Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hiki ndicho kilichoiua Uganda

48627 UG+PIC

Tue, 26 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Hakuna namna unayoweza kutenganisha ushindi wa mabao 3-0 iliyopata Taifa Stars dhidi ya Uganda juzi, ulioipa tiketi ya kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) na mchango mkubwa wa mshambuliaji John Bocco katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Licha ya kutofunga bao, Bocco alifanya kazi kubwa kuanzia mwanzoni mwa mchezo hadi alipotolewa dakika ya 80 na nafasi yake kuchukuliwa na kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’.

Bocco alionyesha nidhamu ya kimbinu kwa kutimiza vyema majukumu aliyopewa akianzishwa kama winga wa kulia badala ya mshambuliaji wa kati kabla ya baadaye kuhamishiwa upande wa kushoto baada ya kutoka Farid Musa.

Bocco alishuka kusaidia mabeki wa pembeni, Hassan Kessy, Gadiel Michael na alipanda mbele haraka Taifa Stars ilipokuwa na mpira jambo lililoongeza idadi kubwa ya washambuliaji katika eneo la ulinzi la Uganda na kuwaweka mabeki wa timu pinzani katika wakati mgumu.

Alitumia vyema nguvu zake katika kukabiliana na mabeki wa Uganda, alipiga pasi ambazo zilifika kwa walengwa kwa usahihi na ndiye alichangia bao la kwanza na la tatu kwa kupiga pasi za mwisho kwenda kwa Saimon Msuva na Aggrey Morris waliofunga.

Kiwango bora alichoonyesha dhidi ya Uganda ni muendelezo wa kazi kubwa anayofanya ndani ya uwanja katika siku za hivi karibuni kwenye mechi kubwa alizocheza.

Bocco ndiye alipiga pasi iliyozaa bao la ushindi katika mchezo wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baina ya Simba na Al Ahly kabla ya kufanya hivyo katika mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Yanga. Nyota huyo alipachika moja ya mabao katika ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Azam.

Pia alipiga pasi mbili za mwisho katika ushindi muhimu wa Simba wa mabao 2-1 dhidi ya AS Vita uliowavusha robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kingine kilichoibeba Taifa Stars ni uimara wa timu kuanzia safu ya ushambuliaji hadi ulinzi uliotokana na juhudi na kiwango bora cha mchezaji mmoja mmoja.

Safu ya ulinzi ilipunguza idadi ya makosa ambayo yangeweza kuipatia Uganda bao jambo lilichangiwa na umakini. Pia safu ya kiungo iliunganisha na kuichezesha vyema timu, kuziba njia na kutibua mipango ya Uganda jambo lililowapa kazi rahisi washambuliaji kupeleka mashambulizi langoni mwa wapinzani wao.

Pamoja na hilo, hamasa ya umati wa mashabiki zaidi ya 60,000 waliojitokeza kwenye Uwanja wa Taifa ilichangia kuongeza morali kwa wachezaji na kuwafanya wajitume ili kutimiza ndoto ya Watanzania ya kufuzu fainali hizo kwa mara ya pili.

Mchango wa nyota wanaocheza soka ya kulipwa nje ya nchi hasa nahodha Mbwana Samatta, uliipa nguvu Taifa Stars kwani wachezaji hao walionyesha utofauti kwa kucheza kwa kujiamini, kufanya uamuzi wa haraka walipokuwa na mpira, uwezo wa kuwasoma nyota wa Uganda na kuwanyima uhuru wa kukaa na mpira muda mrefu.

Kauli za makocha

Kocha Emmanuel Amunike alisema amefurahi kuona ndoto yao ya kufuzu katika mashindano hayo imetimia.

“Ndoto imetimia.Tuliongea sana kuhusu mechi hii na umuhimu wa kufuzu na leo (juzi) tumefuzu.

“Jambo zuri ni kuona timu nne kutoka Afrika Mashariki zimefuzu na zitawakilisha katika mashindano hayo.

“Tunawashukuru mashabiki kutusapoti wameonyesha wanavyoijali timu kwa kujitokeza kwa wingi na kuchangia ushindi huu. Sitaongea mambo ya kiufundi kwa kuwa ni muda wa kusherehekea,”alisema Amunike.

Kocha wa Uganda Sebastien Desabre alisema mechi ilikuwa ngumu kwao na walishindwa kuhimili hali ya mchezo kwa muda mrefu huku akidai baadhi ya wachezaji wake walikuwa na kadi za njano zilizoathiri kikosi.

“Licha ya kwamba kabla ya mchezo huu tulilkuwa tumefuzu lakini mipango yetu ilikuwa kushinda Hata hivyo hatukuweza kuikabili hali ngumu ya kimchezo.Pia baadhi ya wachezaji wangu walikuwa na kadi mbili za njanohivyo sikuweza kuwatumia”alisema

Timu 24 Afco

Tanzania,Uganda,Senegal,Madagascar,Morocco,Cameroon,Mali,Burundi,Algeria Benin,Nigeria,Afrika Kusini,Ghana,Kenya,Zimbabwe,DRC Congo,Guinea, Ivory Coast,Angola,Mauritania,Tunisia, Misri,Guinea-Bissau,Namibia.

Takwimu

Upangaji wa kikosi kilichoanza ulitoa picha ya wazi ya kuwa benchi la ufundi la Stars lilijua umuhimu wa kupata ushindi kwenye mchezo wa jana.

Tofauti na mechi zilizopita, kocha Emmanuel Amunike alianzisha kundi kubwa la wachezaji ambao kiasili ni washambuliaji.

Makala hii inakuletea tathmini ya namna mchezaji mmoja mmoja wa Stars alivyotoa mchango katika mchezo wa jana.

Aishi Manula-7

Hakuna na kazi ngumu kwenye mchezo wa jana kwani Uganda hawakuwa na madhara makubwa pindi walipokuwa langoni mwa Stars.

Hata hivyo alifanya kazi ya ziada mwanzoni mwa kipindi cha pili baada ya kuokoa shuti la mbali la Moses Waisswa ambalo lilionekana kama lingekuwa bao.

Hassan Kessy-6

Alikosa utulivu katika dakika za mwanzoni za mchezo akifanya makosa kadhaa ambayo yangeweza kuipatia Uganda bao lakini baadaye alitulia na kutimiza vyema majukumu yake.

Licha ya mwanzoni kuonekana kwenye hatari ya kuonyeshwa kadi nyekundu baada ya kuonyeshwa kadi ya njano dakika za mapema.

Gadiel Michael-7

Alitengeneza muunganiko mzuri upande wa kushoto sambamba na Farid Mussa jambo lililovunja nguvu ya Uganda upande wa kulia.

Alitimiza vyema jukumu la kulinda na alipanda mara kwa mara kusaidia mashambulizi kwa kupiga krosi nzuri ambazo hata hivyo ziliokolewa na mabeki wa Uganda.

Kelvin Yondani-7

Alimdhibiti vilivyo mshambuliaji Patrick Kaddu hasa kwenye mipira ya juu ambayo imekuwa ikitumiwa vyema na nyota huyo wa Uganda katika kufunga mabao yake.

Alijitahidi kucheza kwa nidhamu kubwa na baada ya Stars kupata mabao matatu hakutaka kuona mpira ukizagaa langoni mwake.

Aggrey Morris-8

Alikuwa imara katika kukabiliana na Farouk Miya ambaye kabla ya mchezo ndiye alionekana ni miongoni mwa nyota hatari zaidi katika kikosi cha Uganda.

Juhudi zake binafsi zilimuwezesha kuifungia Stars bao la tatu baada ya kupiga kichwa kilichojaa wavuni akiunganisha krosi ya John Bocco lakini ni yeye Morris aliyeanzisha shambulizi hilo kwa kumpasia mpira Bocco kutokana na mpira wa faulo.

Erasto Nyoni-8

Aliituliza vyema timu na kuziba mianya kwa viungo wa Uganda kupenyeza mipira. Aliwachezesha vizuri wenzake kutokana na pasi zake ambazo zilifika kwa usahihi.

Alifunga kwa ustadi mkwaju wa penati uliozaa bao la pili kwa Stars ambalo lilishusha presha ya umati wa mashabiki uliojitokeza uwanj wa Taifa.

John Bocco-8

Amezoeleka kucheza kama mshambuliaji wa kati lakini jana alipangwa kama winga wa kulia nafasi ambayo aliitendea haki vilivyo kwani alimlazimisha beki wa kushoto wa Uganda, Godfrey Walusimbi kutopanda mbele.

Nguvu na uwezo wake wa kumiliki mpira vilimfanya awe tishio kwa safu ya ulinzi ya Uganda. Alipiga krosi nyingi kuelekea langoni mwa Uganda na ndiye aliyepiga pasi iliyozaa bao la kuongoza la Stars lakini pia ndiye alipiga krosi iliyounganishwa kwa kichwa na Aggrey Morris na kuandika bao la tatu.

Mudathir Yahya-6

Alijitahidi kuunganisha na kuichezesha timu huku akishuka mara kwa mara chini kusaidiana na Erasto Nyoni katika kuilinda safu ya ulinzi ya Stars.

Hata hivyo kuna nyakati alionekana kukosa umakini na kupoteza pasi jambo ambalo liliiweka matatani Stars ingawa wachezaji wenzake walijitahidi kumfichia udhaifu wake

Mbwana Samatta-8

Alionyesha ustaa wake kwa namna alivyokuwa anaufungua ukuta wa Uganda kwa chenga na uamuzi wake haraka pindi alipokuwa na mpira ambapo pale alipotakiwa kupiga pasi alifanya hivyo pasipo kuchelewa lakini pale palipokuwa na ulazima wa kukokota hakusita kufanya hivyo na kwa usahihi mkubwa.

Alionekana ndiye mchezaji aliyeogopwa zaidi na ukuta wa Uganda uliiongozwa na kipa Dennis Onyango. Na ndiye alisababisha penati iliyozaa bao la pili la Stars.

Saimon Msuva-9

Kasi yake ilionekana kuwapa tabu mabeki wa kati wa Uganda ambao maumbo yao makubwa yalionekana kuwafanya wacheze taratibu.

Alikuwa mwepesi wa kuingia kwenye eneo la hatari la Uganda na kufanya maamuzi na hilo lilizaa matunda mnamo dakika ya 20 alipoinasa pasi ya Bocco na kufanya uamuzi wa haraka wa kupiga shuti lililozaa bao la kuongoza.

Farid Mussa-7

Pengine kuanzishwa kwake kuliwashangaza wengi kwani kwa muda mrefu amekuwa hapati nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza cha Stars.

Hata hivyo hakuliangusha benchi la ufundi lililomuamini alifanya kazi kubwa na nzuri iliyozaa matunda. Kwanza alishuka kwa haraka kumsaidia beki wake Gadiel Michael lakini pindi Stars ilipokuwa na mpira alikaa kwenye nafasi sahihi na kufanya maamuzi ya haraka yaliyowasumbua Uganda.

Pasi zake zilifikia walengwa kwa usahihi na kasi pamoja na uwezo wake wa kumiliki mpira, kukokota na kupiga chenga vilimfanya Nico Wadada kutopanda.

Walioingia

Himid Mao-5

Aliingia kuchukua nafasi ya Farid Musa na alitimiza vyema majukumu yake ambayo yalikuwa ni kuifanya timu iwe imara kwenye safu ya kiungo.

Feisal Salum-6

Alichukua nafasi ya John Bocco na ingawa muda ulikuwa umeshaenda, aliituliza timu kwa kupiga pasi na kumiliki mpira jambo lililopunguza presha ya Uganda iliyoonekana kuwa tishio dakika za mwisho.

Thomas Ulimwengu-3

Kuingia kwake kulilenga kupoteza muda ingawa hakuna kikubwa ambacho alikifanya kutokana na muda mdogo aliocheza.



Chanzo: mwananchi.co.tz