Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dakika 180 zaimaliza KMC

Dakika 180 zaimaliza KMC

Mon, 11 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mbinu za kiufundi zilizofanywa na kocha Mwinyi Zahera katika mchezo wa jana dhidi ya KMC zilizaa matunda, baada ya Yanga kupata ushindi wa mabao 2-1.

Zahera alisema haikuwa kazi rahisi kupata ushindi kwasababu KMC haikuwa timu ya kubeza.

Kocha huyo alisema alitumia dakika 180 kusoma mbinu za KMC kwa kuangalia mikanda yao ya mechi zilizopita.

“Tuliangalia mikanda ya KMC kwa siku mbili kabla ya mechi, tulichokiona tulikifanyia kazi katika mazoezi,” alisema Zahera baada ya mchezo kumalizika.

Mbali na mbinu hiyo, mabadiliko aliyofanya kwa kumuingiza Ajibu yalionekana kuwa na tija kwa Yanga kwani iliongeza kasi ya mashambulizi.

Zahera alimtoa Thabani Kamusoko na kuingia Ajibu aliyebadili sura ya mchezo dakika ya 66, baada ya Yanga kupata bao la ushindi.

Ajibu alisababisha bao la pili baada ya mpira wa krosi aliokuwa akipiga kwa Heritier Makambo kuokolewa vibaya kwa kichwa na beki Ally Ally aliyeujaza wavuni.

Yanga imejikita kileleni katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kufikisha pointi 67 katika mechi 27 ilizocheza.

Azam FC inashika nafasi ya pili kwa pointi 56 sawa na idadi ya mechi za Yanga wakati Simba ipo nafasi ya 51 baada ya kucheza mechi 26.

Licha ya kupoteza mchezo KMC ilipoteza nafasi nyingi ambazo kama ingezitumia vyema ingepata ushindi katika mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jana.

Makambo hakuwa na mawasiliano na kiungo Pappy Tshishimbi baada ya kukosa bao dakika ya 10 tu ya mchezo.

Yanga ilifanya shambulizi tena dakika nne baadaye baada Kelvin Yondani alipiga kiki kali iliyotua mikononi mwa kipa Jonathan Nahimana.

KMC ilifanya shambulizi dakika ya 16 na kupata bao lililofungwa na mshambuliaji Mohammed Rashid aliyewahadaa mabeki wa Yanga na kufunga kirahisi akipokea pasi ya winga Charles Ilamfya.

Dakika ya 27 Kamusoko alifanya kazi nzuri kwa kuokoa kiki ya Ilamfya katika mstari wa goli baada ya mpigaji huyo kupokea pasi ya Hassani Kabunda.

Yanga ilisawazisha katika dakika ya 36 kwa bao likifungwa na Tshishimbi kwa mpira wa kichwa akipokea krosi ya beki wa kushoto Gadiel Michael.

Kipindi cha pili  KMC ilimtoa kipa Nahimana aliyeumia na nafasi yake kujazwa na nguli Juma Kaseja.

Dakika ya 52 Kabunda alishindwa kufunga licha ya kuwapangua mabeki wa Yanga, lakini shuti lake lilitoka nje kidogo ya lango.

Ilamfya aliyekuwa mwiba kwa mabeki wa Yanga, alikosa bao akiwa katika nafasi nzuri dakika ya 61 aliposhindwa kuunganisha mpira wa Kabunda.

Kocha wa KMC Ettiene Ndayiragije alisema wachezaji wake walifanya kosa ambalo liliwagharimu licha ya kumiliki mpira kwa sehemu kubwa ya mchezo.

Ndayiragije alisema timu yake ilitengeneza nafasi za kufunga, lakini washambuliaji wake hawakuwa makini.

Katika mechi nyingine, Mwadui Shinyanga iliichapa Mbeya City mabao 3-1.



Chanzo: mwananchi.co.tz