Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gomes haongezi wapya, haachi wazawa

Ce9190eb86a45b6de753e021da7857b8.jpeg Gomes haongezi wapya, haachi wazawa

Fri, 4 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAKATI dirisha la usajili kwa msimu wa mwaka 2021/2022 likitarajiwa kufunguliwa hivi karibuni kwa timu za Ligi Kuu, daraja la kwanza na la pili Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes amesisitiza hafikirii kuongeza sura nyingi mpya kwakua waliopo wanatosha kuifanya timu hiyo kuwa bora.

Simba ambao ndio mabingwa watetezi wa taji la Ligi Kuu na Kombe la FA, ndio timu bora kwa misimu mitatu iliyopita na imekuwa na utaratibu wa kuongeza wachezaji wachache kwenye usajili wao ili kuziba nafasi zenye mapungufu.

Akizungumza na gazeti hili Gomes alisema mpango wake ni kuongeza wachezaji wawili tu kutoka nje ya Tanzania katika nafasi ya mlinzi wa kati na ushambuliaji ili kuimarisha maeneo hayo ambayo kwa kiasi fulani amebaini kuwa yamekosa ubora anaoutaka.

“Hatuna mapungufu makubwa sana mpango wangu ni kufanya usajili makini ambao utaziba makosa yaliyotugharimu msimu huu kwenye michuano ya kimataifa ndio maana nataka kuongeza nyota wawili wenye uzoefu wa kutosha na mashindano hayo,” alisema Gomes.

Kocha huyo raia wa Ufaransa alisema ndani ya kikosi cha sasa anawachezaji wake 17, ambao hana mpango wa kuachana nao kutokana na kuridhishwa na uwezo wao labda wenyewe watake kuondoka jambo ambalo anaamini siyo rahisi kutokana na huduma nzuri.

Gomes alisema kwamba anaamini endapo atafanikiwa kupata wachezaji hao wawili kwenye kikosi chake, Simba itatisha msimu ujao katika mashindano ya ndani na nje na mikakati yake yeye na uongozi wa timu hiyo ni kutwaa ubingwa wa Afrika.

Alisema kwamba anafikiria kununua wachezaji hao kutoka popote pale lakini bado hajapata machaguo ya mwisho kwavile anapambania kwanza ubingwa kuhakikisha Simba inautetea na kubeba pia taji la FA.

Wachezaji kumi wa kigeni waliopo Simba sasa wanaocheza na ligi ya ndani ni Joash Onyango, Pascal Wawa, Taddeo Lwanga, Luis Miquissone, Clatous Chama, Larry Bwalya, Bernard Morrison, Chriss Mugalu, Meddie Kagere na Parfect Chikwende.

Tayari kiungo wa Kenya Francis Kahata ameshamalizana na timu hiyo baada ya timu hiyo kutolewa kwenye michuano ya kimataifa.

Gomes alisema hana mpango wa kumtema mchezaji yeyote mzawa sababu kwa utafiti wake alioufanya tangu atue nchini anaona viwango walivyokuwa navyo ni bora kuliko wale wa timu nyingine ambazo ni washindani wao kwenye ligi.

Chanzo: www.habarileo.co.tz