Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dk Ndee: Niko tayari kusaidia riadha

96fde8602f793560aed3b2b234bee3eb.png Dk Ndee: Niko tayari kusaidia riadha

Thu, 4 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

KIONGOZI wazamani wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) amesema kuwa yuko tayari kusaidiana na uongozi mpya uliongia madarakani kuendeleza riadha.

Akizungumza katika mahojiano maalum na gazeti hili jijini Dar es Salaam juzi aliyekuwa Makamu wa Pili wa Rais wa RT anayeshughulikia ufundi, Dk Hamad Ndee alisema kuwa yuko tayari kushirikiana na uongozi mpya.

Dk Ndee aliyetaka kugombea tena, alitangaza kujitoa katika dakika za mwisho akidai kuwa hakuwa na jibu la kuwapa wapiga kura, endapo wangemuuliza sababu za uongozi wao kushindwa kuleta maendeleo ya mchezo huo.

Alisema yeye alijitoa kugombea riadha, lakini hajajitoa katika riadha, hivyo yuko tayari kuendelea kusaidia riadha kwa upande wa ufundi ili kusonga mbele.

Alisisitiza kuwa kama alivyosema awali kuwa uongozi wao katika kipindi chote cha miaka minne haukuwa na ushirikiano, hivyo hakuwa na jibu la kutoa kwa wapiga kura na ndio maana akaamua kujitoa.

Alisema kuwa hawakuwa na ushirikiano kwani baadhi ya viongozi wa juu wakipigiwa simu walikuwa hawapokei, huku akikiri kuwa Kamati ya Utendaji ilikutana mara chache sana wakati ilitakiwa kukutana mara nne kwa mwaka.

Alisema hakukuwa na sababu yoyote ya kutokutana ila kikubwa ni kwa uongozi kutokuwa na ushirikiano na kila mtu alikuwa akifanya kazi kivyake vyake tu.

Alisema kuwa mwenyekiti alikuwa haitishi vikao, hivyo yeye pamoja na kuwa ni mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi asingeweza kufanya lolote kama vikao haviitishwi.

Alisema kuwa hakuridhika kabisa na upande wa RT kuwaandaa walimu wa mchezo huo, kwani kuna uhaba mkubwa licha ya kujitahidi kutafuta fedha, lakini fedha zilipofika zilitumika tofauti.

“Pesa zililetwa kama Dola 100,000 kwa ajili ya mafunzo ya makocha, lakini zilipofika matumizi yalikuwa tofauti kabisa, matumizi yalikuwa tatizo, kwani fedha hazikutumika kama zilivyotakiwa, “alisema Dk Ndee, ambaye ni mhadhiri mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Pia alisema kuwa kwa ujumla uongozi uliopita haukutakiwa kugombea tena, labda kwa mtu mmoja mmoja kutokana na juhudi zake binafsi, lakini sio kwa ujumla wake.

Chanzo: habarileo.co.tz