Klabu ya Yanga inakwenda kufanya uchaguzi baada ya mvutano wa wanachama, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Serikali kutokana na kujiuzulu kwa aliyekuwa mwenyekiti wa klabu, Yusuf Manji.
Sarakasi hizo zilihitimishwa kwa pande zote kukubaliana na kufungua upya mchakato wa kuchukua fomu na kurejesha baada ya ule wa awali kupingwa na wanachama baadhi wa Yanga.
Mchakato wa uchaguzi huo umefikia hatua ya wagombea walioenguliwa kukata rufaa kupinga kuenguliwa kwao.
Walioongeliwa kwenye usaili hawa hapa.
Wagombea 15, wakiwamo wanne waliokuwa wajumbe wa kamati ya utendaji kwenye uongozi uliopita walienguliwa ambao ni Samwel Lukumay, Thobias Lingalangala, Hussein Nyika na Siza Lymo ambao waliwekewa pingamizi kwa kutowasilisha ripoti ya mapato na matumizi kwenye uongozi uliopita.
Wengine ambao hawakupenya katika usaili ni Palina Conrad (aliwekewa pingamizi la kutokuwa na uzoefu), Seif Hassan Seif (hakuambatanisha nyaraka muhimu), Mkumbo, Elias Mkoma (hana uzoefu) na Said Rashid Omary (Ntimizi) ambaye hakuudhuria usaili.
Wengine ni Rodgers Gumbo (hana uzoefu wa kutosha), Abdallah Mussa Chikawe (hakuambatanisha nyaraka muhimu), Dk Nassoro Matuzya (amefungiwa na BMT),
Cyprian Musiba na Lucas Mashauri (hawakuhudhuria usaili), Seko Kingo (hana uzoefu wa kutosha na Ally Sultan Hemed ‘Chota’ hakuambatanisha nyaraka muhimu.
Hata hivyo, wagombea hao wanaruhusiwa kukata rufaa kupinga uamuzi huo, huku wale waliokuwa wamejitokeza awali wakiungana na wa sasa kwenye uchaguzi huo wa Mei 5.
Waliopitishwa hawa hapa
Kwenye nafasi ya mwenyekiti, wanaochuana ni Dk Mshindo Msolla na Elias Mwanjala ambao wanaungana na Dk Jonas Tiboroha, Mbaraka Igangula na Erick Ninga.Katika nafasi ya makamu mwenyekiti, wagombea ni Titus Osoro, Salum Chota, Yono Kevela, Pindu Luhoyo, Janeth Mbene na Fredrick Mwakalebela.
Yanga ambayo imekuwa katika kipindi cha mtikisiko wa uchumi kwa muda mrefu huku viongozi wake wa juu wakijiuzuru kwa nyakati tofauti inatazamiwa kuwa tofauti baada ya uchaguzi.
“Hakikuwa kipindi kizuri kwa Yanga, lakini kwa kuwa wanakwenda kwenye uchaguzi mambo yatakaa sawa,” anasema aliyewahi kuwa mchezaji, kocha na katibu mkuu wa klabu hiyo, Charles Boniface Mkwassa. Mkwasa anaamini baada ya uchaguzi, timu hiyo itapata uongozi mambo yatakuwa sawa.”
Nyota wa zamani wa timu hiyo, Ally Mayay anasema; baada ya uchaguzi, uongozi wa Yanga unapaswa kufanya utafiti kubaini Watanzania wangapi wako nyuma ya Yanga ukiachana na wanachama wa klabu.
“Kazi hiyo ikifanyika taasisi nyingine zinaweza kuvunjika moyo kwa kujiona ni ndogo kulinganisha na Yanga na Simba kwani thamani ya kitu ni watu,” anasema Mayay.
Mayay anaamini maendeleo hayawezi kutokea bila kuiga na sio dhambi kwa Yanga kufanya hivyo, kwani Simba leo ikijenga uwanja wake, wanachama watawashinikiza viongozi hata kwa kuandamana nao waboreshe uwanja au kujenga mwingine.
“Lazima Yanga ikubali kujiendesha kisasa, bahati nzuri katiba ya Yanga inatambua kujiendesha kama kampuni, hivyo waanze kuendesha klabu kisasa, iwe klabu ya mfano katika soka la Tanzania, inawezekana,” anasema.
Naye Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Kanali Iddi Kipingu anasema: “Kwa hali iliyofikia Yanga inahitaji mwenyekiti atakayekuwa ‘accountable’.
“Nadhani wanachama wanajua wanamtaka kiongozi wa aina gani, ila cha muhimu mtu atakayechaguliwa kuwa Mwenyekiti arudishe umoja ndani ya klabu, aendeleze dhana ya kujitegemea na awe na sifa ya utawala bora.”
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini, Yusuph Singo anasema Wana Yanga wanafahamiana hivyo ni wajibu wao kuchagua kiongozi atakayeleta maendeleo.” Serikali tunapenda kuiona Yanga imara, wanahitaji mtu wa kuivusha kutoka hapo ilipo, ni yupi wao ndiyo wataamua sababu wanafahamiana,” anasema Singo.
Nyota wa zamani wa timu hiyo, Abeid Mziba na mwanachama wa Yanga anasema: “ Yanga inahitaji kuanza na usajili.
“Huwezi kupigana vita kama huna jeshi, kwanza tuanze na usajili, wenzetu
Simba ukiachana na yote, walianza kusajili ndiyo sababu wanatamba kuwa na vikosi vya kucheza asubuhi na jioni. “Ukiangalia ni kweli, Simba inapambana wanacheza mpira, wanaonekana kweli wana nia ya mafanikio, lakini kwa sababu walitaka kufika huko,” anasema
Anasema klabu haipaswi kumuhudumia kiongozi, isipokuwa kiongozi ndiye aihudumie klabu.
“Yanga isifanywe kama sehemu ya kuchuma, ikifika usajili analetwa mchezaji ili mradi tu kiongozi amepiga pesa, kwenye uongozi ujao yakomeshwe, Yanga si timu ya kuchangishana, Yanga ni kubwa,” anasema.
Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage anasema: “Yanga wachague kiongozi mwenye sifa ya utawala bora na mwenye mipango ya kuiendesha klabu kisasa ili kufikia mafanikio ambayo wana Yanga wanayaota kwani hakuna Simba imara bila Yanga imara.”