Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hakuna namna, ni Simba kuiua AS Vita

47013 Pic+simba

Mon, 18 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Simba inataka kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na wako nyumbani, hakuna namna nyingine zaidi ya kuwakalisha AS Vita katika mchezo huo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa kuanzia saa 1:00 usiku.

Ni maneno manne unaweza kusema, hakuna namna, lazima wafungwe, na ndivyo ambavyo kila shabiki, mpenda soka anataka kuona Simba ikisonga mbele katika michuano hiyo.

Wakati Simba ikiwania ushindi, iko nafasi ya nne na pointi zake sita na ushindi wowote utaifanya ifikishe pointi tisa wakati AS Vita inabakia na pointi zake saba.

Endapo Simba itashinda, itaungana na timu itakayopata matokeo kati ya Al Ahly itakayokuwa nyumbani dhidi ya JS Saoura yenye pointi nane.

Matokeo yoyote kwa timu yoyote itaungana na Simba lakini endapo Simba itapoteza basi AS Vita itasonga na timu mojawapo kati ya Al Ahly au JS Saoura.Matokeo ya sare kwa timu zote, yataipotezea nafasi Simba kwa kuwa JS Saoura itakuwa na pointi tisa na sasa itaangaliwa kati ya Al Ahly na AS Vita nani mwenye wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa. Timu zote hizo zina pointi saba.

Hata hivyo, pamoja na hayo yote, kinachoangaliwa si kingine zaidi ya Simba kushinda mchezo huo.

KAULI YA KOCHA SIMBA

Kocha wa Simba Patrick Aussems alisema: “Bado tuna nafasi ya kusonga mbele kutokana na kundi lilivyo huku tukiwa na mchezo huu hapa nyumbani jambo ambalo si rahisi kwa timu yoyote kuifunga Simba hapa.

“Kwetu wala hatuna presha yoyote katika mchezo huu na tupo tayari kupokea matokeo yatakayopatikana ndani ya dakika 90 lakini wenzetu AS Vita watakuwa na presha kubwa kwani wao msimu uliopita walicheza fainali ya shirikisho,” alisema.

Beki wa Simba Erasto Nyoni alisema mechi itakuwa ngumu lakini wao wamejiandaa vizuri ili kufanikisha malengo yao ya kupata ushindi huku wakiamini wanakwenda kucheza na AS Vita ambao wana timu nzuri. “Tunaomba Mungu atutangulie kwani maandalizi ambayo tumefanya nina imani tutapata ushindi katika mchezo huu kama malengo ya kila mchezaji yalivyo,” alisema Nyoni ambaye alikuwa majeruhi kwa zaidi ya miezi miwili.

REKODI ZA SIMBA NA AS VITA

Ilianza kibarua Januari 12, akiwa ugenini dhidi ya Al Ahly na kufungwa mabao 2-0, baada ya hapo walirudi nyumbani DR Congo dhidi ya Simba Januari 19, na kushinda mabao 5-0.

Rekodi zinaonyesha pia AS Vita wamefungwa mechi zote mbili ugenini na jumla ya mabao yote ambayo wamefungwa katika hatua ya makundi ni matano wakati wao wakifunga mabao manane.

Rekodi za Simba ambao wao walianzia tangu hatua ya mwanzo ya mtoano kabla ya kufuzu hatua ya makundi wamefunga jumla ya mabao 16, na kufungwa idadi kama hiyo.

Katika mechi ya leo usiku Simba itawategemea wachezaji wake wanne Clatous Chama, Meddie Kagere, John Bocco na Emmanuel Okwi.

Rekodi zinaonyesha kuwa mabao 16, ambayo Simba wamefunga tangu hatau ya awali yamefungwa na Okwi mawili, Bocco matatu, Chama manne huku kinara akiwa ni Kagere ambaye mpaka sasa ameweka kambani mabao sita huku bao moja tu likifungwa na kiungo Jonas Mkude ambaye atakosekana katika mechi hii.

MSIKIE SALUM MADADI

Mkurugenzi wa ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Salum Madadi alisema anaamini mechi ya leo itakuwa mechi bora zaidi na Simba wanaweza kusonga mbele kwani una uhakika kabisa benchi la ufundi limeyafanyia kazi makosa yote waliyoyafanya katika mechi walizocheza ugenini.

“Imani yangu mechi hiyo Simba wanauwezo wa kusonga mbele kwani watakuwa wamewafatilia vya kutosha AS Vita kuona ubora na mapungufu yao ambayo yatawasaidia kupata ushindi katika mchezo huu ambao ni muhimu kwa kushinda na si matokeo mengine,” alisema Madadi.



Chanzo: mwananchi.co.tz