Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Haya ndio yaliyowabeba Wanafainali wa 2023

Yanga Kombe 2022 23 Mabingwa wa Ligi Kuu na ASFC Timu ya Yanga

Sun, 18 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Wikiendi iliyopita ilikuwa tamu kwa wapenda soka kutokana na kusheheni fainali pendwa hapa duniani ikiwamo ile ya Ligi ya Mabingwa Ulaya UEFA iliyochezwa Jumamosi na ile ya Ligi ya Mabingwa Afrika CAF iliyochezwa Jumapili.

Ilishuhudiwa Manchester City ikifikia rekodi ya Sir Alex Ferguson ya kutwaa makombe matatu katika msimu mmoja ikiwamo kutwaa Kombe la Ligi ya Mabingwa Ulaya UEFA baada ya kuichapa Inter Milan bao 1-0. Si hao tu hata hapa Bongo alimanusura klabu ya Yanga itwae makombe matatu lakini ikaambulia makombe mawili.

Wahenga walinena kuwa hakuna mafanikio bila juhudi na hakuna juhudi bila maarifa. Vile vile hakuna mafanikio yanayokuja kilaini, kuna kuumia kidogo.

Tumejifunza kuwa ili kufikia mafaniko yoyote ni muhimu kuwa na umoja, mshikamo, uongozi imara, maandalizi ya kiwango cha juu kabla na wakati wa mashindano.

Vituhivi vinaweza kupokewa vyema na kufanyika kwa usahihi kama tu mchezaji mwenyewe ana kipaji na huku akiwa mwenye nidhamu, juhudi na maarifa.

Taaluma ya sayansi ya michezo na nyinginezo ndizo zinawezesha kuwapata wachezaji wenye uwezo mkubwa kama wa timu ya Inter Milan na Manchester City. Wachezaji wale si tu wana viwango bali pia wanaowezo wa kufundishika na kufanya kila kinachotakiwa na walimu wao.

Timu zile hazikufika fainali tu kwa bahati bali ni ukamilifu wa idara zake zote ikiwamo benchi la ufundi, jopo la madaktari na walimu wa mazoezi ya viungo. Leo nitayadodosa mambo ya kimwili ambayo kwa namna moja ama nyingine yaliwabeba wanasoka wa kufika fainali mbalimbali.

Mambo hayo ndiyo yanayowafanya wapenda soka kutoshangaa Ilkay Gundogan kuwa mwanasoka wa kiwango cha juu na Erling Haaland kuwa mfungaji bora wa klabu Bingwa Ulaya UEFA 2023. Mchezaji kucheza kwa kiwango na kuifikisha timu fainali huwa ni utimamu wa afya ya mwili ambapo ndani yake huwa na vitu vitatu.

KASI

Wanasoka wote wanahitaji kuwa na kasi uwanjani, kadiri mchezaji anavyokuwa na kasi ndivyo pia anavyocheza vizuri. Ingawa kasi ya mpira wa miguu ni tofauti na michezo mingine. Mara kwa mara Mwanasoka anahitaji kukimbia na mpira, kukimbia kawaida au kufunguka kwa kasi yenye nguvu.

Mara nyingi kasi katika soka huitajika mahala pasipotarajiwa, mfano mchezaji anaweza kuwa anakimbia kidogo kidogo lakini anaponyakua mpira anaweza kufunguka kwa kasi ili aweze kushambulia. Vile vile mchezaji mkabaji atahitajika kufunguka ghafla kwa kasi ili kuweza kumzuia mshambuliaji ambaye si rahisi kukumkuta hana kasi.

Hivyo ni kawaida kumwona mchezaji wa soka mara kwa mara kukumbana na mbio fupi fupiza kasi ambazo zinahitaji atumie nguvu kubwa kuweza kufanya hivyo. Kasi ya mwanasoka inajengwa kwa mazoezi tangu akiwa kinda kama alivyo kwa Halaand, inahitajika kutunza uwezo wake wa kuwa na kasi kwa kuzingatia programu nzima ya mazoezi anayopewa na wakufunzi. Mazoezi ya kujenga kasi huwa na muda maalum, umbali maalum na mtindo wake.

UKAKAMAVU WA KIMWILI

Soka ni mchezo mgumu unaohitaji mwili mkakamavu ili kuweza kustahimili mikikimikiki yake na kucheza kwa ushindani katika mazingira magumu ya kimchezo. Unapokuwa na mwili mkakamavu ina maana ni mwili ambao unaweza kudumu na kuvumilia mambo mengi ikiwamo kutopata majeraha ya mara kwa mara.

Vile vile mchezaji mkakamavu huweza kudumu na mwili wake na kiwango chake kwa muda mrefu zaidi. Misuli ya mchezaji mkakamavu huwa imejengeka kimazoezi au kwa neno lilizoeleka sana ni neno stamina, neno hili si geni kwa wanamichezo.

Stamina ni uwezo aliojifunza mtu kutokana na mafunzo na kuzoeleka na kujengeka katika ubongo na mwili. Baadaye mwili ukaweza kujijenga na kufanya mambo kwa matendo yenye kuonyesha uwezo mkubwa wa kutenda na hivyo mtu ukautumia mara kwa mara kwa kiwango kinachotakiwa kwa muda mrefu.

Hivyo tunapata picha kuwa stamina ni mchanganyiko wa uwezo wa mwili pamoja na ukakamavu wake kuweza kudumu kwa muda mrefu bila kuchoka katika mazingira magumu ya mwili ikiwemo kucheza mechi nyingi kwa kiwango cha juu.

Misuli inapojengwa kwa mazoezi akili nayo inajifunza na hayo mazoezi na aina ya mafunzo ya mchezo husika. ili kuwa na stamina nzuri ni lazima kuwe na ushirikiano wa hali ya juu ya ubongo na viungo. Ukakamavu wa mwili huweza kujengwa kwa mazoezi mbalimbali ikiwamo yale ya viungo, ya gym kunyanyua vitu vizito, mazoezi ya uchezaji soka, mbio na kuogelea.

NGUVU

Kiungo mkabaji wa Manchester City, Rodri alionekana kuwepo kila mahali katika maeneo mengi uwanjani akikaba, kupokonya mpira, kutoa pasi na kushambulia. Kasi yake na kukimbia kila mahali bila kuchoka na kuwakaba wapinzani katika mechi zote alizocheza, bila kuwa na nguvu ni vigumu kucheza.

Utimamu wa Mwili wa mchezaji mwenye ukakamavu na kasi huitaji kuwa na misuli yenye nguvu ili kuweza kutekeleza majukumu kama yale ya Rodri. Nguvu ya mchezaji inajengwa kwa lishe maalum na mazoezi ya kuimarisha na kujenga misuli. Misuli inakunjuka na kujikunja kwa kutumia nishati tunayoipata katika vyakula.

Ndiyo maana mlo wa mwanamichezo huwa ni tofauti na ule wa mtu wa kawaida kwani mwanasoka anatumia nguvu nyingi sana anapocheza hivyo kuhitaji kula zaidi ili kupata nguvu. Mwanasoka hushauriwa kula vyakula vya kumpa nguvu na kujenga mwili (protini) pasipo kuathiri uzito wa mwili.

Lishe ndiyo inajenga mwili na kuupa mwili uzitowa wastani ambao unahitajika kuweza kukabiliana na mikiki ya soka. Ikumbukwe kuwa mchezo wa soka anahitaji uzito wa wastani kwani uzito mkubwa zaidi unasababisha kutokuwa na kasi au kuwa mvivu. Mara nyingi uzito wa wanasoka wakimataifa huwa ni kati ya kilo 65-80. Hivyo pamoja na kula vyakula mbalimbali mchezaji anahitaji kutunza uzito wake ili usipungue sana wala kuongezeka sana.

Ili kuweza kuwa na nguvu yenye ufanisi yenye kujenga mwili imara wenye afya wachezaji hupumzika na kulala muda mwingi kwa kawaida ni 6-8 kwa siku. Lengo ni kunatoa nafasi kwa mwili kujijenga, kujisahihisha, kuondoa uchovu na kupata utulivu wa kimwili na kiakili.

Mambo haya matatu huweza kuendeshwa vyema na akili na kipaji cha mchezaji binafsi hivyo kuweza kucheza kwa kiwango chakushangaza uwanjani na kufikia mafanikio.

CHUKUA HII

Pamoja klabu kuwa na benchi la ufundi inayosimamia programu za kuvijenga vitu hivi vitatu, zinahitajika juhudi za mchezaji binafsi kwa kujiongeza kwa kufanya mazoezi ya ziada na kula lishe maalum. Vile vile kuwa na mwenendo mzuri na kuishi mitindo mizuri ya kimaisha ikiwamo kutokula kiholela, kutotumia vilevi na tumbaku, kupumzika na kulala masaa 8 na kuwa na nidhamu ya mazoezi.

Chanzo: Mwanaspoti