MSHAMBULIAJI kiongozi wa Azam FC raia wa Zimbabwe, Prince Dube amesema kuwa hesabu zake amezihamishia katika mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam ili kuisaidia timu yake kucheza nusu fainali.
Dube ambaye hadi sasa amepachika mabao 14 na kuwa kinara katika orodha ya wafungaji wa Ligi Kuu Tanzania Bara ameweka wazi kuwa sasa akili na nguvu zake anahamishia katika michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam.
Akizungumza na gazeti hili, Dube alisema kuwa hivi sasa akili yake ipo katika mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam dhidi ya Rhino Rangers, iliyokuwa ikishiriki Ligi Daraja la Kwanza.
“Tuko vizuri na tunaendelea na mazoezi kwaajili ya mchezo ujao, nipo hapa kwaajili ya kuipambania timu yangu pamoja na kutimiza malengo yangu na klabu.
“Kila mtu anafanya kitu kwa malengo fulani nipo hapa kwaajili ya kuipambania Azam FC, ambayo imeonesha imani juu yangu naamini tunaenda kushinda na mchezo huu,” alisema Dube.
Alisema kuwa anaamini utakuwa mchezo mgumu kwake, kwani hii ni mara ya kwanza kukutana na timu hiyo lakini kazi yake iliyomleta hapa nchini ni kufunga na kuisaidia timu yake kutimiza malengo waliyojiwekea, ikiwemo kutwaa mataji.