Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

HERITIER MAKAMBO: Bongo anapiga mabao, Congo anapiga pesa tu

40173 Pic+makambo HERITIER MAKAMBO: Bongo anapiga mabao, Congo anapiga pesa tu

Tue, 5 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

NDANI ya Jiji la Kinshasa nchini DR Congo, kama unatokea katikati ya jiji, basi fanya kama unaelekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa N’djili, lakini kabla ya kufika uwanjani hapo utakutana na sanamu kubwa la Hayati Patrice Emery Lumumba, ambaye amebeba historia nzima ya taifa hilo.

Wakati unashangaa sanamu hilo huku ukipewa historia fupi ya mnara wa Lumumba utakuwa umeingia eneo moja lililochangamka mithili ya pale Manzese jijini Dar es Salaam.

Eneo hilo ni maarufu kama kwa Masina karibu na kambi kuu ya Rais mpya wa DR Congo, Felix Tshisekedi.

Sasa ukifika eneo hilo kisha fanya kama unauliza jina la straika matata wa Yanga, Heritier Makambo basi fasta tu madereva wa Bodaboda watakugombania na kukufikisha kwenye mtaa mmoja mrefu ambako inapatikana nyumba ya mtambo huo wa mabao.

Mtaa huo ulionyooka vyema chini ukiwa na barabara yenye mchanga mwingi ndiyo makazi ya sasa ya Makambo, ambaye huko Bongo anafahamika kama mzee wa kupampu. Ndio, si unajua ile staili yake ya kushangilia kama anajaza upepo?

Mwanaspoti ambalo lilifunga safari hadi mtaani hapo na kupokewa na mdogo wa Makambo, Ezekiel ambaye alikuwa tayari anafahamu kuna ugeni kutoka Tanzania utatia timu nyumbani hapo.

Ezekiel ni nani?

“Mimi ni mdogo wa kwanza wa Makambo katika familia ya Mzee Ogoloa Makambo na Heritier ni kaka yetu mkubwa na hapa ndipo nyumbani kwake kwa sasa. Karibu sana,” anasema Ezekiel ambaye anaonekana kuwa na furaha kubwa.

Nyumba hiyo ambayo ipo ndani ya geti na ndani kuna nyumba nyingine ndogo ndogo (Apartments) ambazo ni kwa ajili ya biashara na zote zina wapangaji. Pia, ndani ya nyumba hiyo yenye eneo la kutosha, kuna nyumba kubwa ambayo ndiyo anaitumia Makambo akiwa kwao.

Ingawa Mwanaspoti lilishindwa kuingia ndani. Kiashiria cha kwanza ni kukutana na mdogo wake wa mwisho akiwa amevalia jezi ya Yanga ambapo, mara baada ya kujitambulisa alionekana kufurahia huku akiangalia jezi yake.

Mjengo wa Makambo

Ezekiel akiendelea na kufafanua baadhi ya maswali ya Mwanaspoti, kuwa nyumba hiyo na mali ya Makambo.

“Kaka ndiye anamiliki nyumba hii na aliinunua kwa mara ya kwanza wakati akiitumikia DC Motema Pembe na baadaye alipohamia Tanzania kuichezea Yanga, ndo alimalizia kila kitu.

“Kutokana na ukubwa wa nyumba hii akaona wenyewe hatutaweza kukaa kutokana na ukubwa hivyo, akapangisha ili iwe inaingiza pesa na sasa kuna wapangaji katika nyumba zote.

Wazazi wako mbali

Akizungumzia wazazi wao Ezekiel anasema: ‘Wazazi wetu hawakai hapa, huwa hawapendi vurugu za mji, hivyo wameamua kuishi nje kidogo ya mji wakiendelea na shughuli zao, lakini mara kwa mara tunakwenda kuwasalimia na wao huwa wanakuja.

anajenga mjengo mwingine

“Hii nyumba Makambo hatakaa sana, kwa sasa kuna nyingine kubwa anaijenga nje ya mji karibu na wazazi wanapokaa hiyo ndio ambayo atakuwa anaishi na familia yake. Kwa sasa ujenzi unaendelea,” anaeleza Ezekiel.

Maisha ya Makambo

mtaani

“Makambo akiwa hapa mtaani ni mtu anayejulikana sana katika eneo lote hili na hii limetokana na wakati anaichezea DCM (DC Motema Pembe) alikuwa akiifunga TP Mazembe tangu hapo amekuwa akipendwa.

“Akiwa nyumbani Makambo kila asubuhi hufanya mazoezi makali sana, unaona huu mtaa? Hii barabara inamsaidia sana, huamka alfajiri na kukimbia kwa saa moja na nusu, lakini jioni hubadili mazoezi.

“Jioni anahamia uwanjani kucheza mpira, lakini wakati mwingine anakwenda gym kufanya mazoezi mengine.

Ratiba ya jioni huwa ni tofauti kutokana kama unavyoona sasa watu ni wengi huwa anapata shida kufanya mazoezi kila mtu atakuwa akitaka kuongea naye ndiyo maana huwa anahama wakati wa jioni.

Anaizungumziaje Yanga Congo?

“Wakati anakuja Tanzania kwa mara ya kwanza hakuna aliyekuwa anajua kama atacheza huko, tulikuwa hatuijui Tanzania, lakini kupitia Samatta (Mbwana Samatta) na jinsi alivyokuwa anacheza hapa tukajua kwamba, huko kutakuwa na kazi kubwa kwake kufanikiwa.

“Aliporudi akatuambia amesajiliwa tulifurahi sana, lakini tulichofurahi ni pale aliposema mashabiki wa soka kule Tanzania wanapenda sana mpira na mashabiki wake wa Yanga ndiyo zaidi kila anapopita wanamuita tulifurahi sana,” anasimulia Ezekiel, ambaye ndiye mtu pekee kwao anayejua lugha ya Kiingreza kufuatia wengi kujua lugha ya lingala na kifaransa.

yuko peke yake kwao

“Katika familia yetu ni Makambo pekee anacheza soka labda na huyu mdogo wetu anayecheza sasa ngazi ya vijana, lakini mimi nilijaribu nikaona niache ili nijikite kwenye masomo, sasa nipo mwaka wa mwisho kumaliza masomo yangu ya udaktari.

Kidogo asisaini Yanga

Ezekiel anafichua kuwa wakati Makambo anasaini Yanga ilibaki kidogo zoezi hilo lisitishwe kama lisingefanyika haraka na sababu ilikuwa ni hii: “Kuna siku alinipigia simu akaniambia kesho anakwenda kusaini mkataba mpya.

Kweli siku ilipofika jioni akaniambia ameshasaini, lakini baada ya siku moja kuna wakala wa hapa Congo akaja nyumbani kumtafuta akitaka hati yake ya kusafiria ili amtafutie visa ya kwenda Ufaransa na Ubelgiji kwa majaribio.

Tulipomwambia jamaa yuko Tanzania na ameshasaini mkataba, yule wakala alikasirika akasema kule Ufaransa ni kama alishakubalika baada ya kuona video zake na kukubali anavyojua kufunga kwa kichwa

Msikie mpangaji wake

Mmoja wa wapangaji katika nyumba ya Makambo aitwaye Mama Tettee alisema: ‘Uamuzi wa kupanga hapa ni baada ya kuona jinsi Makambo kuwa maarufu katika eneo hili na kupendwa. Mtoto wangu humwelezi kitu kwa Makambo na akikua nitafurahi sana kama atafuata nyayo zake. Baba Tettee anataka mwanaye acheze mpira kama Makambo na tumemnunulia vifaa vyote.”

Makambo ndio kinara wa kufumania nyavu kwenye Ligi Kuu Bara akiwa amefunga mabao 11 akifuatwa na Said Dilunga mwenye mabao 10.



Chanzo: mwananchi.co.tz