Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

GSM yaleta utamu Yanga

78973 Yanga+pic

Tue, 8 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

ACHANA na mjadala kuhusu lile bao lao kama mpira ulivuka mstari ama la, ila Yanga imeendelea kuokoa pointi kwenye Ligi Kuu Bara na kujichomoa eneo la mkiani baada ya jana Jumapili kupata ushindi wake wa kwanza mbele ya Coastal Union.

Yanga ikicheza mechi yake ya tatu katika ligi ya msimu huu iliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililowekwa kimiani dakika ya 51 na kiungo Abdulaziz Makame lililozua utata licha ya mwamuzi Abubakar Mturo kutoka Lindi na msaidizi wake Credo Mbuya kutoka Mbeya kulikubali huku Coastal wakililalamikia wakidhani mpira haukuvuka mstari.

Bao hilo lilitokana na mpira wa kona ulioleta kizaaza langoni baada ya ya Makame aliusukumia wavuni mpira uliopigwa na Ali Ali na kutolewa kwa kichwa na beki wa Wagosi, Omar Salum aliyeonekana kuwa ndani ya goli kabla ya kudunda nje ya mstari, lakini tayari filimbi ilishalia kwamba ni bao.

Licha ya ushindi huo, lakini Yanga huenda inashukuru kuvuna alama hizo kwa jinsi wapinzani wao walivyowabana kwa muda mrefu na kuwapa shughuli mabeki wa kati Ali Ali na Kelvin Yondani kufanya kazi ya ziada kuokoa sambamba na kipa Farouk Shikhalo aliyeanza langoni.

Kabla ya mchezo huo, matajiri wa GSM waliamua kuwajaza upepo nyota wa Yanga kwa kutinga uwanjani na Sh 10 milioni wakiahidi wakishinda wanaondoka na mzigo wote huo, jambo lililotimizwa baada ya dakika 90 kumalizika.

Ushindi huo umeifanya Yanga kuchupa kutoka nafasi ya 19 hadi ya 13 ikifikisha alama nne na mabao manne, pia ikifungwa manne ikiporomosha Coastal Union iliyokuwa nafasi ya 12 hadi 14 wakitofautiana kwa mabao ya kufunga na kufunga.

Pia Soma

Advertisement
Katika mchezo huo ambao Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera hakuonekana uwanjani bila kueleweka sababu nini, licha ya kwamba kwa sasa anatumikia adhabu ya kukaa jukwaa katika mechi tatu kwa kosa la utovu wa nidhamu Wagosi walitawala.

Wakicheza soka la kuvutia na kasi, wakitawala eneo la kiungo ambalo nyota wa Yanga, Feisal Salum na Makame walionekana kukosa mawasilianao na kugongana, Coastal watajilaumu kwa kushindwa kutoka na ushindi ugenini.

Katika mchezo huo David Molinga ‘Falcao’ ambaye alikuwa shujaa kwenye mechi iliyopita baada ya kutupia mabao mawili dhidi ya Polisi Tanzania, jana alidhibitiwa vilivyo na mabeki wa Coastal na kushindwa kuonyesha makeke licha ya kufunga bao kipindi cha pili akiwa ameotea.

Baada ya dakika 45 kumalizika kwa suluhu na kipindi cha pili kuanza kwa mabadiliko kadhaa kwa timu zote ndipo ikatokea kona na kusababisha bao hilo pekee la Yanga ambalo lilizua mjadala kwa baadhi ya mashabiki uwanjani na pia wachezaji wa Coastal.

Hata hivyo, baadhi ya wadau akiwamo kocha wa zamani wa Yanga, Charles Mkwasa ambaye aliwahi kuichezea klabu hiyo, alisema yupo njia panda kuzungumzia bao la Makame kutokana na kuwa kwake uwanjani.

“Aina ile ya bao inahitaji marejeo ya usaidizi wa picha ya video. Sikuwa kwenye eneo zuri kiasi cha kusema halikuwa bao sahihi, nadhani waamuzi walifanya kazi yao kwa sababu mbali na yule aliyechezesha kati, kulikuwa na msaidizi wake pembeni.”

Naye kiungo wa zamani wa Yanga, Ally Yusuph ‘Tigana’ alisema ule mpira uliingia ndani, hivyo hakuna utata kwenye lile bao, waamuzi walikuwa makini ndio maana ilikuwa rahisi kwao kufanya maamuzi.

“Ushindi kwa Yanga una maana kubwa kwani wachezaji wataongeza kujiamini. Na kwangu sikuona tatizo juu ya lile bao, maadamu waamuzi walilikubali,” alisema.

Chanzo: mwananchi.co.tz