Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

ERASTO NYONI: Achomoa Azam kimizengwe, akomaliwa na Makonda

82120 Nyoni+pic ERASTO NYONI: Achomoa Azam kimizengwe, akomaliwa na Makonda

Tue, 29 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

KIRAKA fundi gwiji ni kati ya sifa nzuri ambazo daima zimekuwa zikimfuata Erasto Nyoni katika maisha yake ya soka la kimafanikio nchini.

Na rekodi tamu tamu katika mchezo huo daima zinamzunguka nyota huyo wa klabu ya Simba.

Oktoba 18 alifunga bao kali la kusawazisha kwa ‘friikiki’ iliyotinga moja kwa moja kwenye lango la Wasudan katika ushindi wa Taifa Stars wa 2-1 ugenini Khartoum na kuisaidia Tanzania kufuzu kwa fainali zao za pili za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa Ligi za Ndani (Chan) 2020.

Rekodi ya kuvutia ni kwamba Nyoni ndiye mchezaji pekee katika kikosi hiki cha Stars kilichofuzu fainali za pili 2020 ambaye alikuwamo katika kikosi kile kilichofuzu fainali za awali 2009.

Mwanaspoti lilizungumza na kiraka huyo wa Simba ambaye alifunguka mengi kuanzia maisha yake ya soka yalipoanzia hadi sasa.

MCHEZAJI PEKEE ALIYESALIA KATIKA KIKOSI KILICHOFUZU 2009

Pia Soma

Advertisement
Nyoni ni mchezaji pekee ambaye alikuwamo katika kikosi kilichofuzu fainali za Chan 2009 zilizofanyika kwa mara ya kwanza nchini Ivory Coast baada ya kuanzishwa kwa michuano hiyo. Stars iliwang’oa Wasudan hao hao ili kufuzu.

Na sasa kuelekea fainali zijazo za 2020 zitakazofanyika nchini Cameroon, bao lake nchini Sudan liliwarejesha wachezaji wenzake kwenye morali na kuibuka na ushindi wa 2-1, shukrani kwa bao la ushindi la Ditram Nchimbi lililoisaidia Stars kusonga mbele kwa faida ya mabao ya ugenini baada ya kulala 1-0 nyumbani Dar es Salaam katika mechi ya mkondo wa kwanza ya kufuzu.

“Mimi binafsi nafurahi sana unajua kazi yetu ni ngumu sana na unapopata bahati hii ni jambo la kumshukuru Mungu sana,” alisema Nyoni kuhusu bao lake hilo muhimu dhidi ya Sudan .

SIRI YA KUCHEZA MUDA MREFU

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alimkataza Nyoni na Kelvin Yondani kustaafu kuichezea timu ya Taifa baada ya wawili hao kutangaza kujiweka ndano ya soka la kimataifa baada ya fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2019 nchini Misri ambako Stars ilipoteza mechi zote tatu za hatua ya makundi.

Nyoni ambaye vitabu vinaonyesha ana umri wa miaka 32, anasema siri yake ya kucheza soka kwa muda mrefu na kwa kiwango cha juu ni kufanya mazoezi kwa bidii na kutambua kwamba mpira ni kazi yake, hivyo anapata muda wa kupumzika na kujitunza.

“Mimi ni nina familia, kwahiyo naishi ndani ya familia yangu, naheshimu na sina mambo mengi, nazungumzia kwamba kuna vitu ambavyo nilivipunguza kwa spidi mpaka kufikia kuviacha, mambo ya kwenda disko na starehe nyingine niliviacha kabisa,” anasema.

CHANGAMOTO HAZIJAMKATISHA TAMAA

Nyoni anasema katika maisha yake marefu ya soka amekutana na changamoto nyingi lakini hazikuwahi kumkatisha tamaa.

“Mpira wetu una mambo mengi sana kuna muda unatamani kuachana nao, lakini hii ni kazi yetu, inabidi tupambane na hicho ndicho kitu kilichonifanya nisikate tamaa. Nimepitia changamoto nyingi, nikisema nizielezee nitaandika kitabu kabisa, lakini ukweli ni nyingi,” anasema.

CHEKI ALIVYOTUA AZAM KIFALME NA KUCHOMOKA KIWEPESI

Nyoni anasema akiwa yupo nchini Burundi huku akiwa ameshacheza takribani miaka mitatu nchini humo, viongozi wa Azam walimtuma mtu wao na kwenda kuzungumza naye.

“Alikuja mtu wa Azam ambaye alikuwa ananifuatilia, akanambia kwamba kuna timu imepanda Ligi Kuu nyumbani na inanihitaji. Mwisho wa siku nikaamua kurudi nyumbani,” anasema.

Anasema Ligi ya Burundi sio yenye ushindani kama Tanzania hivyo ilipokuja ofa hiyo aliona hana nafasi ya kusita zaidi ya kurejea.

“Maisha ya Azam yalikuwa mazuri kwa wakati ule, lakini pia kulikuwa na changamoto nyingi kwasababu timu ilikuwa na wachezaji wengi kutoka Kenya na Uganda kwahiyo tulikuwa na ushindani mkubwa wa namba, lakini nilipambana na kuweza kupata namba na kiukweli nilicheza sana” alisema.

Licha ya kucheza kwa muda mrefu na mafanikio akiwa na Azam, Nyoni anasema sababu kubwa ya yeye kuondoka ni baada ya mkataba wake kumalizika na uongozi kuanza kumzungusha katika kukaa chini na kujadili mkataba mpya.

“Wao walisema kwamba hawahitaji tena huduma yangu kwahiyo ikabidi niondoke, nadhani nilifungiwa riziki yangu na Mwenyezi Mungu akanifungulia sehemu nyingine ndivyo ilivyo mpaka hivi sasa,” alisema.

“Nisingeweza kulazimisha kubaki pale, riziki ilishafungwa,”

YANGA YASUASUA KUMSAJILI, SIMBA WAMALIZA MCHEZO

Baada ya kuachana na Azam kwa kumuacha hewani, Nyoni alipokea ofa kutoka Simba na Yanga wote wakitaka huduma yake.

Wakati anapokea ofa hizo Yanga walionekana kama bado wanajiuliza. Wakati huo huo, wapinzani wao Simba hawakuwa na maneno mengi zaidi ya kuweka mzigo mezani na kumalizana naye.

“Unajua mimi mpira ni kazi yangu, inategemea nani alikuwa ananihitaji kwa moyo wote na kitu kilichokuwepo Simba walikuwa wananihitaji kweli, tulipozungumza nilimalizana na Simba,” anasema.

Anaongeza Yanga walikuwa wanazungumza bila ya vitendo tofauti na Simba ambao walipopanga muda na siku walienda kuzungumza na kumalizana.

SIRI YA KUCHEZA STARS MFULULIZO

Nyoni amekuwa ni mchezaji anayeitwa mara kwa mara katika kikosi cha timu ya Taifa Tanzania licha ya kubadilishwa mara kwa mara makocha wake.

Yeye anafichua siri ya kuitwa mara kwa mara katika kikosi cha Stars, kwamba ni kujituma na kuwa na maelewano mazuri ndani ya uwanja na wachezaji wenzake.

“Nashukuru sana viongozi kwa kunipa nafasi, lakini kubwa zaidi ni mimi mwenyewe kujitambua na kujituma pale ninapopewa nafasi na pia kumsikiliza kocha anataka nini nifanye,” anasema.

AJIPANGA KUZUNGUMZA NA MAKONDA ILI ASTAAFU

Kutokana na umri na mafanikio aliyoyapata kama mchezaji akishiriki fainali za Chan 2009, Afcon 2019 na kuiwezesha nchi yake kufuzu fainali za Chan 2020, Nyoni sasa anapiga hesabu za kustaafu kuitumikia timu yake ya taifa ili awapishe wengine.

Awali Makonda aliwazuia kustaafu yeye na beki Yondani baada ya kusikia wanataka kuachana na Stars.

Erasto anasema: “Mkuu wa Mkoa ni mkubwa wangu, mpango wangu wa kustaafu ukiwadia lazima nitaenda kumshirikisha tuone inakuwaje, sasa hivi kuna vijana wengi wanakuja na wanahitaji kucheza, hivyo kama nitaendelea kuwepo basi nikae pembeni niwaangalie vijana wakicheza,” anasema.

Anaongeza ni muda sahihi wa vijana kuanza kupewa nafasi ili wapate uzoefu ili hata atakaposema anaachana na soka la kimataifa, basi vijana wawe wameiva.

“Vijana wanafundishika vizuri, unachowaelekeza uwanjani huwa wanafanya, kwahiyo ni jambo zuri, kuanza kuwapa nafasi sasa.”

GOLI LAKE DHIDI YA SUDAN NI KICHEKO

Nyoni anasema goli lake alilofunga dhidi ya Sudan ni moja ya mabao yake muhimu zaidi katika maisha yake ya soka.

Anasema: “Nina furaha kwasababu nimeifungia nchi yangu goli muhimu, kikubwa namuomba Mwenyezi Mungu azidi kunipa afya njema ili niweze kufanya kazi yangu vizuri.”

FAMILIA YAKE

Erasto ni mzazi mwenye watoto watatu, wa kwanza ni Naila mwenye umri wa miaka 9, wa pili ni Nekla mwenye miaka mitatu na wa tatu ni Riyan mwenye miezi saba.

Chanzo: mwananchi.co.tz