Mwanariadha wa kimataifa na bingwa wa mbio ndefu nchini, Gabriel Geay ametoa msaada wa vifaa vya michezo vyeenye thamani ya Sh450,000 katika Shule ya Sekondari Ilboru iliyopo jijini Arusha.
Vifaa hivyo ni mipira mitatu ikiwa miwili ni ya kikapu na mmoja wa soka pamoja na nyavu ambapo zinalenga kuhamasisha michezo katika shule hiyo.
Akizungumza na Mwanaspoti baada ya kukabidhi vifaa hivyo, Geay amesema huu ni mwanzo katika harakati zake za kurudisha fadhila kwenye jamii kwa kile anachopata na pia kusaidia michezo kwa vijana waliopo shuleni.
“Nina imani kupitia hili itawapa fursa na nafasi ya kila mmoja kutambua kipaji chake kikubwa shule zote nchini zizingatie muda wa michezo ili kutoa nafasi kwa vijana kutimiza ndoto zao,” amesema Geay.
Makamu Mkuu wa shule hiyo, Salvatory Mrutu amempongeza mwanariadha huyo kwa sapoti yake kubwa ambayo anaendelea kutoa kwa wanafunzi wake kupitia vifaa vya michezo.
“Kipindi kilichopita ulitoa vifaa vya michezo na leo tena umetuongezea vingine, sisi tunashukuru kwa kile unachorudisha kwa jamii. Hii itatoa nafasi kwa vijana wangu kushiriki vyema katika michezo,” amesema Mrutu.
Abednego Elias, kwa niaba wa wanafunzi wenzake ameahidi kuvitumia ipasavyo vifaa hivyo na kuongeza kuwa kama michezo inavyosapoti taaluma, basi watahakikisha wanaendelea kufanya vizuri kotekote kwa maana ya viwanjani na darasani.
Ikumbukwe kwamba Geay ni miongoni mwa wanariadha wanne wa mbio ndefu za kilomita 42 kutoka Tanzania ambao tayari wamefuzu kushiriki Olimpiki itakayofanyika Paris, Ufaransa mwezi Julai, mwaka huu.
Mwanariadha huyo alifuzu kushiriki Olimpiki kupitia mbio za Valencia Marathon nchini Hispania zilizofanyika Desemba 3,2023 ambapo alimaliza wa tano akitumia saa 2:04:33 - kigezo kikiwa ni saaa 2:08:10 kwa wanaume na 2:26:50 kwa wanawake.
Nyota huo pia anajiandaa kushiriki mbio za Boston Marathon zitakazofanyika Aprili 15 nchini Marekani akiwa na kumbukumbu nzuri ya kumaliza wa pili mwaka jana, akizidiwa na mkongwe ambaye amekuwa akishikilia rekodi mbalimbali za dunia katika riadha, Eliud Kipchoge kutoka Kenya.