wa pembeni (2), amepanga kutumia vyema fursa aliyopata ya kucheza Ligi Kuu Misri kuwa daraja la kumvusha kwenda Ulaya.

Himid anayesifika kucheza kibabe, alianza kucheza soka ngazi ya chini ya timu ya vijana ‘Azam Academy’ iliyotwaa ubingwa wa mashindano ya vijana ‘Uhai Cup mara mbili mfululizo’.

Pia ametoa mchango kwenye makombe mengine ya Azam FC, kama vile Kombe la Ujirani Mwema mwaka 2012 nchini Congo DRC, Kombe la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2013/2014, walilotwaa bila kufungwa.

Nyota huyo pia amechangia mafanikio ya Azam kutwaa ubingwa wa Kombe la Kagame Agosti, 2015 kwa rekodi ya aina yake ya kutofungwa bao na mchezo wowote.

Himid ambaye ni nahodha msaidizi wa Taifa Stars, amepitia timu zote za vijana za Tanzania za miaka chini ya 17, 20 na 23 akiwa mmoja wa wachezaji tegemeo.

Kocha wa zamani wa Taifa Stars, Marcio Maximo raia wa Brazil, ndiye aliyemuibua Himid katika Kituo cha Kukuza Vipaji cha TSA na kumjumuisha mara kadhaa katika kikosi cha wakubwa kupata uzoefu.

Himid ni wa mtoto wa kwanza kuzaliwa kati ya watoto watano akiwa na ndugu zake Femina, Rozmana, Feisal na Rahim.

Elimu yake ya msingi alipata katika Shule ya Msingi Kiwandani, Turiani, Morogoro darasa la kwanza na la pili na kuhamia Karume ya Dar es Salaam aliposoma hadi darasa la sita.

Mchezaji huyo alihama na kumalizia elimu ya msingi Shule ya Msingi ya Dk. Omary Ali Juma iliyopo Magomeni, Dar es Salaam kabla ya kujiunga na Shule ya Sekondari ya Tabata ambako alimaliza kidato cha nne mwaka 2011.

Chanzo: mwananchi.co.tz