Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hii hapa ‘kolabo’ ya Pluijm na Mwambusi Azam FC

Tue, 17 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kufanya kweli kwa Azam kwenye Kombe la Kagame kumechangiwa na benchi lao la ufundi lililoongozwa na Mholanzi, Hans van der Pluijm.

Azam imetetea taji lao la Kagame kwa kuifunga Simba mabao 2-1, matajiri hao wa Chamazi wamezifikia rekodi za Simba na Yanga kwa kutwaa kombe hilo mara mbili mfululizo.

Yanga ilitwaa Kombe la Kagame mara mbili kwenye miaka ya 2011 na 2012 huku kwa upande wa Simba ikiwa 1991 na 1992. A.F.C. Leopards ya Kenya iliwahi kufanya hivyo kutwaa mara tatu mfululizo, 1982, 1983 na 1984.

Nguvu ya benchi la ufundi la Azam ni kubwa, ukiachilia mbali uwepo wa Pluijm pia wapo, Idd Nassor Cheche na Juma Mwambusi ambaye aliwahi kuinoa Mbeya City.

Pluijm na Mwambusi hii ni mara yao ya pili kufanya kazi pamoja. Wawili hao walifanya kazi kwa maelewano mazuri na kwa mafanikio makubwa kwa misimu miwili Yanga, 2015-2016 na 2016-2017.

Ndani ya misimu hiyo, wakitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara mfululizo, Ngao za hisani mara mbili na Kombe la FA mara moja huku timu hiyo ikivunja rekodi yake iliyoiweka mwaka 1998 kwa kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Mfanikio hayo waliyapata kabla ya wote kuondoka kwa awamu tofauti kupisha benchi jipya la ufundi chini ya Mzambia, George Lwandamina ambaye naye tayari ameondoka.

Pluijm alikwenda Singida United baada ya kuondoka Yanga huku aliyekuwa msaidizi wake, Mwambusi aliamua kupumzika kwa kutojihusishwa na mchezo wa soka kwa muda kabla ya Azam kumnasa.

Akiwa na Singida United, Pluijm aliendelea kuonyesha ubora wake wa ufundishaji licha ya timu hiyo kuwa ngeni Ligi Kuu Tanzania Bara ilileta ushindani kwa Simba, Yanga na Azam.

Licha ya kuiongoza Singida United kumaliza kwenye nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa msimu huo, lakini pia aliiwezesha timu hiyo kucheza fainali ya Kombe la FA dhidi ya Mtibwa Sugar ambayo walipoteza kwa mabao 3-2.

Mara baada ya msimu wa 2017/18 kumalizika, Azam iliingia mkataba na Pluijm kuwa kocha wake mpya, akichukua nafasi ya Mromania, Aristica Cioaba aliyeondolewa baada ya matokeo mabaya msimu huo.

Pluijm alikuja Tanzania mwaka 2014 na kujiunga na Yanga SC alikofanya kazi kwa msimu mmoja kabla ya kwenda Al Shoalah FC ya Saudi Arabia na kurejea Jangwani mwaka 2015.

Mashabiki wanasubiri kuuona moto wa Azam msimu ujao chani ya kolabo hiyo.

Kagame Cup

Sasa ile kolabo yao inaonekana Azam. Endapo wachezaji watamwelewa Mholanzi huyo, Azam FC ijayo itakuwa moto.

Mchezo ulikuwa na ushindani wa aina yake lakini makosa ya ukabaji kwa upande wa Simba yaliifanya Azam kutangulia kwa bao la Shaaban Chilunda ambaye amejiunga na Tenerife ya Hispania.

Chilunda alitumia ujanja wa kuwatoroka mabeki wa Simba kwa kufunga bao la kichwa kwenye mpira wa kona iliyochongwa na Ramadhani Singano ‘Messi’.

Simba walitoka nyuma na kusawazisha bao hilo kwa kutumia udhaifu wa kujisahau kwa beki wa kati wa Azam, Nicolas Wadada ambaye alimsindikiza kwa macho , Meddie Kagere aliyefunga bao hilo la kusawazisha kirahisi kabisa.

Faulo ya Aggrey Morris iliwafanya Azam kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo, kipa wa Simba, Deogratius Munish ‘Dida’ hakuwa na hesabu nzuri za kucheza mpira uliokufa wa Morris baada ya kupanga ukuta wake nje ya eneo la hatari.

Kilichowaponza Simba

Simba ambao ni mabingwa wa Kihistoria katika michuano ya Kagame wameponzwa na kutowakaba wapinzani wao na kuwakabia macho.

Pascal Wawa na Paul Bukaba pengine walikuwa wazito kutoa mipira haraka kwa wenzao ili kusaidiana ukabaji wa kona na mipira iliyokuwa inapigwa kwenye eneo lao la hatari kutokea pembeni.

Bao la kwanza lililofungwa na Chilunda aliwaponyoka na kufunga kirahisi. Ule ni uzembe ambao umewaponza kwenye mchezo huo na kuruhusu bao la kwanza.

Hata hivyo, kocha wa kikosi hicho, Masoud Djuma alionekana kutofurahishwa na namna walivyokuwa wachezaji wake wakijipanga katika kona iliyowapa Azam bao la kuongoza.

“Umakini ulipotea wakati inapigwa kona ndiyo maana wenzetu walipata bao la kuongoza, tumefanyia sana kazi ukabaji wa aina ile ya mipira na kikawaida kwenye soka unapofanya kosa unakuwa kwenye nafasi ya kufungwa.

“Bao la pili tulilofungwa ni kosa ambalo linaweza kutokea kwa kipa yeyote huwezi kutoa lawama za moja kwa moja, lakini pamoja na yote niwapongeze wachezaji wangu kwa kazi kubwa ambayo wameifanya,” amesema kocha huyo.

Mbinu za Pluijm

Kocha wa Azam, Hans van der Pluijm ameendelea kuwa muumini wa mpira wa pasi fupi fupi za kasi huku akishambulia kupitia eneo la kati kati ya uwanja na pembeni kwa mawinga. Ramadhani Singano ambaye alikuwa hapati nafasi ya kucheza mara kwa mara ameibuliwa na kuanza kutumika kwenye mfumo wake huo.

Chanzo: mwananchi.co.tz