Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gharama za Dreamliner zaibua mjadala

20936 Pic+dreamliner TanzaniaWeb

Sat, 6 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikitangaza gharama za safari ya timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ kwenda Cape Verde ni Dola1500 (Sh3.4 milioni) na Dola2000 (Sh4.6 milioni), wadau wameibuka na kudai fedha hizo ni nyingi kwa Mtanzania wa kawaida kumudu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, wadau hao walisema gharama hizo ni kubwa kulinganisha na hali ya kiuchumi ilivyo na wametoa rai kwa Serikali kuangalia upya gharama ya usafiri.

Hata hivyo, Serikali imesema inaangalia namna ya kupunguza gharama hizo kwa kuanzisha mazungumzo na Shirika la Ndege ATCL ambao ni wamiliki wa ndege ya Boeing 787-8 Dreamliner.

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo Tanzania, Yusuf Singo, alisema juhudi za kuishawishi ATCL kupunguza gharama hizo zinafanyika ili kupata idadi kubwa ya mashabiki kwenda kuishangalia Taifa Stars.

“Kama unavyojua ndege inamilikiwa na ATCL na gharama waliyoweka ni ndogo kuliko nyingine kwa sababu safari ya kwenda Cape Verde ni ndefu ina njia nyingi. Ndege itakaa huko kwa siku mbili, lakini juhudi zinaendelea kufanyika ili kuona kama wamiliki watapunguza gharama,”alisema Singo.

Mchezaji wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua alisema Serikali imefanya uamuzi wa busara wa kuisafirisha timu kwa ndege yake, lakini gharama kwa mashabiki inaweza kuwa kikwazo.

“Ni jambo jema Serikali kufanya hivyo kwa kuwa itawasaidia wachezaji kutochoka na watakwenda kupambana vizuri katika mchezo huo, ukiangalia muda baina ya mechi hizo mbili ni mfupi.

“Pamoja na Serikali kuwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi, sidhani kama watamudu gharama ya ndege kwa sababu ni kubwa. Sijui gharama ya uendeshaji wa ndege hizo lakini Serikali inaweza kufikiria kupunguza gharama ya usafiri ili kutoa fursa kwa mashabiki kwenda kwa wingi,” alisema Chambua.

Naye mshambuliaji wa zamani wa Simba, Innocent Haule alisema Serikali inatakiwa kupunguza gharama ya usafiri kwa mashabiki ili Taifa Stars ipate idadi kubwa ya Watanzania watakaokwenda kuiunga mkono ugenini.

“Najua kila mmoja ana uwezo wake, lakini kwa maoni yangu gharama ni kubwa sidhani kama wengi wataimudu, Serikali inabidi kuangalia hilo ili mashabiki waende wengi kwa sababu shabiki ni mchezaji wa 12 uwanjani,”alisema Haule.

Mchambuzi Ally Mayay alitoa wito kwa kampuni mbalimbali kununua tiketi za ndege na kuzitoa kama motisha kwa mashabiki ili kupata idadi kubwa ya mashabiki kwa kuwa gharama ni kubwa.

“Mpaka jana (juzi) watu walioonyesha nia ya kwenda Cape Verde hawazidi hata 10 na ukizingatia ugumu na umuhimu wa mechi hiyo angalau hata wakipatikana mashabiki 150 kwenda kuiunga mkono timu ingekuwa jambo zuri,” alisema nahodha huyo wa zamani wa Yanga.

Kwa upande wake kocha Mrage Kabange alisema muda uliobaki ni mfupi kwa mashabiki wa kawaida kumudu gharama hiyo, hivyo ameitaka Serikali kutafakari.

Boeing 787-8 Dreamliner ina uwezo wa kubeba hadi abiria 262 ikiwa pia na uwezo wa kusafiri umbali wa kilomita 13,621 bila kusimama kujaza mafuta au kupumzisha injini.

Taifa Stars inatarajiwa kuondoka Oktoba 9 au 10 kwenda kuivaa Cape Verde, mchezo utakaochezwa mjini Praia, Oktoba 12 kabla ya kurudiana jijini Oktoba 16.

Taifa Stars inayonolewa na kocha Mnigeria Emmanuel Amunike, inashika nafasi ya tatu katika Kundi L na inapaswa kushinda mchezo huo ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kukata tiketi ya kucheza fainali hizo.

Timu hiyo ina pointi mbili katika msimamo wa Kundi L ilizopata baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Lesotho kabla ya kulazimisha suluhu na Uganda ‘The Cranes’ mjini Kampala.

Chanzo: mwananchi.co.tz