Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dakika hizi moto Simba, Yanga

90595 Derby+pic Dakika hizi moto Simba, Yanga

Thu, 2 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati homa ya mchezo wa watani wa jadi Simba na Yanga ikiendelea kupanda huku zikiwa zimebaki siku chache, dakika 45 za kipindi cha pili zinaonekana kuwa ni moto katika safu zao za ushambuliaji.

Simba ambayo itakuwa mwenyeji, itaikaribisha Yanga katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Jumamosi wiki hii.

Takwimu za timu hizo zinaonyesha safu zao za ushambuliaji zimekuwa na makali dakika 45 za kipindi cha pili ingawa Simba inaonyesha iko vizuri pia dakika 45 za mwanzo.

Simba katika mechi 10 zilizopita imefunga mabao 10 kipindi cha pili dakika ya 46,90, 49, 57, 65, 47, 75, 49, 78, 87. Kipindi cha kwanza imefunga mabao 10 dakika ya 41, 23,55, 79, 5, 35 40, 8, 44 na 11 wakati mabeki wameruhusu bao moja dakika ya 33.

Yanga nayo imekuwa moto kipindi cha pili na mabao manane ilifunga dakika ya 85, 72, 75, 57, 65, 68,71, 56 na kipindi cha kwanza mabao sita dakika ya 4,25, 11, 22, 35 na 6.

Mabeki wameruhusu mabao matano kipindi cha pili dakika ya 90, 55, 55, 58 na 87 na kipindi cha kwanza imefungwa matatu dakika za 13, 45 na 34.

Hata hivyo, inaonekana ni bora zaidi kulinganisha na Yanga katika rekodi ya washambuliaji wake katika kufunga mabao tangu ligi hiyo ilipoanza Agosti 24, mwaka jana.

Katika mechi hizo 10 mshambuliaji raia wa Kigeni, Meddie Kagere amefunga mabao sita akifuatiwa na Miraji Athumani aliyepachika manne. Hata hivyo Kagere anaongoza kwa kufunga mabao tisa na Miraji sita katika mechi zote msimu huu.

David Molinga na Patrick Sibomana wamekuwa na mchango Yanga katika mabao 14 waliofunga timu hiyo, kila mmoja amepachika manne. Huenda mshambuliji mpya Ditram Nchimbi mwenye mabao matatu akicheza mchezo wa Jumamosi.

Rekodi

Simba katika mechi 10 imefungwa mechi moja, imetoka sare moja, imeshinda nane mabao 2-0 dhidi ya KMC, iliichapa Lipuli 4-0, iliifunga Mbeya City 3-0, ilizichapa Ruvu shooting na Kagera 2-0, ilizilaza Biashara United 1-0, Azam na Singida, imefungwa 1-0 na Mwadui na kutoka suluhu dhidi ya Tanzania Prisons.

Katika mechi 10 za mwisho, Yanga imeshinda saba, suluhu tatu na ilishinda bao 1-0 dhidi ya Biashara United, Tanzania Prisons, Ndanda, Coastal Union, iliilaza Mbao mabao 3-2 ilizichapa JKT Tanzania 2-1 na Alliance. Ilitoka suluhu na Mbeya City ilitoka sare ya bao 1-1 na KMC kabla ya mabao 3-3 dhidi ya Polisi Tanzania.

Yanga katika mechi 10 safu ya ushambuliaji imefunga mabao 14 na mabeki wameruhusu manane.

Simba katika mechi 10 safu ya ushambuliaji imefunga mabao 20 na mabeki wameruhusu bao moja.

Kauli za Wadau

Mwenyekiti wa zamani wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Idd Kipingu alisema ingawa mechi hiyo haitabiriki, lakini Simba iko vizuri kulinganisha na Yanga.

“Tusubiri dakika 90 lolote linaweza kutokea ingawa mechi ya watani ambayo huwezi kutabiri,”alisema Kipingu.

Mchambuzi Ally Mayay alisema mechi hiyo ni ngumu kwa pande zote ingawa anatarajia matokeo ya timu hizo kutoka sare ya aina yoyote.

Bondia wa ngumi za kulipwa Mada Maugo alisema anaipa ushindi Simba na aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta), Anna Kibira alisema Yanga ina nafasi nzuri ya kupata pointi tatu dhidi ya wapinzani wao.

Chanzo: mwananchi.co.tz