Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fei Toto kawa mtamu zaidi, wengine mjipange tu

Fei Pic Data Fei Toto kawa mtamu zaidi, wengine mjipange tu

Wed, 23 Jun 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

KWA mara ya kwanza katika maisha yake ya soka la Ligi Kuu, Feisal Salum ‘Fei Toto’ (23), Alhamisi iliyopita alifunga mabao mawili katika mechi moja tena yote akiyatupia kiufundi kabisa akitumia mguu wa kushoto, ambao si mguu wake bora zaidi.

Yanga ilishinda mechi hiyo kwa mabao 3-2 dhidi ya Ruvu Shooting huku Fei akiibuka nyota wa mchezo baada ya kuupiga mpira mwingi siku hiyo.

“Nimekuwa nikifanyia mazoezi ufungaji wa kutumia mguu wa kushoto kwa muda sasa na naona matunda yameanza kuonekana,” alisema Fei alipozungumza na Mwanaspoti kuhusu mabao hayo ambayo yaliwapagawisha mashabiki.

Umaliziaji mzuri wa kiufundi kama unaofanywa na mastraika wa kiwango cha juu siku hiyo, ulionekana kumchanganya hadi kocha Nasreddine Nabi ambaye aliamua kumuanzisha Fei kama straika wa pili nyuma ya Fiston Abdoulrazaq katika mechi iliyofuata juzi dhidi ya timu iliyoshuka daraja ya Mwadui.

Hata hivyo, mabadiliko mengi ya kiufundi ikiwamo kuwaacha nje wachezaji wenye mchango mkubwa zaidi kwenye matokeo ya timu hiyo msimu huu, Yacouba Sogne na Tuisila Kisinda, nusura yamtokee puani kocha Nabi, ambaye katika hali ya kushangaza alimuanzisha beki wa kulia Kibwana Shomary katika nafasi ya beki ya kushoto na kuwa uchochoro wa Mwadui, ambao mashambulizi yao ya hatari yote waliyapitishia kwake Kibwana.

Kocha Nabi alipojistukia kuwa anaizamisha Yanga kwa mikono yake mwenyewe, akawaingiza Tuisila, Yacouba na Wazir Junior, ambao waliifichia aibu timu hiyo iliyokuwa imetanguliwa 2-1 na Mwadui hadi kufikia dakika ya 90, kabla ya watatu hao kushirikiana na kufunga mabao mawili ndani ya dakika mbili za majeruhi na kuipa Yanga ushindi wa usiku wa mabao 3-2.

Related HISIA ZANGU: Bado simshikii dhamana Kibu, tusubiri na tuone MZEE WA UPUPU: Dk Msolla na wenzako mnawajibika ishu ya MetachaFei anasema matokeo yao ya uwanjani yanatokana na kujituma kwa timu na pia mchezaji mmoja mmoja.

“Ningekuwa sipambani sidhani kama makocha wangekuwa wananitumia kwenye vikosi vyao vya kwanza, pia ninaocheza nao ndio wanaonifanya niwe bora na nisibweteke, huwa nafanya maandalizi ya makubwa, la sivyo nisingekuwa fiti,” anasema.

ANAVYOIONA LIGI KUU

Anasema msimu huu ligi ina ushindani mkali, unaomfanya mchezaji asibweteke, aongeze juhudi kwenye majukumu ya kuisaidia klabu yake na anakiri hiyo imemkomaza kiufundi.

“Ligi ikiwa ngumu inakufanya mchezaji uwe mbunifu wa kujua ni jinsi gani utaisadia timu kufanikisha malengo ya mechi na msimu kwa ujumla, ukitaka kuamini ugumu upo wapi Yanga tulianza kuongoza ligi, Simba imepambana imefanikiwa kuongoza, kilichobakia ni kinyang’anyiro cha ubingwa nani atatwaa taji hilo,” anasema.

Staa huyo kutoka Zanzibar pia anazungumzia ushindani wa namba kwenye kikosi chao kwamba ni mgumu na kwamba kujituma na kutoridhika ndio silaha ya kusaka mafanikio ya maisha yake ya soka.

“Nimetoka nyumbani kuja kufanya kazi Yanga, siwezi kubweteka, natambua soka ni kazi itayoendesha maisha yangu, la sivyo ningeendelea na shule kuikamilisha ndoto yangu ya pili ya kusomea mambo ya fedha na kuwa mhasibu.

“Nilichapwa sana na mama kuhusu shule, maana nilipenda sana mpira kiasi kwamba nilikuwa nafanya utoro, ndio maana nasema siwezi kubweteka kufanya kazi yangu hata kama napata nafasi kikosi cha kwanza na mpira upo kwenye damu,” anasema.

MAANA YA FEI TOTO

Anamtaja bibi yake Faida, mzaa mama yake kwamba ndiye aliyempatia jina la Fei Toto, akisema lilitokana na unene wa mwili wake akiwa mdogo hivyo alimuita jina hilo.

“Fei Toto sijapewa na wanasoka bali ni bibi yangu, wakati nikiwa mtoto nilikuwa kibonge hivyo bibi akaona ndilo linalonifaa, alimaanisha mtoto kibonge,” anasema.

Fei Toto ambaye ni mtoto wa kwanza kati ya wanne waliozaliwa kwenye familia yao, anasema jina hilo lilipata umarufu kutokana na vijana wenzake kuvutiwa na kipaji chake cha mpira.

MAISHA YAKE YANGA

Anasimulia maisha yake ndani ya Yanga, tangu alipojiunga msimu wa 2018/19 akitokea JKU ya Zanzibar, kwamba yamemfanya awe na mtazamo tofauti kuhusi kuheshimu kipaji chake cha soka na kujua jinsi ya kukiendeleza.

“Kama unavyojua Yanga ni klabu kubwa, ina wachezaji wenye ushindani wa juu, mitazamo tofauti, hilo limenifunza kujijua mimi ni nani na natakiwa kufanya nini ili kipaji changu kinifikishe mbali zaidi;

“Yanga imenikomaza kiushindani, Fei Toto yule wa mwaka 2018 sio huyo wa mwaka 2021 kuna vitu vimeongezeaka kwasababu napenda kujifunza kila siku na nimepitia mikononi mwa makocha tofauti na nimecheza na wachezaji tofauti.”

Kuhusu soka la kulipwa, anasema ikitokea dili atakubaliana nalo kwasababu ndio ndoto yake kubwa.

“Kama isingekuwa ugonjwa wa Covid -19, ambao ulitikisa dunia nzima huenda ningekuwa nacheza nje, sijakata tamaa, nina safari ndefu, ikitokea sitaichezea nafasi hiyo na umri wangu unaruhusu,” anasema.

UCHEZAJI WA MUDATHIR

Anasema tangu mdogo hadi sasa anavutiwa na uchezaji wa kiungo wa Azam FC, Mudathir Yahya na vitu anavyovipenda ni kucheza kwa kujiamini bila kutumia nguvu kubwa, umiliki wa mipira, anavyokaba wakati mwingine kuchezesha pamoja na nidhamu yake ya kazi.

“Mudathir ana kipaji cha hali ya juu, anaujua mpira, akicheza hatumii nguvu bali akili, mguu wake ni kipaji kinachofanya uone burudani ya soka, anavutia anavyocheza na hachuji,” anasema huku akimtaja staa wa zamani wa Barcelona, Andres Iniesta kuwa ndiye mtu aliyemvutia tangu akiwa mdogo kutokana na staili yake ya uchezaji iliyoufanya mchezo wa soka uonekana kama ni mchezo rahisi sana.

TUKIO LILILOMUUMIZA

Kama kuna kitu anajutia basi ni tukio alilolifanya mwaka 2019 alipojumuishwa Stars, kikosi kilichoshiriki Fainali za Afcon nchini Misri.

Anasema kitendo chake cha kuimba taarabu ndani yake akiwataja mashabiki waliokuwa wanamsema vibaya kucheza chini ya kiwango, ni kitu kilichomgharimu kwani alikutana na maneno mazito aliyoshindwa kuyabeba.

“Kiukweli maneno niliyokumbana nayo katika mitandao ya kijamii yaliniumiza mimi hadi wazazi wangu, siombei linitokee tena,” anasema.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz