Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gomes aeleza jeuri ushindi Kaizer Chiefs

Simbaa.jpeg Gomes aeleza jeuri ushindi Kaizer Chiefs

Tue, 11 May 2021 Chanzo: ippmedia.com

Simba ambayo ni timu pekee kutoka Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati iliyosalia kwenye michuano hiyo, Jumamosi majira ya saa 1:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki itashuka katika Uwanja wa FNB jijini Johannesburg, Afrika Kusini, kuwavaa wenyeji wao, Kaizer Chiefs katika robo fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa.

Kwa mujibu wa uongozi wa klabu hiyo, mabingwa hao wa Tanzania walitarajia kuondoka leo alfajiri kuelekea Kenya wakiwa na kikosi cha wachezaji 27, huku msafara mzima ukitarajiwa kuwa na watu 40.

“Kikosi cha mabingwa wa nchi kitaondoka alfajiri ya Jumanne Mei 11, 2021 (saa 9:45) kuelekea Afrika Kusini kupitia Kenya tayari kwa mchezo wa kwanza wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Kaizer Chiefs utakaopigwa Jumamosi,” ilieleza taarifa ya klabu hiyo.

Aidha, akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes, alisema anatarajia kuwapo kwa ushindani mkubwa katika mchezo huo, lakini anaamini wachezaji wake watafanya vizuri na kupata matokeo chanya.

Alisema analifahamu vema soka la Afrika Kusini na uzoefu huo anao, hivyo anaamini utamsaidia kuendelea kuandaa kikosi chake kwa ajili ya kwenda kutafuta matokeo chanya ili kuweza kusonga mbele katika michuano hiyo.

"Nilipenda kukutana na Yanga kabla ya kucheza mchezo wa robo fainali dhidi ya Kaizer Chiefs, ili kuongeza utimamu wa wachezaji, lakini hilo limeshindikana na tunaendelea na maandalizi yetu kwenda kukabiliana na wapinzani wetu hao kufanya vizuri ugenini na kuja kutafuta ushindi nyumbani," alisema Gomes.

Alisema kutokana na uzoefu wa kulifahamu soka la nchi hiyo, ana matarajio makubwa kwa namna alivyokiandaa kikosi chake watahakikisha wanaenda kupambana kutafuta matokeo chanya katika mchezo huo wa ugenini.

"Malengo yetu ni kusonga mbele katika kila hatua, baada ya kufanikiwa kufika robo fainali, sasa tunatakiwa kupambana kupata matokeo mazuri ili kushinda mechi zote mbili ugenini na nyumbani kuweza kucheza nusu fainali ya michuano hii," alisema kocha huyo.

Baada ya mechi hiyo, timu hizo zitarudiana Jumamosi ya Mei 22, mwaka huu, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam na timu itakayopata matokeo ya jumla, itatinga nusu fainali ambapo itakutana na mshindi wa jumla kati ya Wydad Casablanca ya Morocco ama MC Alger ya Nigeria.

Chanzo: ippmedia.com