Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Himid Mao awapa Simba siri za Al Ahly

35085 Pic+himid Himid Mao

Mon, 7 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kiungo wa Tanzania anayecheza soka ya kulipwa nchini Misri na klabu ya Petrojet ya Ligi Kuu ya nchini humo, Himid Mao ameipa Simba ujanja itakapoikabili Al Ahly ya nchini humo mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba itapambana na JS Saoura ya Algeria Jumamosi ijayo katika mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mabingwa hao wa Tanzania wamepangwa Kundi D pamoja na Al Ahly ya Misri na AS Vita ya DR Congo ambayo itacheza mchezo wa pili na Simba mjini Kinshasa na baadaye Al Ahly Dar es Salaam.

Akizungumza na Mwananchi kutoka Cairo, Mao aliitahadharisha Simba kujipanga kwa kuwa Al Ahly kwa sasa inarudisha makali yake ya zamani.

Mao aliyeifungia Petrojet mabao mawili ilipoilaza ENPPI 2-1 mechi ya robo fainali Kombe la Misri juzi alisema kuwa wamejikita kwenye usajili lakini bado wanakikosi kizuri chenye uwezo wa kushindana.

“Simba wajipange kweli, sisemi kinazi, jamaa nawaona huku wana kikosi cha kushindana kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kama ilivyokuwa msimu uliopita.

“Wanacheza soka la kushambulia, upigaji wa pasi nyingi kwao ni kitu cha kawaida. Zile pasi zina lengo la kuwachanganya na mkiachia upenyo wanawaadhibu kwa kuwa pasi zao wanasogea golini,” alisema Mao kwa kifupi.

Desemba Mosi mwaka jana, Petrojet ilifungwa bao 1-0 na Al Ahly kwenye mchezo wa Ligi Kuu Misri. Miamba hiyo ya Misri inayoshika nafasi ya sita sita katika msimamo, juzi ilichapwa mabao 2-1 na Pyramids mchezo wa ligi hiyo.

Msuva wapa Simba fleva za waarabu

Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Saimon Msuva anayeichezea Difaa El Jadida ya Morocco naye amewamegea siri Simba SC ya namna ambavyo wanatakiwa kuwa makini na soka la timu za Waarabu.

Msuva ambaye alikuwa akiichezea Yanga hapa nchini kabla ya kujiunga na Waarabu hao wa Morocco, anadai kulifahamu vizuri soka lao ambalo halikumchukua muda kuendana nalo.

“Nilipokuja hapa Morocco kichwani kwangu nilikuwa nina mawazo ya kuwa jamaa ni watu wa kujiangusha ovyo ovyo, nilihisi pia hawana nguvu yaani wamelegea kwa hiyo nilipania kucheza soka la kukamia. “Mawazo yangu yalikuwa tofauti na uhalisia, ni kweli huwa wanajiangusha lakini sio kila wakati hutumia mbinu hiyo kupoteza muda kwenye michezo muhimu hasa wakiwa ugenini.

“Hii wanautumia wakitangulia kufunga kwa hiyo wajitahidi kutotoa nafasi za wao kuwatangulia, wanaweza kujikuta kwenye dakika 90 kiuhalisia zikachezwa 60 au 70, nyingine wakazipoteza wao, “ alisema Msuva. Nyota huyo wa Kitanzania, alisema Waarabu wanapenda kucheza kwa kumiliki mpira kwa kiasi kikubwa ni ngumu kushindana nao kwenye eneo hilo, Simba wanatakiwa kuanza kukabia juu ili kuwapa presha.

Msuva alisema kukabia juu kwa nguvu kutawalazisha kufanya makosa na wakisema wakabie chini kwa maana ya kwenye eneo lao kutawaweka kwenye mazingira ya kupoteza labla wawe na ukuta imara.

Msuva akiwa na Difaa El Jadida msimu uliopita ambao aliipachikia klabu yake hiyo mabao 11 kwenye Batola Pro, alisema kilichokuwa nyuma ya mabao aliyokuwa akifunga ni presha ambayo alikuwa akiitengeneza kwa mabeki wa Kiarabu.

“Mbali na presha ya kukaba pia kasi yangu ilikuwa ikiwafanya washindwe kunidhibiti kwa hiyo washambuliaji wa Simba wanatakiwa kusogea kwa kasi wakati wakishambulia.

“Uzuri Simba wanaye Shiza Kichuya ana mbio na anaweza akatumika na mwisho wa siku hata kama asipofunga anaweza kuwatengenezea wengine,” alisema Msuva. Pia kitu kingine ambacho Msuva alisema Simba wanatakiwa kuwa makini ni namna yao ya umiliki mipira hasa wakiwa kwenye eneo lao la hatari wanatakiwa kuwa nao makini maana ni wepesi kujiangusha kwa hiyo wanaweza kuwapa penalti za kizembe.

Pamoja na Msuva kukutana kwake na timu kadhaa za Morocco, msimu uliopita alikutana na klabu za Algeria kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo alipangwa nazo Kundi B, ambazo ni ES Sétif na MC Alger.



Chanzo: mwananchi.co.tz