Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

HATARI: Zilikuwa raundi tano za moto Bara

Yangasc.png?fit=717%2C416&ssl=1 HATARI: Zilikuwa raundi tano za moto Bara

Mon, 8 Nov 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

MBEYA. SIKU 37 za pilikapilika kuwania pointi tatu Ligi Kuu Bara msimu huu zilikamilika kibabe Novemba 3 kwa pambano la 40 lililozikutanisha Simba na Namungo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Katika mchezo huo uliokuwa na matukio kadhaa likiwamo la winga Mghana Bernard Morrison kuonekana akipiga mtu kiwiko, lakini akasalimika kulimwa kadi na mwamuzi Hassan Mwinchui ambaye kuna muda alikosa msaada wa wasaidizi wake.

Ligi imesimama kama wiki mbili ili kupisha maandalizi ya mechi za kimataifa kwa timu ya taifa, Taifa Stars, inayowania kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2022 zitakazofanyika Qatar. Wakati ligi hiyo ikienda mapumziko imeshuhudia soka tamu, lenye mvuto na ubabe katika mechi zote raundi tano za awali zilizopigwa hadi sasa, huku Yanga ikiwa kileleni na alama 15 ikifuatiwa na watetezi, Simba yenye pointi 11.

Katika mechi 40 kumekuwa na matukio yaliyobamba yenye kuumiza na kufurahisha, lakini kubwa ligi imekuwa na mvuto na ushindani mkali hasa kwa timu kupambana kufa na kupona ili kujiweka pazuri na kuepuka kushuka daraja.

Ikumbukwe kuwa msimu huu umekuwa tofauti na uliopita kutokana na kushirikisha timu 16 kutoka 18, ambapo timu mbili za mwisho zitashuka daraja, ilhali zile za nafasi ya 13 na 14 zikicheza mchujo.

Mwanaspoti linakuletea matukio kadhaa yaliyobamba mechi tano za kila timu ikiwa ni ndani na nje ya uwanja yanayofurahisha na kuumiza.

Related Kadi nyekundu zaibua mjadala Ligi Kuu Bara Maajabu mechi tano za Ligi Kuu Bara



Mayele: Kufunga ni akili, mabeki ni wagumu


CV ya kocha mpya Simba hii hapa....

Maajabu ya Mbeya Kwanza

Moja ya vitu vilivyoshangaza wengi ni matokeo ya sare mfululizo kwa Mbeya Kwanza iliyopata katika michezo minne kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya. Ukiachana na ishu ya matokeo, timu hiyo imekuwa ikitanguliwa kufungwa kipindi cha kwanza, huku wakirejesha mabao yote kipindi cha pili.

Timu hiyo ngeni Ligi Kuu, ilianza msimu kwa kuitungua Mtibwa Sugar bao 1-0 ugenini, kisha kuanza sare dhidi ya Mbeya City ikisawazisha mabao mawili dakika za mwisho. Mbeya Kwanza walirudia tena dhidi ya Dodoma Jiji wakisawazisha bao dakika za mwisho, kisha kufanya hivyo na Biashara Utd na zaidi wakashangaza kwa Polisi Tanzania sare ya 2-2.

MBILI zatimua makocha

Ikiwa ni msimu wake wa kwanza Ligi Kuu, Geita Gold iliweka rekodi kwa kumtimua kazi kocha wake mkuu, Etienne Ndayiragije kwa kutoridhishwa na matokeo.

Ndayiragije kabla ya kutimuliwa alikuwa ameiongoza katika michezo minne akipoteza miwili na sare mbili - matokeo ambayo hayakuwafurahisha mabosi wake.

Mbali na Geita Gold, Simba nao walifikia makubaliano na aliyekuwa kocha mkuu, Didier Gomes baada ya mchezo dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana wa Ligi ya Mabingwa Afrika walipolala 3-1 na kutolewa. Kabla ya kuondoshwa kocha huyo alikuwa ameiongoza Simba msimu huu katika mechi mbili za Ligi Kuu akishinda dhidi ya Dodoma Jiji na sare kwa Biashara United.

Fei, Ngushi noma

Hadi inakamilika michezo mitano kwa kila timu, yalishuhudiwa mabao kadhaa mazuri yakifungwa lakini miongoni mwa yaliyokuwa gumzo ni ya nyota wa Yanga, Feisal Salum na kinda wa Mbeya Kwanza, Crispin Ngushi.

Mabao yao yamekuwa gumzo yakitajwa kuweza kuwa bao bora la msimu kutokana na ufundi uliotumika kufunga.

Ngushi alifunga bao kali akiisawazishia timu yake dhidi ya Mbeya City, akiruka ‘tikitaka’ na kuukwamisha mpira wavuni akiwaacha mashabiki wameshika kichwa.

Kwa upande wa Feisal alifunga dhidi ya Ruvu Shooting akipokea mpira kifuani kisha kukunjuka shuti kali nje ya eneo la hatari lililogonga kidogo mwamba kama linatoka nje na kujaa wavuni. Bao hilo lilikuwa la tatu kwa nyota huyo wa kimataifa akiungana na Ngushi wakimfukuzia kinara mwenye mabao manne, Vitalis Mayanga wa Polisi Tanzania.

Kadi nyekundu zatawala

Huenda msimu huu kadi nyekundu zimeanza mapema kuwa nyingi kulinganisha na uliopita katika michezo mitano ya mwanzoni.

Hadi sasa kadi nyekundu nane zimetolewa. Wachezaji walioonyeshwa kadi hizo ni Anuari Jabir aliyekuwa wa kwanza wakati akiisaidia timu yake ya Dodoma Jiji dhidi ya Simba ambapo Wekundu walishinda bao 1-0.

Kisha akafuata Ismail Gambo wa KMC aliyelimwa kwenye mechi dhidi ya Coastal Union, Japhet Majagi (Mbeya Kwanza) dhidi ya Dodoma Jiji na Juma Ramadhan wa Polisi Tanzania walipovaana na Simba jijini Dar.

Wengine ni Jacob Benedicto wa Coastal Union dhidi ya Simba ambao pia ulishuhudia beki Hennock Inonga ‘Varane’ wa Simba akizawadiwa kadihiyo, Santos Mazengo (Ruvu Shooting) aliipata dhidi ya Yanga kisha aliyefunga hesabu ni Abdulaziz Makame wa Namungo dhidi ya Simba na kuiponza timu yake kulala 1-0 kwa bao la jioni.

Msala atibua Yanga

Pamoja na kwamba Yanga haijapoteza mchezo wowote, lakini straika wa Ruvu Shooting, Shaaban Msala alivunja mwiko kuwa mchezaji wa kwanza kumtungua kipa Djigui Diarra.

Licha ya kwamba Ruvu Shooting ilipoteza mchezo huo mbele ya Yanga kwa mabao 3-1, lakini Msala alimtibulia Diarra kwa kumfunga bao baada ya kucheza mechi nne bila kuruhusu wavu kuguswa. Hata hivyo, Yanga imekuwa na rekodi tamu na ya kipekee kwa kuwa timu mojawapo ambayo haijapoteza wala kupata sare katika michezo mitano na ipo kileleni.

Biashara, Prisons acha tu

Tanzania Prisons ilikuwa ya kwanza kufungwa idadi kubwa ya mabao -matatu dhidi ya Biashara United ambayo yaliweka rekodi.

Hadi raundi ya tatu hakuna timu iliyokuwa imefungwa au kufunga zaidi ya mabao mawili, ambapo Prisons ikiwa kwa mara ya kwanza nyumbani Sumbawanga iliambulia kichapo.

Matokeo hayo ya kikatili yaliwachanganya Wajelajela na kuwafanya kuwa mkiani kwa pointi moja, huku Biashara wakijiweka pazuri.

Nne kuti kavu

Wakati ligi ikisimama kwa muda, timu za Mtibwa Sugar, Geita Gold, KMC na Tanzania Prisons zimejikuta katika wakati mgumu kwa kushika nafasi za mkiani.

Katika michezo mitano timu hizo zimekusanya pointi mbili kila moja, huku zikiwa zimeruhusu mabao mengi kuliko timu nyingine.

Mtibwa Sugar wameruhusu mabao manne, Geita Gold ikifungwa matano, huku KMC na Prisons kila moja ikiruhusu wavu kutikiswa mara sita.

Wazawa 33 noma

Katika mechi 40 za raundi tano za awali, wazawa wameonekana kukikimbiza kwa kufunga mabao msimu huu na hata kuongoza msimamo wa wafungaji wakiongozwa na Vitalis Mayanga wa Polisi Tanzania akiwa na mabao manne, huku Feisal wa Yanga na Ngushi wa Mbeya Kwanza wanafuata na mabao matatu kila mmoja.

Wazawa 33 wamefunga mabao 43, huku nyota wa kigeni wakiongozwa na Fiston Mayele na Jesus Moloko wa Yanga sambamba na Meddie Kagere wa Simba wakiwa kila mmoja ametupia mawili.

Rekodi zinaonyesha nyota wa kigeni 11 wametupia kambani mabao 14. Mfungaji Bora wa msimu uliopita, John Bocco hadi sasa hajafunga bao lolote, kwani penalti iliyopata timu yake katika mechi ya kwanza dhidi ya Biashara United aliyoipiga ilipanguliwa na kipa James Ssetuba.

Penalti za kumwaga

Katika mechi 40 za awali zimeshuhudiwa penalti tisa zikipigwa, huku nne zikitinga nyavuni na tano zikipotezwa ikiwamo ile ya kwanza kabisa msimu huu iliyopewa Simba dhidi ya Biashara United. Penalti hiyo ilipotezwa na John Bocco, ila ile ya pili kwa Simba dhidi ya Polisi ilizamishwa na Rally Bwalya.

Timu nyingine zilizopata penalti na kupata ni Yanga dhidi ya Ruvu Shooting ilifungwa na Djuma Shaban, Namungo dhidi ya KMC na kukwamishwa wavuni na Shiza Kichuya na Khamis Mcha wa Dodoma Jiji aliyefunga dhidi ya Tanzania Prisons.

Penalti zilizokoswa ukiondoa ya Bocco ni ile ya Eliud Ambokile wa Mbeya City dhidi ya Mbeya Kwanza, Raymond Masota wa Geita Gold dhidi ya Mtibwa Sugar ambao nao walikosa siku hiyohiyo kupitia Boban Zirintusa na nyingine ilipotezwa na Lusajo Mwaikenda wa Azam walipovaana na Geita.

Bao la kujifunga

Mchezaji mmoja tu alimejifunga katika harakati za kuokoa hatari langoni mwake ambaye ni Yahya Mbegu wa Polisi Tanzania dhidi ya Mbeya Kwanza mechi iliyoisha kwa sare ya 2-2, huku kukiwa hakuna hat trick hata moja katika mechi tano za mwanzo timu zote.

Kwa mujibu wa takwimu hadi sasa timu yenye nidhamu mbovu ni Polisi Tanzania yenye j kadi moja nyekundu na 14 za njano ikifuatiwa na KMC ambayo ina kadi moja nyekundu na 12 za njano na inayofunga tatu bora kwa nidhamu mbovu ni Mbeya City yenye kadi 10 za njano.

Yanga ndio vinara wa timu zenye nidhamu nzuri ikiwa na kadi mbili za njano ikifuatiwa na watani zao, Simba yenye kadi moja nyekundu na nne za njano na Geita inafuatia kwa kadi tano za njano.

Wachezaji - Abdulaziz Makame wa Namungo akiwa kinara kwa utovu wa nidhamu akiwa na kadi nyekundu moja na tatu za njano. Wenye kadi za njano wengine ni Sospeter Bajana (Azam), Kelvin Yondani (Polisi Tanzania), Salum Salum (Biashara) na Salmin Hoza (Dodoma Jiji) wakiwa pia na kadi tatu za njano kama Makame.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz