Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

HISIA ZANGU: Tuzitafakari dakika 64 za Ali Kiba dhidi ya Mbeya City

31155 PIC+ALIKIBA TanzaniaWeb

Wed, 12 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

DAKIKA 64 za Ali Kiba katika jezi ya Coastal Union dhidi ya Mbeya City katika Uwanja wa Mkwakwani juzi Jumapili zilitosha kuweka historia.

Ilifurahisha sana. Mwimbaji wa kwanza wa kulipwa kuwa mchezaji wa kwanza wa kulipwa nchini na inawezekana duniani kwa jumla.

Mwanasoka wa kulipwa ni yule ambaye amesaini mkataba na klabu na maisha yake yanategemea soka. Hii ni tafsiri fupi zaidi ya mwanasoka wa kulipwa kwa mujibu wa Fifa. Mwanasoka wa ridhaa ni yule ambaye anaweza kuuza madafu halafu akacheza soka kwa kujifurahisha. Kama mimi.

Dakika 64 za Kiba katika Ligi Kuu sikuziona lakini zimenifurahisha, zimefungua ukurasa mpya wa historia. Kwanza kabisa ni jinsi ambavyo Coastal Union imefanikiwa katika lengo lake kwa Kiba. Ilitaka aitangaze tu timu yao na kweli wamefanikiwa.

Mara tu ilipogundulika juzi Kiba angevaa jezi ya Coastal mitandao mingi iliandika kuhusu mechi hiyo. Naamini kuna mashabiki wengi walikwenda uwanjani kumtazama Kiba akicheza. Kwa hapo tu Coastal ilifanikiwa.

Lakini pia ilifanikiwa katika ukweli walitangaza jina. Sawa, Coastal ni timu kubwa na yalipita majina makubwa hapo zamani. Wale wa kizazi changu watawakumbuka kina Juma Mgunda (kocha wa sasa wa Kiba pale Coastal), Razak Yusuph ‘Careca’, Said Kolongo, Douglas Muhani, Kassa Mussa, Abdalah Tamimu, Idrissa Ngulungu na wengineo wengi ambao siwezi kuwataja hapa.

Hata hivyo, kwa Kiba kusajiliwa Coastal katika zama hizi ni wazi kwamba jina lilichangamka mitandaoni. Kwa Kiba kucheza juzi, jina lilichangamka zaidi mitandaoni. Hizi ni zama tofauti zaidi na zile za kina Careca. Hizi ni zama za biashara.

Pamoja na yote haya, mtu mmoja ninayemuamini aliniambia Kiba alicheza vema juzi. Hapa ndipo ninapojiuliza, Kiba anachezaje vyema katika pambano la Ligi Kuu?

Kwanza kabisa sina mashaka na kipaji cha Kiba. Kwa ambao hawajawahi kumuona wanaweza kudhani ni mchezaji wa kawaida sana lakini kwa ambao tumewahi kucheza naye vijiweni ni kweli Kiba ana kipaji.

Hata hivyo, nina sababu ya kuhoji. Kwanini Kiba acheze vema katika mechi yake ya kwanza ya ushindani ya Coastal Union? Inaacha maswali mengi nyuma yake. Kwanza ni kwa sababu wenzake wakati wapo bize na soka yeye alikuwa bize na kazi zake za muziki.

Hakufanya mazoezi ya kutosha kuweza kuwa fiti. Lakini pia hakucheza mechi za mazoezi za kutosha kuweza kuwa fiti. Kwanini acheze vizuri? Jibu ni moja tu kiwango cha ligi yetu kipo chini kiasi watu wengi wanatamani kurudi katika soka kwa sasa.

Lakini pia hata kiwango cha sasa kwa kiasi kikubwa kilimtamanisha Kiba atake kucheza Ligi Kuu. Kiba sio mwehu. Alipoamua kulazimisha kusaini Coastal kuna kitu alikuwa amekiona. Alijua anaweza kucheza.

Zamani kuna wachezaji wengi mahiri waliishia Ligi Daraja la Tatu. Hawakuweza kucheza Ligi Kuu na hata wenyewe walikuwa hawatamani sana kucheza Ligi Kuu kwa sababu viwango ambavyo kina Method Mogella, Dadi Athuman ama Ramadhani Lenny walikuwa wanaonyesha viliwakatisha tamaa. Leo wangeweza kucheza na kuchaguliwa timu ya taifa.

Mfano mdogo ambao tunaishi nao ni huu wa Mrisho Ngassa.

Alionekana amepotea. Alipoenda Mbeya City halafu Ndanda ilionekana kama vile amefika mwisho. Hata hivyo, baada ya kuondoka kwa Simon Msuva kwenda Morocco pale Yanga warithi wengine wa Msuva pale Yanga walimtamanisha yeye mwenyewe kisha wakawatamanisha mabosi wa Yanga Ngassa arudi kukipiga Yanga.

Hili ndilo tatizo la soka letu kwa sasa. Kiba asingetamani kucheza Ligi Kuu kama wale wachezaji aliokuwa anawaona utotoni wangekuwepo mpaka leo.

Lakini vile vile inawezekana hata yeye mwenyewe leo tungekuwa hatumzungumzii kama mwanamuziki kama soka letu lingekaa katika njia sahihi kwa muda mrefu.

Kwanini alitamani kuwa mwimbaji wa muziki wa kizazi kipya badala ya kuwa mwanasoka? Ni kwa sababu mpira wetu haulipi kuliko kazi yake. Haishangazi kuona tumepoteza wachezaji wengi mahiri ambao baadaye walikwenda katika fani mbalimbali kwa sababu kutafuta pesa zaidi.

Lakini hapo hapo kuna kitu cha kujifunza zaidi. Huu mchezo ambao wengi wetu tunauchukulia poa hatuutendei haki sana. Kwa jinsi ambavyo tunaouongoza ni wazi tumeurudisha chini ya kuruhusu watu wa fani nyingine watupite.

Katika timu kubwa kama Coastal iweje leo mashabiki wajaze uwanja kwa sababu ya Kiba? Unaamini Manchester United ikisema katika mechi yao ya kiushidani watampanga Usain Bolt mechi inaweza kujaa kwa sababu amepangwa Bolt? Mbona kila siku mechi zao zinajaza mashabiki?

Dakika 64 za Kiba dhidi ya Mbeya City inabidi tuzitafakari sana.

Kuna sehemu tumekosea. Hatujakosea kidogo, tumekosea sana. Kwa mwimbaji kumudu pambano la Ligi Kuu huku maisha yake mengi yakiwa katika fani yake basi kuna sehemu tumekosea. Tujitafakari.



Chanzo: mwananchi.co.tz