Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gharama za Basi la Azam zinaweza kufanya mambo haya matano

Basi Pic Data Fedha za Basi la Azam zingefanya haya

Mon, 8 Nov 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

BASI aina ya Mercedes Irizar ambalo Azam FC imelinunua nchini Afrika Kusini na sasa inalitumia katika safari zake ndilo habari ya mjini katika medani ya soka nchini.

Thamani kubwa ya basi hilo pamoja na muundo wake wa kifahari ndio umelifanya kuwa gumzo kwa wadau wa mpira wa miguu.

Uongozi wa Azam FC licha ya kukiri kuwa wamenunua basi hilo kwa kiasi kikubwa cha fedha, umeshindwa kuanika kiwango halisi ambacho umetoa katika kuligharamia basi hilo hadi lilipofika nchini na kuanza kutumika.

“Ni basi la gharama kubwa sana ya fedha ambayo siwezi kukutajia, lakini fahamu ni kubwa mno na kwa hapa Afrika ni timu chache sana ambazo zinamiliki mabasi ya aina hiyo,” alisema mtendaji mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin ‘Popat’.

Hata hivyoj taarifa za uhakika ambazo Mwanaspoti linazo ni kwamba basi hilo limeigharimu Azam FC takriban Sh900 milioni na ushee pasipo kujumuisha gharama za kulisafirisha ardhini kutoka Afrika Kusini hadi Tanzania.

Kiasi hicho cha fedha si kidogo na kingeweza kufanya mambo mengi katika mchezo wa soka na gazeti hili linakuletea baadhi ya vitu ambavyo vingepatikana au kufanyika kutokana na kiasi hicho cha pesa ambacho kimetumika kulinunua.

UJENZI UWANJA WA MECHI

Gwambina FC wana uwanja wao unaoingiza takribani mashabiki 10,000 na pia ukiwa na eneo la maegesho ya magari. Uwanja huo hadi ulipoanza kutumika unakadiriwa umegharimu kiasi cha takribani Sh1 bilioni.

Hii inamaanisha kwa fedha iliyotumika kununulia basi, Azam wangeweza kujenga uwanja unaoingiza idadi ndogo ya mashabiki kuliko ule wa Gwambina ingawa tayari wanao uwanja wao wa bora na wa kisasa wa Azam Complex ambao wanautumia kwa mechi na mazoezi.

USAJILI KISINDA, MOLOKO

Kiasi cha takribani Dola 200,000 ndio kinatajwa kutumiwa na RS Berkane ya Morocco kumsajili winga wa Yanga, Tuisila Kisinda.

Sehemu ya fedha hizo ndizo zilizotumika na Yanga kumsajili winga Jesus Moloko kutoka AS Vita Club.

Kwa fedha ambayo Azam imetumia kununulia basi lake, ingeweza kuwasajili wachezaji hao wote wawili na chenji ingebaki.

VIWANJA VITATU VYA KISASA VYA MAZOEZI

Uwanja wa kisasa wa mazoezi wenye nyasi za asili unagharimu kiasi cha kuanzia Sh200 hadi 300 milioni kama ilivyo ule wa Simba kule Bunju au wa Boko Veterans ambavyo vipo wilayani Kinondoni.

Bahati nzuri kwa Azam FC tayari wana miliki Uwanja wa kisasa wa mazoezi ambao ni wa nyasi asili lakini fedha hiyo waliyotumia kununulia basi, ingetosha kutengeneza viwanja vitatu vya hadhi ya juu kwa ajili ya kufanyia mazoezi ambavyo vina nyasi asili.

UDHAMINI TIMU TISA

Idadi kubwa ya timu zinazoshiriki Ligi Kuu Bara hazina wadhamini na zinategemea fedha za mgawo wa wadhamini wa ligi.

Fedha hizo zilizotumika kununua basi la Azam FC zingeweza kugawanywa kwa timu tisa za Ligi Kuu na kila moja ikapata mgawo wa Sh100 milioni ambazo zinaweza kuzisaidia kujiendesha msimu mzima.

Kwa hali ya ukata iliyopo kwa timu nyingi za Ligi Kuu, ni chache sana ambazo zinahitaji zaidi ya Sh100 milioni za udhamini binafsi ili kusaidia kujiendesha.

MABASI YA TIMU 5

Basi zuri la timu linaloweza kubeba abiria takribani 45, linakadiriwa kuuzwa kati ya Sh 150 hadi 200 milioni.

Kwa maana hiyo, fedha zilizotumika kununulia Irizar hiyo zingesaidia timu tano au nne kupata mabasi ya kutembelea.

Ofisa Habari wa timu hiyo, Thabit Zakaria ‘Zaka Zakazi’ alisema basi hilo limedhihirisha ukubwa wa nembo ya timu hiyo. “Hii ni klabu kubwa na lazima ifanye mambo makubwa. Hili ni basi la kisasa na lenye hadhi ya juu na ujio wake nchini unaendelea kudhihirisha ni kwa jinsi gani Azam FC imejitofautisha na klabu nyingine za hapa,” alisema

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz