Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gomes kupangua mabeki

4d1165e0ffea38e942a747feef736f43.jpeg Gomes kupangua mabeki

Fri, 21 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KOCHA Mkuu wa Simba, Didier Gomes amesema anaendelea kuyafanyia kazi mapungufu ya kikosi chake hasa safu ya ulinzi iliyoruhusu idadi kubwa ya mabao manne katika mchezo wa kwanza wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Kaizer Chiefs nchini Afrika Kusini.

Aidha, amesema wataishangaza dunia katika mechi ya marudiano kesho na kuwataka mashabiki watarajie mabadiliko kadhaa kwenye kikosi cha kwanza kwa vile anataka ushindi.

Simba iliruhusu mabao 4-0 ugenini Afrika Kusini, kati ya mabao hayo, mawili yalifungwa kwa mipira ya krosi, huku mengine yakisababishwa na mashambulizi ya kushtukiza na ukosefu wa umakini wa mabeki katika kuokoa mipira iliyorudi.

Akizungumza na HabariLEO jana, Gomes alisema walicheza vizuri katika mchezo wa kwanza, lakini ukosefu wa umakini walipopata nafasi na kuwapa nafasi wapinzani ya kuwashambulia ilikuwa moja ya sababu wakafanya makosa mengi.

“Tulicheza vizuri tulimiliki mpira kwa asilimia kubwa, tulitengeneza nafasi chache za kufunga ambazo hatukuzitumia, tayari tumelifanyia kazi suala hili sina wasiwasi na kikosi changu naamini tunaenda kushinda mchezo huu.”

“Najua kuna watu wamekata tamaa baada ya matokeo yale, nataka niwaambie hizi ni dakika 90 za jasho na damu zitakazo kuwa na maajabu, wachezaji wangu wamejiandaa katika hilo tunaenda kuishangaza Afrika na dunia.”

“Makosa yetu yalituhukumu naamini uwepo wa mashabiki utaenda kuongeza morali zaidi, najua tuna deni lakini tunaenda kulilipa kwa kufuzu hatua ya nusu fainali ambayo ndio malengo yetu ya msimu huu.”

“Ingawa tupo nyuma kwa idadi kubwa ya mabao, lakini hilo haliwezi kutuzuia sisi kutinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo ndio malengo yetu tunapaswa kuyatimiza,” alisema Gomes.

Alisema kikosi chake kiko kamili kuelekea mchezo huo, hakuna mchezaji mwenye majeraha wote wako fiti, lakioni mashabiki watarajie kuona mabadiliko kadhaa katika kikosi cha kwanza kwani dhamira yake ni kuona timu yake inasonga hatua inayofuata.

Chanzo: www.habarileo.co.tz