Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gomes: Tumepata dawa ya Yanga

Gomez Pic Data Gomes: Tumepata dawa ya Yanga

Mon, 5 Jul 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

NDIO Yanga wameshinda, lakini dawa imeshapatikana na subirini muone kitakachotokea kule Kigoma, ndio kauli ya kocha wa Simba, Didier Gomes akizungumzia mipango ya Wekundu wa Msimbazi katika mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC) itakayopigwa Julai 25.

Kocha huyo Mfaransa amesema wamegundua walichokosea katika mechi yao iliyopita waliyolala 1-0 dhidi ya Yanga juzi, na tayari wanajipanga kwa ajili ya mechi ijayo.

Kuhusu kupoteza mechi ya juzi, alisema si kama wachezaji wake waliingia kwa kujiamini kupita kiasi, lakini mechi iliisha nje ya matarajio yao.

Alisema walikuwa na malengo mawili, kuwafunga Yanga na kutangaza ubingwa mbele ya mashabiki wao ambao walikuwa wengi uwanjani hapo, lakini baada ya kushindwa kutimiza hilo anatumia nafasi hii kuwaomba msamaha.

“Nipo tayari kuwajibika katika hili kwa nafasi yangu ya ukocha, kwani si jambo zuri kupoteza mechi kubwa ya namna hii ambayo ndani yake ilikuwa na rekodi nyingi bora kama tungepata ushindi.

“Kipindi cha kwanza tulicheza kwa kiwango cha chini jambo ambalo hata upande wangu ilinishangaza licha ya kutenga muda mwingi kuiangalia Yanga namna walivyocheza mechi zao za mwanzo.

“Yanga ni moja ya timu nzuri baada ya kuwaangalia kupitia luninga niliwapa kazi ya kufanya wachezaji wangu ili kuwazidi lakini kipindi cha kwanza tulishindwa kufanya hivyo, ingawa kipindi cha pili tulibadilika na kucheza vizuri kama ambavyo nilikuwa nahitaji kutoka kwao.

“Jambo jingine tulipata nafasi za kufunga wachezaji wangu walishindwa kuzitumia vizuri na kuwafanya wachezaji wa timu pinzani kuendelea kujiamini.” alisema Gomes.

Katika hatua nyingine Gomes alisema kupoteza mechi hiyo siyo mwisho wa maisha yao wanaingia kambini kwa ajili ya maandalizi ya kutosha dhidi ya mchezo wa KMC.

“Tutaweka nguvu kwa ajili ya mechi ya KMC, ili kupata ushindi pamoja na michezo mingine mitatu iliyo mbele yetu dhidi ya Coastal Union, Azam na Namungo ili kuchukua ubingwa kama malengo yetu yalivyo,” alisema Gomes.

WALIKOSEA HAPA

Aliyewahi kuwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Azam, Saad Kawemba alisema kilichoipa ushindi Yanga ni kuingia uwanjani na kuwaonyesha Simba kwamba wanaweza kupata ushindi mbele yao.

“Simba waliingia wakajiona kama mabingwa na wakawa wanacheza kwa kujiamini, Yanga waliingia kama wachezaji ambao wanaenda kupambana na hilo likaonekana ndani ya uwanja.

“Simba upande wa kushoto walikuwa hawashambulii kabisa, alipotoka Kisinda (Tuisila) ndio wakaanza kucheza, Yanga walicheza na plani ya Simba, pia kucheza na viungo wakabaji wawili iliwayumbisha Simba, alipoingia Bwalya (Larry) walianza kusogea,” alisema Kawemba na kuongeza

“Simba bado wana nafasi ya kubadilika, Yanga wamejua mfumo wa Simba wakaufanyia kazi.”

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz