INATIA huruma. Ukiwasikiliza masimulizi yao makocha waliofutwa kazi na klabu ya Simba juzi, utawahurumia, hasa Adel Zrane ambaye alilia hadi macho yakamvimba.
Iko hivi: Juzi Simba iliachana na kocha wake mkuu Didier Gomes da Rosa na kuwatupia virago wasaidizi wake kadhaa baada ya timu hiyo kutolewa na Jwaneng Galaxy katika raundi ya mwisho ya kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kutokana na kipigo cha 3-1 kwenye Uwanja wa Benjama Mkapa na Jwaneng kusonga mbele kwa faida ya kushinda mabao mengi ya ugenini (ilala 2-0 nyumbani Botswana), kocha Gomes ameiambia Mwanaspoti kuwa aliandika barua ya kuachana na Simba.
Katika mahojiano maalum na Mwanaspoti, kocha huyo Mfaransa alisema aliwasilisha barua ya kuachana na Simba kwa sababu hakutimiza malengo yaliyoainishwa kwenye mkataba wake na klabu hiyo.
Gomes alizungumzia pia tuhuma za wachezaji Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ na Pascal Wawa kucheza chini ya kiwango ni za kweli sababu walipoteza kujiamini na kwamba amefanya kikao kilichotumia muda wa saa mbili na Wawa ili kumrudishia kujiamini.
“Wawa alilia sana, alionekana kukosa amani,” alisema Gomes kuhusu kikao hicho na beki huyo.
Gomes alisema yeye ni sawa kuondoka Simba, lakini anaamini wasaidizi wake akiwamo Zrane wameonewa kwa kuingizwa katika mkumbo huo.
Zrane alishindwa kushiriki mahojiano haya na Mwanaspoti kwa sababu alikuwa akilia sana na akaomba kukaa pembeni.
Katika taarifa iliyotolewa mapema jana, klabu ya Simba iliandika: “Klabu ya Simba imeridhia ombi la aliyekuwa kocha mkuu, Didier Gomes da Rosa la kuachana na Simba kuanzia leo tarehe 26.10.2021. Baada ya tathmini na majadiliano ya kina, pande zote zimeafikiana kwa mujibu wa mkataba na manufaa ya wote.
“Aidha, Klabu imefanya mabadiliko madogo katika benchi la ufundi kwa kusitisha mikataba ya aliyekuwa kocha wa makipa, Milton Nienov na Kocha wa Viungo, Adel Zrane.”
Katika taarifa hiyo ya Simba, kwa sasa benchi la ufundi la timu hiyo litasimamiwa na Thierry Hitimana atakayesaidiana na Selemani Matola.
Miezi 10 ya heshima Simba
Gomes ametimuliwa Simba akiwa ndio kwanza ametimiza muda wa miezi 10 ya kuinoa klabu hiyo tangu alipojiunga nayo Januari 24 mwaka huu akichukua nafasi ya Sven Vandenbroeck aliyetimkia FAR Rabat ya Morocco
Katika kipindi hicho cha miezi 10 aliyoinoa Simba, Gomes amepata ushindi katika idadi kubwa ya michezo kuliko kupoteza au kutoka sare.
Kocha huyo ameiongoza Simba katika jumla ya michezo 38, amepata ushindi katika mechi 27, ametoka sare sita na kupoteza michezo mitano, Simba imefunga jumla ya mabao 68 na imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara 21.
Kati ya mechi 38 alizoiongoza Simba, 10 ni za Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo kati ya hizo imepata ushindi mara sita, kutoka sare moja na kupoteza mechi tatu, imefunga mabao 15 na kufungwa mabao tisa wakati mechi 21 ni za Ligi Kuu, ikipata ushindi mara 16, kutoka sare nne na kupoteza mechi moja tu huku ikifumania nyavu mara 42 na zake zkitikiswa mara tisa.
Mechi nne ni za Kombe la Shirikisho la Azam ambazo Simba ilishinda zote, ikifunga mabao saba na kufungwa bao moja, imecheza mechi moja ya Ngao na kupoteza kwa bao 1-0 na mechi nyingine mbili imecheza katika mashindano ya Simba Super Cup ikishinda moja na kutoka sare moja huku ikifunga mabao manne na kufungwa bao 1-0.
Kocha wa Mataji
Gomes ameipa mataji matatu ambayo ni Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na Simba Super Cup.
Hata hivyo, ameambulia patupu katika Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo msimu uliopita alitolewa na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini katika robo fainali na msimu huu ametolewa katika raundi ya kwanza na Galaxy na alikosa Ngao ya Jamii msimu huu baada ya kuchapwa na Yanga kwa bao 1-0.
Katika mechi tatu ambazo Gomes ameiongoza Simba dhidi ya Yanga, imepata ushindi mara moja tu huku ikipoteza mara mbili.