Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dk Mwakyembe asema kiu yake ni Afcon 2019

34203 Pic+mwakyembe Tanzania Web Photo

Tue, 1 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Hatimaye siku 365 za mwaka 2018 zinakamilika saa sita usiku leo na kesho tunaanza mwaka mwingine. Ni saa chache tu zimesalia kusherehekea mwaka mpya wa 2019.

Mataifa ya Australia wenyewe ikifika saa 6:00 mchana watakuwa wameshaingia mwaka mwingine kutokana na mzunguko wa dunia inayozunguka kwenye mhimili wake, hapa inakamilisha saa hizo.

Ukiachana na hayo, mwaka huu unaomalizika leo haukuwa na mafanikio makubwa katika michezo, kuna maeneo kuna yaliyofanyika lakini maeneo mengine, kwa kiasi kikubwa hayakuwa mazuri. Ni mlolongo mrefu wa matukio ya michezo.

Mwaka 2019 unaoanza kesho, ni mwaka ambao familia za michezo nchini zinautazamia kuwa wa kipekee, mwaka utakaoiweka Tanzania kwenye rekodi nyingine endapo Watanzania watajipanga na kujiandaa kuweka rekodi hiyo.

Pamoja na hayo, tunataka kusikia mapya, kauli za kujipanga zimeshafunikwa mwaka huu.

Kila tunapopoteza, kinachofuata tunajipanga....

2018 mambo yalikuwa hivi

Alipoingia madarakani kuchukua nafasi ya Nape Mosses Nnauye ambaye uteuzi wake ulitenguliwa na rais John Magufuli, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harisson Mwakyembe alisema anataka kuicha michezo ikiwa mahali salama kabla ya kumaliza muhula wake 2020.

Mwaka 2018, haukuwa wa mafanikio makubwa kwenye sekta ya michezo, licha ya kuwa na baadhi ya maeneo kama nilivyogusia hapo juu. Mwaka huu ni mwaka ambao mwanariadha, Alphonce Simbu alitwaa medali ya shaba ya dunia na bondia Hassan Mwakinyo kuweka rekodi nchini Uingereza, wengine hawakufanya maajabu.

Ukiachilia mbali hayo, wanariadha, Failuna Abdi, Stephano Huche , Ezekiel Ngimba na Agostino Sulle ambao waling’ara kwenye mbio za binafsi na kufuzu kuiwakilisha Tanzania kwenye mbio za dunia.

“2018 ulikuwa ni mwaka wa kusafisha njia kwenye michezo, tulipamba ili kuvirejesha kwenye mstari baadhi ya vyama ikiwamo Kamati ya Ngumi za kulipwa (TPBRC) na Shirikisho la ngumi za Wazi (OBFT),” anasema Dk Mwakymbe.

Anasema mkakati huo umesaidia kwa kiasi kikubwa kuweka hamasa kwenye michezo na hata kurejesha imani kwa Watanzania katika ushindani wa kimataifa.

“Tumeona mafanikio kadhaa mwaka 2018, binafsi niliwaongoza Watanzania kumpokea Alphonce Simbu aliporejea na medali ya shaba ya dunia, japo ni wa tatu lakini ni mwanzo na mwakani atafanya makubwa zaidi.

Pia Mwakinyo alitikisa dunia kule Uingereza alipomchapa bondia namba nane kwa ubora duniani kwenye uzani wa super welter, Sam Eggington,”.

Msikie Waziri Mwakyembe na mkakati wa 2019

Waziri Mwakyembe anauita ni mwaka wa Tanzania kuonyesha makeke Afrika, kuandika rekodi na kuirejesha kwenye ramani ya ushindani wa kimataifa katika michezo.

Mwaka 2019, Tanzania itakuwa mwenyeji wa mashindano ya Afrika (Afcon) kwa vijana. Hapa ndipo tunapotaka kuonyesha dunia kuwa Tanzania ni ya namna gani. “Ifike hatua hata CAF wenyewe watamani mashindano mengine na mengine yafanyike Tanzania, huu ndio mpango ambao tunataka kuuweka. Tutaweka nidhamu kwa kila atakayekuja kuionyesha sura ya Tanzania.”

Waziri Mwakyembe anasema: “Serikali itapeleka timu kuchuana kwenye Michezo ya Afrika (All African Games) nchini Morocco. Michezo ya Afrika lazima iiletee Tanzania heshima kwa kuwa kuna wanariadha wenye sifa na hadi kufikia michezo hiyo watakuwa wameimarika.”

Mwaka 2019, baada ya droo juzi Ijumaa, Simba itakuwa na kazi ya kusaka heshima ya Tanzania na kama vipi kuisimamia kuhakikisha inafanya vizuri katika mechi zake na hata kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kufuzu hatua ya makundi.

Mpango mwingine ambao Waziri Mwakyembe ameusema ni kuipigania Taifa Stars kwa hatua iliyobaki kuhakikisha inacheza fainali za Afrika ambazo zitafanyika Afrika Kusini. Cameroon imepokwa uwenyeji wa michuano hiyo ya Afcon.

Kama haitoshi, timu ya riadha itakwenda kutetea medali yake ya shaba iliyoshinda mwaka 2018 kwenye mbio za dunia zitakazofanyika Qatar na hadi mwaka 2018 unaelekea ukingoni, nchi ina uhakika wa kupeleka wanariadha wanne ambao tayari wamefikia viwango, na wengine wakitarajiwa kufuzu mwaka 2019.

“Safari ndiyo inaanza, Serikali tutakuwa bega kwa bega na timu hizi kuhakiksha zinafanya vizuri Afrika, hakuna kinachoshindikana tukiamua,” anasisitiza Waziri Mwakyembe.

Anasema furaha yake ni kumaliza kipindi chake cha uwaziri akiicha Tanzania na mataji makubwa ya Afrika na dunia na anaamini ndoto hiyo itatimia mwaka 2019 unaonza kesho Jumanne.

Safari ya mafanikio

Timu za riadha, ngumi, soka, kuogelea na judo ni miongoni mwa zinazopewa nafasi ya kuiwakilisha Tanzania kwenye michezo ya Afrika (All African Games) itakayofanyika nchini Morroco.

Hata hivyo, timu hizo zinapaswa kufikia viwango vya nchi ili kupata nafasi hiyo, huku Taifa Stars yenyewe ikihitaji ushindi kwenye mchezo wake wa mwisho wa makundi dhidi ya Uganda ili kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kufuzu kucheza fainali za Afcon mwaka unaoanza kesho.

Stars itacheza na Uganda jijini Dar es Salaam siku 90 kuanza sasa, wakati Simba yenyewe itaanza hatua ya makundi baadaye Januari ambapo itacheza mechi tatu za nyumbani na tatu za ugenini kusaka tiketi ya robo fainali.

Huku Serengeti Boys yenyewe ikiwa nyumbani kusaka taji la Afrika kwa vijana, mashindano ambayo yatafanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Aprili 14 hadi 28.

“Nina imani kubwa na vijana wa Serengeti Boys ambao watatuwakilisha kwenye Afcon ya vijana watatuwakilisha vizuri, lakini pia timu ambazo zinatarajiwa kutuwakilisha kwenye

‘All African Games’ hata kwa Stars bado nafasi ipo. “Simba nayo imeonyesha matumaini makubwa kimataifa, hii ni dalili njema kwa Tanzania,” anasema.

Wasikie wasaidizi wa Mwakyembe sasa

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini, Yusuph Singo anasema mkakati waliouweka 2018 ndiyo utawapa matokeo chanya 2019.

“Tulikubaliana ni bora tujitoe kimataifa, lakini si kupeleka timu isiyokuwa ya ushindani, eti ili mradi Tanzania tuonekane tumeshiriki, hii mbinu iliviamsha vyama vingi,” anasema Singo.

Anasema kingine ambacho kiilikuwa kikwazo ni vyama kufuata Katiba zao, mfano ishu ya uchaguzi wa Yanga, kulikuwa na mgogoro mkubwa kwenye ngumi na baadhi ya vyama kufanya vyama vya michezo kama mali zao, tulianza kukata mizizi yote hiyo na sasa kila kitu kiko sawa,” anasema.

Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Alex Nkenyenge anasema, kilichokuwa kinachelewesha maendeleo ni migogoro ndani ya vyama vingi.

“Ilifikia mahali badala ya kufikiria maendeleo, tunafikiria kutatua migogoro, lakini kila kitu kilisimamiwa na tulipoona mambo hayaendi ilibidi tusimame kidete ili kuweka mambo sawa, ndiyo sababu kwa kiasi fulani 2018 michezo yetu ilikaa kwenye mstari.

“Tunaelekea 2019, msimano ni ule ule, tunahitaji mafanikio ya michezo, tunahitaji kuona wadhamini wanamiminika kwenye vyama vyetu vya michezo, lakini ili wajitokeze ni mafanikio ya timu, kwa msingi tuliouanza bila shaka mafanikio zaidi yanakuja,” alisema Nkenyenge.

Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) yenyewe kilio chake kikuu kwa vyama vya michezo ni kuwasilisha mipango kazi yao ya 2019 kwenye kamati hiyo mapema endapo vinahitaji msaada wa TOC. “Mwaka 2018 mwitikio kwa vyama vya michezo ulikuwa hasi, lakini vyenyewe ndivyo vilijinyima fursa, kwani TOC imekuwa ikitoa misaada mbalimbali ya hali na mali kwa vyama ambavyo viko chini yake, lakini pale tu vinapoleta mipango mikakati yao mapema kwetu,” anasema Katibu Mkuu wa TOC, Filbert Bayi.



Chanzo: mwananchi.co.tz