Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dalali, Mo wachomoza Simba

25005 MO+PIC%255D TanzaniaWeb

Thu, 1 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Zikiwa zimebaki saa 72 kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Simba kufanyika, majina ya mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji ‘Mo’ na aliyekuwa mwenyekiti wa zamani wa klabu hiyo, Hassani Dalali yanatumika kama kete muhimu kwa wagombea kuwashawishi wapigakura.

Tangu kampeni kwa wagombea zilipozinduliwa rasmi Jumapili iliyopita hadi sasa ambapo zimebaki siku tatu kabla ya uchaguzi kufanyika, idadi kubwa ya wagombea wamekuwa wakiyataja mara kwa mara majina ya Dewji na Dalali wakiamini kuwa watafanikiwa kuwashawishi wanachama kuwapigia kura katika Uchaguzi Mkuu wa Novemba 4 utakaofanyika, Dar es Salaam.

Wakati Mo ana heshima kubwa ndani ya klabu hiyo baada ya kushinda zabuni ya uwekezaji kwa asilimia 49 ambapo klabu hiyo itaendeshwa kwa mfumo wa kampuni, Dalali ni miongoni mwa viongozi wenye ushawishi na mafanikio Simba.

Wagombea wameamua kuwatumia wawili hao kama daraja la kuwapeleka katika Bodi ya Simba ambayo itajumuisha wajumbe sita watakaochaguliwa kutoka upande wa wanachama.

Katika midahalo iliyofanyika juzi na jana ikihusisha matawi ya Simba Wilaya za Temeke, Kigamboni, Kinondoni, Ubungo na kampeni ambazo wamekuwa wakifanya kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, wagombea hao wameonekana kubuni mbinu ya kutumia majina ya Mo na Dalali ili kunufaika siku chache kabla ya uchaguzi huo.

“Utawala wangu mimi na Mzee Hassani Dalali ndio uliifanya Simba iwe na ekari 25 za ardhi kule Bunju. Pia ndio uliingia mikataba na kampuni mbalimbali kama TBL ambapo leo hii Simba ina basi la kisasa.

“Lakini pia mimi na Dalali, ndio viongozi pekee ambao uongozi wetu uliweza kuunganisha wanachama, mashabiki na wapenzi wa Simba, Tanzania nzima hadi tukaweza kutwaa ubingwa na mafanikio mengine,” alisema Mwina Kaduguda.

Mgombea ujumbe ambaye ni Mhadhiri wa Shule ya Sheria Tanzania, Wakili Hussein Kitta alisema yeye ni mtu sahihi kuingia kwenye Bodi ya Simba kwa kuwa atapata fursa ya kushauri na kuanzisha mipango mbalimbali itakayompa faida mwekezaji na klabu.

“Anawekeza mwekezaji kiasi cha Sh 20 bilioni, nia yake ni apate faida ya kile alichowekeza, pia Simba ifike mbali kimaendeleo. Kwa hiyo kunahitajika watu wenye mipango mizuri kama mimi, ili fedha hizo ziweze kusimamiwa vizuri, mwekezaji apate faida na klabu pia inufaike,” alisema Kitta.

Mgombea mwingine wa nafasi ya ujumbe, Dk Zawadi Kadunda alisema uwekezaji wa Mo na mafanikio ya Simba yanahitaji watu wenye upeo wa ubunifu wa miradi na wenye uchungu wa Klabu ya Simba kama yeye ili fedha iliyowekezwa iwe na faida.

“Hivi Simba leo hii ikianzisha Benki ya Biashara ikaitwa kwa jina lake itashindwa? Je Simba ikitengeneza viberiti vikauzwa kwa kutumia jina lake itashindwa?,” alihoji Dk Kadunda.

“Mimi naamini kuwa mwekezaji na mwanachama mwenzetu wa klabu ya Simba, Ndugu Mohammed Dewji ana nia nzuri hivyo atateua watu makini na wenye weledi wa hali ya juu, hivyo ni lazima sisi huku upande wa wanachama tupate watu ambao wana hekima, busara na weledi ili tuisadie klabu yetu isonge mbele na kupata mafanikio nje na ndani ya uwanja,” alisema mgombea wa nafasi ya ujumbe, Abdallah Migomba.

“Nimefurahi kuona kampeni zinafanyika kistaarabu wagombea hawatoleani lugha za kashfa. Wito wangu kwa wanachama ni kuchagua watu ambao wataifanya timu yetu ipate maendeleo ndani na nje ya uwanja,” alisema Dalali

Hata hivyo, Dalali alionyesha kuwaunga mkono wagombea Swedi Mkwabi anayewania nafasi ya Mwenyekiti na wajumbe Patrick Rweyemamu, Hussein Kitta, Dk Mohammed Wandi, Hamisi Mkoma, Juma Pinto, Dk Zawadi Kadunda na Asha Baraka ambao amekuwa akitembea nao kila kona kuwaombea kura za ndio.

Charles Abel, Mwanahiba Richard, Thobias Sebastian

Chanzo: mwananchi.co.tz