Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

GEAY: Nini Boston Marathon! Ni zamu ya Olimpiki

Gabriel Geay Bosto Marathon Mwanariadha wa kimataifa wa Tanzania, Gabriel Geay

Sat, 18 May 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Umepita mwezi mmoja tangu kufanyika kwa mashindano makubwa ya dunia ya mbio za Boston Marathon nchini Marekani, ambapo mwanariadha wa kimataifa wa Tanzania, Gabriel Geay alikuwa ni miongoni mwa nyota ambao walipewa nafasi kubwa ya kushinda.

Hata hivyo, Geay ambaye alifanya vizuri mara mbili katika mbio hizo akimaliza wa nne mwaka 2022 kwa muda wa saa 2:07:53, wa pili 2023 saa 2:06:04, lakini mwaka huu joto lilizidi na kujikuta akishindwa kumaliza mbio.

Kushindwa kumaliza kwa bingwa huyo wa marathoni nchini kulitoa nafasi kwa Sisay Lemma wa Ethiopia ambaye mwaka jana alishindwa kumaliza mbio hizo, mwaka huu aliziweka katika mikono yake.

Sisay (34) katika mbio hizo zilizofanyika Aprili 15 aliwatimulia vumbi wenzake akikimbia mwanzo mwisho kwa muda mrefu peke yake na kumaliza wa kwanza kwa saa 2:06:17 akifuatiwa na Muethiopia mwenzake Mohamed Esa 2:06:58.

Mshindi mara mbili mfululizo wa mbio hizo 2022 na 2023, Evans Chebet kutoka Kenya alishindwa kutetea ubingwa na kujikuta akimaliza wa tatu kwa saa 2:07:22.

Mwanadada Hellen Obiri kutoka Kenya aliongoza upande wa wanawake na kuweka rekodi ya kuwa mwanamke wa kwanza kushinda mbio hizo mara mbili mfululizo. Ushindi huo ulimfanya Obiri kushinda mbio ndefu za kilomita 42 mara tatu kati ya nne alizoshiriki akiwa miongoni mwa wanawake wanaotazamiwa kufanya vyema Olimpiki zitakazofanyika Paris, Ufaransa, Julai, mwaka huu.

Mshindi huyo wa medali ya fedha ya Olimpiki mara mbili katika mbio za mita 5000 licha ya kwamba alipata upinzani mkali kutoka kwa Mkenya mwenzake Sharon Lokedi, lakini alimaliza wa kwanza akitumia saa 2:22:37.

Baada ya kupita mwezi mmoja tangu mbio hizo kufanyika, Mwanaspoti limefanya mahojiano na Geay ambaye anaweka wazi sababu ilimfanya kufanya vibaya.

SIKUJIVUNJA, AKOSA MAMILIONI

Geay anaweka wazi kwamba hakujivunja katika Boston Marathon kama baadhi ya Watanzania wanavyodhani, bali alishindwa kumaliza kutokana na majeraha ya nyonga ambayo yalikuwa yanamsumbua.

“Nilipata majeraha ya nyonga ambayo yalinifanya nishindwe kufanya vizuri hivyo Watanzania watambue niliumia kwani hata mimi nilitamani kushinda ila ndo ikawa hivyo,” anasema Geay.

Anasema kufanya vibaya katika mbio hizo kulisababisha akose pesa nyingi kutoka kwa mdhamini wake, kampuni ya Adidas, ambapo kwa mujibu wa mkataba kuna fedha hupata akishika nafasi tatu za juu.

“Pesa nalipwa kulingana na mkataba wa malipo, ila ya kufanya vizuri ni kuanzia mshindi wa kwanza wa pili na wa tatu,” anasema.

Geay anasema kiasi alichokosa baada ya kushindwa kushika nafasi ya kwanza ni Dola 60,000 (takriban Sh 154.8 milioni, ya pili Dola 30,000 (zaidi ya Sh77.5 milioni) na ile ya tatu angepata Dola 20,000 (takriban Sh51.7 milioni).

NJE MWEZI MMOJA

Mwanariadha huyo anasema kwa mujibu wa madaktari alitakuwa kukaa nje kwa mwezi mmoja na wiki mbili ambapo anatarajia kuanza kufanya maandalizi kwa ajili ya mashindano ambayo yapo mbele yake mwezi huu mwishoni.

“Hili jeraha la nyonga lilinifanya nisifanye maandalizi mazuri kuelekea Boston, lakini kwa sasa maendeleo si mabaya, naendelea kusubiri kwa kwa mujibu wa vipimo vya madaktari ambavyo nilifanya baada ya kutoka Boston."

Geay anasema anaamini ni mkimbiaji bora licha ya jeraha kumfanya ashindwe kufurukuta katika mbio za Boston, ambapo anaweka wazi ujasiri alionao siku zote ndio unamfanya kuwa alivyo.

Nyota huyo ambaye anashikilia rekodi ya ubingwa wa marathoni ya taifa kwa muda wa 2:03:00 akiwa na mbio mbili pekee, tayari alitoka kuwa mkimbiaji anayechipukia hadi kuwa nyota ambaye anajiandaa kwa mafanikio makubwa zaidi.

MIKAKATI YA OLIMPIKI

Wakati dunia ikitarajiwa kuhamishia macho na masikio katika Olimpiki jijini Paris, mwezi Julai, Geay anasema kuwa nguvu zote ataelekeza huko na ana matarajio makubwa ya kushinda.

Ndoto kubwa ni kushinda Olimpiki na kuwa Mtanzania wa tatu kufanya hivyo. Itakumbukwa mwaka 1980 jijini Moscow, Urusi, Suleiman Nyambui alishika nafasi ya pili katika mbio za mita 5000 na kupata medali ya fedha sawa na Filbert Bayi katika mbio za mita 3000.

“Sijawahi kushinda moja ya medali ya dunia ya marathoni au hata kupata medali ya ubingwa na kama kila mwanariadha ndoto yangu ni kushinda medali ya Olmpiki. Wakati mwingine unaweza kuhisi labda ni kama bahati nasibu, lakini hilo ndilo lengo langu kuu yaani kupata medali," anasema.

Anasema maandalizi ya Olimpiki yataanza mwishoni mwa mwezi huu kwani baada ya kutoka Boston Marathon kulingana na hali ilivyokuwa alijipa mapumziko samamba na matakwa ya madaktari.

“Nategemea mazoezi ya Olmpiki kufanya mwezi mmoja kuanzia sasa. Nimejipa mapumziko kwa mwezi na wiki mbili, kwa lengo ni kumpuzisha mwili ili nikianza maandalizi yawe mazuri.”

URAFIKI NA KIPTUM

Geay anagusia urafiki aliokuwa nao na mshindi wa rekodi ya dunia ya mbio za marathoni kwa wanaume, Mkenya Kelvin Kiptum aliyefariki dunia katika ajali ya barabarani Februari, mwaka huu, nchini mwake.

Mwaka 2023 Kiptum alidhihirisha kuwa mpinzani wa Eliud Kipchoge, mmoja wa wanariadha ambao wanafanya vizuri katika mbio za barabarani baada ya kumaliza wa kwanza katika mbio za Chicago.

Alimaliza umbali wa maili 26.1 (42km) kwa saa 2:00:35 na kuweka rekodi mpya ya dunia huku akifuta muda wa awali wa saa 2:01:09 uliokuwa unashikiliwa na Kipchoge.

Geay ambaye mara kwa mara hufanya mazoezi katika kambi ya Iten nchini Kenya anasema Kiptum alikuwa mshikaji wake kwelikweli.

“Alikuwa mshikaji wangu. Nakumbuka mbio za Valencia ilikuwa maalumu kwa ajili yetu. Tulisafairi pamoja hadi Valencia tukatumia muda mwingi kabla na baada ya mbio na kiwango changu kilikuwa kinamvutia,” anasema.

“Ndio alikuwa anaanza ubora wake kulikuwa na mengi makubwa ambayo angefanya katika riadha.”

Chanzo: Mwanaspoti