KAMA atashinda na kuvunja rekodi kwenye mbio za Abu Dhabi Marathoni, mwanariadha nyota wa Tanzania, Alphonce Simbu ataondoka na kitita cha dola 80,000 ambazo ni zaidi ya Sh 176 milioni Ijumaa ijayo.
Simbu ni miongoni mwa wanariadha 4000 wanaotarajiwa kuchuna kwenye mbio hizo za Novemba 26 zitakazofanyika kwenye mji mkuu huo wa falme za kiarabu.
Kocha binafsi wa Simbu, Francis John amesema mwanariadha huyo anayefanya vizuri nchini kwenye mbio ndefu za barabarani amepewa mualiko wa kushiriki mbio hizo za kilomita 42.
“Ataondoka nchini Novemba 21, atakaa Abu Dhabi kwa siku kadhaa kabla mbio,” alisema Francis na kusisitiza Simbu yuko fiti kimwili na kiakili tayari kwa mbio hizo ambazo waandaaji wametoa bonasi ya dola 30,000 (zaidi ya Sh 66 milioni) kwa atakayevunja rekodi.
Taarifa kutoka Abu Dhabi inasema dola 303,000 zimetengwa kwa ajili ya zawadi kwa mabingwa ambao kwenye mbio ya kilomita 42 washindi wataondoka na dola 50,000 (zaidi ya Sh 110 milioni) kila mmoja.
Mwanaume atakayekimbia kwa saa 2:04:40 ambayo ni sawa na dakika 124 na mwanamke atakayekimbia kwa saa 2:21:01 au chini ya muda huo kila mmoja atondoka na dola 30,000 (zaidi ya Sh 66 milioni) za bonasi.
“Naamini Simbu atafanya vizuri, mbio hizi ni kubwa na zenye pesa ambazo kama atashinda itakuwa ni faraja kwake,” alisema Francis.
Hata hivyo, Francis amepingana na baadhi ya wanariadha wa zamani ambao wameonyesha wasiwasi wa nyota huyo kukimbia mbio nyingi ndani ya muda mfupi hapa nchini kutapunguza ubora wake.
Hivi karibuni, Simbu alikimbia mbio nne tofauti ndani ya siku 30, jambo ambalo lilionekana kutoa wasiwasi kwa wadau wa riadha ambao walisema ni mbio za kumchosha na kupunguza kiwango chake.
“Alizitumia mbio hizo kama sehemu ya maandalizi kuelekea Abu Dhabi, zote zilikuwa za kilomita 21, hivyo haiwezi kumuathiri chochote, Simbu yuko fiti na kutokana na maandalizi aliyoyafanya, sina shaka atafanya vema huko Abu Dhabi,” alisema.
Muda mkali wa Simbu ni wa saa 2:08:27 ambao aliuweka mwaka 2019 kwenye mbio za Lake Biwa Marathon hivyo ili kuvunja rekodi kwenye mbio za Abu Dhabi atahitaji kupunguza dakika 4:30 zaidi ya muda wake bora zaidi.
Nyota huyo anatarajiwa kupata upinzani kutoka kwa mabingwa watetezi, Reuben Kiprop Kypiego aliyeibuka kinara akitumia saa 2:04:40 na Joel Kemboi Kimurer aliyemaliza wa pili kwa kutumia muda wa saa 2:06:21 (wanariadha hawa wote ni kutoka Kenya) na Fikadu Teferi Girma wa Ethiopia aliyemaliza wa tatu akitumia saa 2:09:16.