Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fedha za Mo zina manukato ya Kibongo

77941 Mo+pic

Tue, 1 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Nilikuwa katika televisheni, wikiendi ya mwezi Agosti wakati Simba ikiwa na Wabrazili watatu benchi huku UD Songo ikiwa inakata tiketi kwenda hatua inayofuata ya Ligi ya Mabingwa Afrika kupitia mikono ya Simba. Walikuwa wanapita tundu ambalo Simba waliliona ni rahisi, hawakujipanga kuliziba. Waliona ufa lakini ukuta kwao ulionekana imara siku zote. Kuanzia Shiboub, Kagere mpaka Chama, wote wanakula mshahara wa Ligi ya Mabingwa Afrika, kipaumbele sio ligi Kuu Bara. Simba walihisi kazi imeisha, waliamini wao ndio wababe wa vita na waliamini kila walilofanya katika usajili lilikuwa sahihi.

Ukifuatilia kauli ya Kocha wa UD Songo, Chaquir Bemate alikiri walishaisoma Simba na waligundua safu ya ulinzi haikuwa imara.

Kwa tafsiri ya haraka walishasoma Simba hawakufanya kazi ya ziada kwenye nafasi iliyodharaulika kwa kipindi kirefu, nafasi ya James Kotei.

Samba hawakusoma hesabu hawakuchanganua mlinganyo na aljebra yao ilikuwa nyepesi kupangilia kusajili wachezaji wapya takribani 10.

Bao la Luis Miquissone lilikuwa linawarudisha Simba kwenye utimamu wa kawaida kuwa kila kitu kilikuwa kinahitaji sayansi, kila jambo lilitakiwa mahesabu na iliwabidi kuwa wapya kiutendaji tofauti na ujanja uliozoeleka miaka mingi.

Mwezi mmoja baadaye Simba inamtumia Deo Kanda vilivyo dhidi ya Kagera Sugar na wengi wanaamini lazima Simba itwae ubingwa wa Tanzania Bara.

Pia Soma

Advertisement
Ulazima ambao waliuweka kwenye mdomo wa Haji Manara kuhusiana na wao kuwa ‘nusu fainali material’ wa Klabu Bingwa Afrika.

Wakati sakafu ikishuhudia mbio zikigota ukingoni, naamini Simba watakuwa waliutumia wakati huu sahihi wa kuketi chini na kusoma kurasa za kitabu ambazo kwa makusudi waliziruka na kusoma vichwa vya habari tu kuhusiana na mafanikio ya soka. Najaribu kuwaza walishika kalamu na kuhakikisha wananakiri kila kosa lililoambatana na ‘usajili wa kutisha wa Patrick Aussems’. Kama waliamini kilichotokea dhidi ya UD Songo ni kipigo cha Anthony Joshua dhidi ya Andy Ruiz basi wanakosea kwasababu Simba haijawahi walau kuwa katika uzito wa uzani wa juu.

Simba inaongezeka uzito ngumi zake hazina ujazo kwa sasa, hawana kasi ya mikono ya kuwa na uhakika wa ngumi ya ‘knockout’ katika mashindano ya kimataifa. Tulishuhudia yote ya robo fainali kuanzia mabao dhidi ya Vita mpaka uhalisia dhidi ya TP Mazembe.

Simba inapanda ngazi na haihitaji kupaa wanahitaji muda wa maandalizi sahihi ili kuwa kwenye uhalisia wa mdomo na maneno ya mitandao ya Manara. Si jambo baya kuwa na ndoto lakini ni jambo jema kusimamia ndoto kwa kufanya jambo sahihi.

Jambo sahihi ni kutumia muda huu kujipanga zaidi kufanya ‘skauting’ inayoeleweka na kuhakikisha kuwa pengo la Emmanuel Okwi haliwi sababu ya washabiki kujiuliza wataishi vipi. Ule uwanja wa Bunju ukamilike ili Simba isiwe inakosa pa kufanya mazoezi pale ambapo Serikali ikiamua kufanya “JamaFestival” kwenye viwanja vyake. Shiboub aendelee kuwepo na baadhi ya wenzie na sio mabadiliko ya wachezaji kumi kwa dirisha moja la usajili ambayo inakuwa sio tafsiri sahihi ya watu wenye mipango.

Pamoja na Yanga kuwa wapinzani wakuu, amini kuwa walitamani kuwa Simba kwa wakati Fulani tofauti na sasa ambapo wanaamini kuwa wapo kwenye kikao kimoja cha kahawa za soka la Tanzania. Simba ilionekana kuwa inapiga simu za kimataifa na kuwa vikao vyao vingekuwa vya Tp Mazembe na Mamelodi Sundowns. Muda bado upo na bado kuna mengi yanawezekana nyuma ya fedha za Mo Dewji, fedha zinazonuka manukato ya soka la Bongo.

Fedha zinazoweza kumtesa Mbao FC, zikamnyima usingizi Coastal Union na zikapandisha timu ndege kuelekea ‘mapumzikoni’ Afrika Kusini. Fedha hizi inabidi zibadili manukato lazima zibadili mwondoko na lazima zilete taswira sahihi ya uwekezaji.

Umefika wakati ambao Simba lazima ifanane harufu na Esperance au isimike nguzo ambazo inaweza kuzitumia kuning’inia kwa kipindi kirefu kutoka sasa.

Nimekutana na kikosi hiki ghali jijini Mwanza kikiwa safarini kuelekea Musoma na nikakumbuka uhalisia huu.

Nikakumbuka kuwa wanaishi nje ya ndoto ambazo hazikuwekewa mkazo na mipango sahihi. Kwao hiki inabidi kiwe kitabu cha mafunzo, lazima kiwe kitabu wanachosoma na kama ningekiandika ningekipa jina linaloshabihiana na uhalisia wa Manukato Ya Kibongo kwenye fedha za Mo Dewji.

Chanzo: mwananchi.co.tz